Mkutano juu ya usalama wa nyuklia wamalizika. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 14.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mkutano juu ya usalama wa nyuklia wamalizika.

Mkutano mkubwa kuhusiana na usalama wa nyuklia, ulioshirikisha wakuu wa nchi na viongozi kutoka mataifa 47, umemalizika jana mjini Washington, Marekani.

Viongozi kutoka mataifa 47 duniani waliohudhuria mkutano wa usalama wa nyuklia mjini Washington.

Viongozi kutoka mataifa 47 duniani waliohudhuria mkutano wa usalama wa nyuklia mjini Washington.

Rais Barack Obama ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo amewataka viongozi duniani kuchukua hatua ya pamoja kuzuia makundi ya kigaidi kupata silaha za nyuklia, hatua ambayo amesema itaifanya Marekani na dunia kwa ujumla kuwa na usalama. Akitoa hotuba ya mwisho ya kufunga mkutano huo kuhusiana na usalama wa nyuklia, amesema mkutano huo ni thibitisho tosha la nini kinachowezekana, iwapo mataifa yataungana pamoja kwa ari ya ushirikiano katika wajibu wa pamoja kukabiliana na changamoto. Katika taarifa ya pamoja ya viongozi waliohudhuria mkutano huo, waliunga mkono wito uliotolewa na Rais Obama wa kudhibiti vyema malighafi za nyuklia zilizo na uwezekano wa kuathiriwa katika muda wa miaka minne ijayo. Katika harakati za kupambana na biashara haramu ya silaha za nyuklia viongozi hao wamekubaliana pia kushirikiana kupeana taarifa na upelelezi, mahakama na utaalamu mwingine wa kisheria katika kushughulikia tatizo hilo. Viongozi hao wamesema wametambua mahitaji ya kushirikiana miongoni mwa mataifa kuweza kuzuia kikamilifu matukio ya biashara haramu ya nyuklia. Akiwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kuwahi kufanyika nchini Marekani kwa zaidi ya miongo sita iliyopita, Rais Obama pia ameishinikiza China na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao wana mashaka kuunga mkono vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia wenye utata. Akizungumza katika mkutano huo kuhusiana na suala hilo la Iran, Rais Hu Jintao wa China amesema nchi yake kwa hakika inapinga silaha za nyuklia, lakini inaunga mkono matumizi ya nyuklia kwa raia.
Nuklear Gipfel Konferenz Atom Merkel Jintao

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akisalimia na Rais wa China Hu Jintao .

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambaye ameunga mkono azimio lililofikiwa katika mkutano huo, ameelezea kufurahishwa kwake na hatua hiyo iliyofikiwa na China ya kuonesha uwezekano wa kuchukuliwa hatua dhidi ya Iran. Mbali na kuizungumzia Iran Rais Obama pia alielezea hofu iliyopo kuhusiana na maghala ya silaha za nyuklia nchini Pakistan, nchi ambayo ni ngome kubwa ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na makundi mengine ya wapiganaji. Hata hivyo amesema nchi hiyo na nyingine ziko katika hatua ya kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kutangaza hatua mpya ya kuimarisha usalama katika bandari kuzuia biashara haramu ya nyuklia. Naye Rais Dmitry Medvedev wa Urusi ameuelezea mkutano huo kama wa mafanikio wakati nchi yake ikiwa imetangaza mipango ya kufunga mtambo wake wa mwisho wa madini ya Plutonium ambayo ni ya sumu kali yanayotumika kutengenezea silaha za nyuklia.

Nuklear Konferenz Obama und Dmitry Medvedev

Rais wa Marekani Barack Obama na Rais wa Urusi Dmitry Medvedev wakati wa mkutano wa usalama wa nyuklia, mjini Washington.

Afisa wa Urusi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alilithibitishia shirika la habari la AFP kwamba Rais Medvedev alitangaza mipango hiyo katika mkutano wa Washington. Mkutano mwingine wa usalama wa nyuklia unatarajiwa kufanyika Korea ya Kusini miaka miwili ijayo. Mwandishi: Halima Nyanza(afp,Reuters) Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 14.04.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MvqB
 • Tarehe 14.04.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MvqB
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com