1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu biashara ya binadamu wafanyika nchini Austria

Thelma Mwadzaya13 Februari 2008

Wajumbe wanajadili njia za kupambanana biashara hiyo haramu

https://p.dw.com/p/D77M
Antonio Maria Costa, mkurugenzi mtendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na dawa za kulevya na uhalifuPicha: AP

Kwa mujibu wa wanaharakati washiriki wa biashara hiyo haramu hupata faida ya dola bilioni 31.6 kwa mwaka.

Katika mkesha wa kikao hicho Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC, Antonio Maria Costa, alitoa wito wa kusambazwa kwa maelezo zaidi kuhusu uhalifu huo ulioenea kote ulimwenguni na kusababisha kutotambulika kwake.

Bwana Costa anaeleza kuwa uhalifu huo una maumbo tofauti na hufanyika katika shughuli zinazopigwa marufuku mfano uhamiaji haramu, kazi ya kulazimishwa, mazingira ya vita, unyanyasaji wa watoto vilevile ukahaba.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake unaeleza kuwa hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kupambana na biashara hiyo haramu huku serikali zikitimiza wajibu wake.

Biashara haramu ya kusafirisha binadamu inayojumuisha biashara ya ukahaba au matumizi ya watoto katika vita ni uhalifu unaofanyika ulimwenguni na kuwa katika viwango sawa na vitendo vya mateso na utumwa. Hata hivyo hali halisi ya uhalifu huo haifahamiki.

Kiongozi wa Shirika hilo la Umoja wa Matiafa anatoa wito kwa serikali kutilia kasi utekelezaji wa makubaliano ya Palermo yatakayowezesha hatua za kisheria kuchukuliwa aidha kuwatendea haki wahanga.

Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya kimataifa walioko mjini Vienna wanatia juhudi ili kusambaza maelezo zaidi kuhusu biashara hiyo haramu kwa upande mwingine kushinikiza mataifa ambayo hayajachukua msimamo mkali.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa mataifa mhalifu mmoja pekee huchukuliwa hatua za kisheria kwa kila watu 800 waliosafirishwa kimagendo.

Kongamano hilo la Vienna linatilia mkazo zaidi mada tatu muhimu katika biashara haramu ya kusafirisha binadamu ikiwa ni pamoja na vyanzo vyake, athari za kijamii na kiuchumi vilevile hatua za kuchukua ili kupambana na uhalifu huo.

Mkutano huo unanuia kujadili mazingira na sababu zinazofanya watu kuwa katika hatari ya kutumiwa katika uhalifu huo mfano umasikini, unyanyasaji wa kijinsia, vita, kutengwa kwa misingi ya kidini, kikabila au ubaguzi.

Wakati huohuo athari za biashara hiyo haramu nazo zitajadiliwa hasa yakifahamika mazingira ambayo huenda yakatishia maisha ya wahanga.

Mkutano huo unafanyika chini ya uandalizi wa Kitengo cha Umoja wa mataifa cha kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu UN.GIFT.

Kitengo hicho kilizinduliwa rasmi mwezi Machi mwaka jana na Shirika la Umoja wa mataifa la kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu UNOCD.