Mkutano kuhusu amani ya Afghanistan washambuliwa na Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano kuhusu amani ya Afghanistan washambuliwa na Taliban

Washambuliaji wa kujitoa muhanga maisha wa kundi la Taliban waliokuwa wamejihami na makombora leo wameushambulia mkutano kuhusu amani ya Afghanistan, ulioandaliwa na rais wa nchi hiyo, Hamid Karzai, mjini Kabul

Makombora yamelipuka na milio ya risasi kusikika karibu na hema kubwa mjini Kabul ambapo mkutano kuhusu amani ya Afgahanistan unafanyika. Rais wa nchi hiyo Hamid Karzai, alikuwa akiwahutubia wajumbe 1,600 na wanadiplomasia wa nchi za magharibi wakati wa mashambulio hayo.

Mkutano huo wa siku tatu ulioanza leo mjini Kabul, unalenga kutafuta njia ya pamoja ya kuvimaliza vita vya takriban miaka tisa nchini humo.

Maafisa wanasema washambuliaji hao walikuwa wamevalia mikanda ya vifaa vya kulipuka na mavazi ya kike aina ya burqa, yanayoufunika mwili mzima hadi miguuni na kutatiza ufunguzi wa mkutano huo uliokuwa ukilindwa na maafisa 12,000 wa usalama. Hata hivyo shambulio hilo limetibuka.

Mshipa haukumpiga rais Karzai, bali alisimama kiume kuuhutubia mkutano huo, huku akiwatolea mwito wajumbe wamshauri kuhusu njia za kuikomboa Afghanistan kutokana na mzozo wa sasa uliozuka baada ya uvamizi ulioongozwa na Marekani mnamo mwaka 2001 na kuwahimiza wanamgambo wa Taliban wasalimishe silaha zao.

"Ninawafahamu watu ambao ni maadui wa nchi yetu ambao wameshawahi kupigania amani ya nchi hii. Wengi wao wamefanyiwa vitendo vibaya na kukamatwa. Wameihama nchi yao na kuwa wapinzani wetu. Kwa mara nyengine tena ndugu zangu Wataliban, Mungu awalete nchini mwenu, msiiharibu nchi yenu, msijiangamize wenyewe. Tujikomboe kutokana na mauaji haya na tuijenge nchi hii kupitia mashauriano na viongozi wa kidini na wazee wa nchi hii," ameongeza kusema rais Karzai.

Kiongozi huyo ameondoka eneo la mkutano akiwa ndani ya gari lake lisiloweza kutobolewa na risasi, kama ilivyokuwa imepangwa, na kuuacha mkutano huo ukiendelea.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Staffan de Mistura, ambaye ni miongoni mwa wanadiplomasia 200 walioalikwa kuhudhuria mkutano huo, amebashiri kuwa mashauriano ya kumaliza vita nchini humo yatakuwa magumu na yatakabiliwa na vikwazo vingi.

Wakosoaji wameonya kwamba mkutano huo wa jirga huenda ukawa na matokeo machache mno, sio tu kwa sababu wapiganaji wa Taliban hawashiriki rasmi.

Mkutano wa leo ni wa tatu kuwaleta pamoja viongozi wa mbari, dini na jinsia kutoka sehemu mbalimbali wenye maslahi tofauti, tangu uvamizi ulioongozwa na Marekani ulipouangusha utawala wa Taliban uliodumu kati ya mwaka 1996 na 2001. Washirika wa rais Karzai, wakiongozwa na Marekani, wameueleza mkutano huo kuwa hatua kubwa muhimu katika kukomaa kwa siasa nchini Afghanistan.

Kundi la Taliban limeupuuza mkutano huo likiutaja kuwa chombo cha propaganda. Msemaji wa kundi hilo, Zabihullah Mujahid, ameliambia shirika la habari la AFP, kwa njia ya simu akiwa mahala pasipojulikana kwamba wametuma washambuliaji wanne wa kujitolea muhanga maisha waliokuwa wamejihami na bunduki na makombora kuushambulia mkutano huo.

Mkutano wa jirga unatarajiwa kumalizika keshokutwa Ijumaa kwa tamko la pamoja kuhusu hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kumaliza upinzani uliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu nchini Afghanistan, makundi gani yanayotakiwa kujumuishwa kwenye mchakato huo, na vipi makundi hayo yatakavyojulishwa.

Mwandishi: Josephat Charo/ AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 02.06.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ng0S
 • Tarehe 02.06.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ng0S

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com