1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu amani ya Mashariki ya Kati waanza leo Annapolis

27 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CTXi

Mkutano kuhusu amani ya Mashariki ya Kati unaanza leo huko Annapolis katika jimbo la Maryland nchini Marekani.

Viongozi wa Israel na Palestina wanaohudhuria mkutano huo wameeleza matumaini yao kwamba makutano huo huenda uyafufue mazungumzo ya amani yaliyokwama.

Rais George W Bush wa Marekani

ameahidi msaada wa serikali yake katika kutafuta suluhisho la mataifa mawili. Amewakaribisha viongozi kutoka nchi karibu 50 na mashirika mbalimbali kwenye chakula rasmi kilichaondaliwa kwa ajili ya wageni mjini Washington.

Akimkaribisha waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert rais Bush amesema,

´Ni heshima kuwa nawe tena katika ikulu, asante kwa kuja kwenye mkutano wa Annapolis. Natazamia kuendelea na mazungumzo muhimu pamoja nawe na rais wa mamlaka ya Palestina kuona ikiwa amani inawezekana. Nina matumaini, na ninajua hata ninyi pia mna matumaini. Nataka niwashukuru kwa ushujaa na urafiki wenu, Najivunia kwa sababu yenu.´

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema anafuraha kwa kualikwa kwenye mazungumzo ya Annapolis na amemshukuru rais Bush na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, kwa kuuandaa mkutano huo.

´Nina furaha kwa kuwa nimekuja pamoja na wenzangu kwa mara nyingine katika ikulu. Natumai tutaanzisha mchakato mpya wa mazungumzo ya maana kati yetu.´

Hapo awali rais Bush alikutana na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, wakati tofauti.

Mkutano wa mjini Annapolis unaanza leo katika juhudi kubwa ya kuyafufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Wapalestina katika kipindi cha miaka saba.