1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkenya Rita Jeptoo asubiri hatma yake

16 Januari 2015

Mwanariadha wa Kenya Rita Jeptoo, anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kuongeza nguvu anasubiri kujua hatma yake baada ya kufika mbele ya maafisa wa tume ya riadha ili kusikilizwa kesi yake

https://p.dw.com/p/1ELlo
Rita Jeptoo 2014 Chicago Marathon
Picha: picture-alliance/dpa

Jeptoo amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa maafisa wa kitaifa kueleza kinaga ubaga na kufichua ukweli namna alivyopata dawa hizo zilizopigwa marufuku.

Mwanachama wa tume ya matibabu ya Shirikisho la Riadha Kenya na ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji Isaac Mwangi amesema wamekusanya habari nyingi kuhusu kesi hiyo lakini bado wataendelea kushauriana. Jeptoo bado amepigwa marufuku kushiriki mashindano yoyote. Pia amesema shirikisho la riadha Kenya - AK litashauriana na Shirikisho la Riadha Ulimwenguni - IAAF kuhusu kama Jeptoo anastahili kuadhibiwa kwa kupigwa marufuku ya miaka miwili au kwa kuzingatia sheria mpya ya kupigwa marufuku ya lazima kwa miaka minne ambayo ilianza kutekelezwa Januari mosi. Kikao kingine kitaskikilizwa katika kipindi cha wiki mbili.

Meneja wa Jeptoo, Federico Rosa na kocha Claudio Berardelli, ambao wote wamejitenga na sakata hilo, pia walifika mbele ya tume hiyo. Mumewe Jeptoo, Noah Busienei -- ambaye alimshutumu Jeptoo kwa kufanya uovu huo katika mwaka wa 2011, pia alihojiwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu