Mkataba wa baada ya Brexit kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya wapatikana | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.12.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkataba wa baada ya Brexit kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya wapatikana

Uingereza na Umoja wa Ulaya zimefanikiwa kupata mkataba wa baada ya Brexit siku chache kabla ya muda wa mwisho uliowekwa kumalizika.

Brüssel | Johnason bei von der Leyen Brexit Gespräche

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akiwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen mjini Brussels

Ikiwa imesalia muda usiozidi wiki mojakabla ya Uingereza kujitoa kikamilifu kutoka Umoja wa Ulaya, serikali mjini London imesema "mkataba umepatikana"

Imesema mkataba huo ni  "makubaliano ya kwanza ya biashara huria chini ya kanuni zisizo na ushuru wala mgawanyo wa mapato kuwahi kufikiwa pamoja na Umoja wa Ulaya"

Maafisa wa Umoja wa Ulaya pia wamethibitisha taarifa za kupatikana kwa mkataba huo wa biashara.

"Hatimaye tumepata makubaliano. Ilikuwa njia ndefu na yenye kona lakini tumepata mkataba mzuri wa kujifaharisha" amesema Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.

Von der Leyen ameongeza kusema kuwa makubaliano yaliyofikiwa ni ya haki na usawa na lilikuwa jambo la busara kwa pande zote kulifanikisha.

Kwa upande wake mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya baada ya Brexit Michel Barnier amesema mkataba uliopatikana ni ahueni kwa sababu umefikiwa siku chache kabla ya muda wa mwisho uliowekwa kumalizika.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema Baraza lake la Mawaziri litaujadili mkataba huo Disemba 28 na kufikia uamuzi wa Ujerumani kuuridhia mkataba huo au la:

Johnson asifu mkataba uliopatikana 

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameusifu mkataba uliopatikana akisema unaota nafasi kwa Uingereza kuwa "taifa jipya na huru" litakalosimamia tena sheria zake, mipaka na eneo lake la bahari.

"Nina furaha kuwatangaza mchana huu kuwa tumekamilisha mkaaba mkubwa zaiid wa kibiashara, wenye thamani ya paundi bilioni 660 kwa mwaka" amesema Johnson wakati wa mkutano wake na waandishi habari

Mkuu wa ujumbe wa Uingereza kwenye mazungumzo ya kutafuta mkataba David Frost ameandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba Uingereza sasa itakuwa taifa huru kuanzia Januari 1, na kuelezea pia furaha yake kwa tangazo la kupatikana mkataba

"Hatma na ustawi wetu upo mikononi mwetu. Nina imani tunapambana na kufanikiwa" aliandika Frost.

Hatma ya ushirikiano bado ni ngumu 

Mkataba huo unahakikisha kuwa pande hizo mbili zitaweza kuendelea kufanya biashara ya bidhaa bila ushuru au mgawanyo wa mapato.

Lakini licha ya mafanikio hayo, masuala muhimu kuhusu ushirikiano wa siku za usoni kati ya kanda ya Ulaya yenye nchi wanachama 27 pamoja na Uingereza, mwananachama wa zamani bado hayatatuliwa.

Mabunge ya Uingereza na Umoja wa Ulaya yote yatapaswa kupiga kura ya kuridhia au kuukataa mkataba huo, lakini kura katika bunge la Ulaya haitaitishwa hadi baada ya Uingereza kuondoka chini ya kanuni za uchumi za kanda hiyo hapo Januari mosi, 2021.