Mkutano kuhusu kuidhamini Palestina wafanyika Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano kuhusu kuidhamini Palestina wafanyika Berlin

Steinmeier awatolea mwito wafadhili watoe michango

Mkutano wa siku moja kwa ajili ya Palestina unaowaleta pamoja wafadhili wa kimatiafa unafanyika leo mjini Berlin hapa Ujerumani. Mkutano huo unalenga kuisaidia polisi ya Palestina na kuimarisha vyombo vya sheria.

Wajumbe kutoka nchi takriban 50 wamealikwa kuhudhuria mkutano huo na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier. Miongoni mwa viongozi mashuhuri walioalikwa ni waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni, na waziri mkuu wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Salam Fajad.

Kiongozi wa sera za kigeni wa Umoja waUlaya, Javier Solana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, pia wanahudhuria mkutano huo.

Jumuiya ya kimataifa inataka kuutumia mkutano wa Berlin kuimarisha vyombo vya sheria na polisi ya Palestina kwa uwezekano wa kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina.

Waziri Frank Walter Steinmeier ameutolea mwito mkutano huo wa wawafadhili wa kimatafia utoe fedha kuimarisha polisi ya Palestina na vyombo vya sheria. Serikali ya Ujerumani inasema mkutano huo wa siku moja ni hatua muhimu katika kufikia suluhisho la kuundwa kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina yatakayokaa kwa amani.

Mkutano wa Berlin unalenga kutafuta njia za kulifikia lengo hilo kama anavyoeleza waziri Frank Walter Steinmeier.

´Tuna mpango mpya ambao hauzingatii tu makubaliano ya amani na usitishwaji wa mapigano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Annapolis nchini Marekani, bali pia mazungumzo kati ya Israel na Syria ambayo sio ya ana kwa ana. Kwa sasa kuna mkataba wa kusitisha mapigano baina ya Israel na Palestina katika Ukanda wa Gaza na kwa hiyo nadhani tuna sababu nzuri kusaidia hali hii iliyojitokeza wiki iliyopita, bila tashuishi.´

Waziri Steinmeier pia amesema haiwezekani taifa kuendesha shughuli zake pasipo kuwepo na taasisi thabiti. Kwa kuwa Wapalestina hawana taifa lao, swala linalojitokeza ni ikiwa mkutano wa Berlin utatoa mwanya wa kuchukuliwa hatua nyengine ya kufikia lengo hilo. Waziri Steinmeier anasema hata hivyo kazi yenyewe inatakiwa kufanywa na pande zinazohasimiana.

´Kazi yenyewe inatakiwa kufanywa na pande zinazohasimiana. Lakini Ujerumani, nchi za Umoja wa Ulaya na Umoja wa Ulaya kwa ujumla, kwa pamoja zinaweza kuboresha mazingira ya kufanyika kwa mazungumzo na kwa njia hiyo kuwasaidia wapatanishi wa Palestina na Israel.´

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Berlin, kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema, ´Siasa kama tujuavyo sote, linapokuja swala la raia kuipokea vizuri, sharti ifahamike wazi. Na ndio maana serikali ya Ujerumani pamoja na mkutano huu unataka kutoa mchango kusaidia usalama wa raia na haki kwa kuwa hii, pamoja na utengamano, ni msingi wa kufaulu kwa utawala wa kidemokrasia. Mkutano huu wa Berlin unajadili ujenzi wa msingi huo.´

Huku Ujerumani ikitazamia kutoa kiasi cha dola milioni 180 za kimarekani kudhamini miradi ya ujenzi wa mahakama na magereza, mazungumzo ya kisiasa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati yanatarajiwa kufanyika kandoni mwa mkutano huo.

Wapatanishi wa pande nne zinahosukia na mpango huo wa amani zikiwemo Umoja wa Ulaya, Urusi, Umoja wa Mataifa na Maremkani, wanatarajiwa kukutana baadaye leo mjini Berlin.

 • Tarehe 24.06.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQ1A
 • Tarehe 24.06.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQ1A
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com