1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkakati wa Obama waungwa mkono

3 Desemba 2009

Mkakati mpya uliotangazwa na Rais Obama kuhusu Afghanistan umetetewa na maafisa waandamizi wa Marekani huku mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wakikusanyika Brussels kuzingatia wito wa kupeleka wanajeshi zaidi Afghanistan.

https://p.dw.com/p/KprK
U.S. Military commander in Afghanistan General Stanley McChrystal, right, arrives to a round table meeting of NATO defense ministers in Bratislava, on Friday, Oct. 23, 2009. (AP Photo,CTK/Jan Koller) ***SLOVAKIA OUT***
Jenerali Stanley McChrystal, Mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan.Picha: AP

Mkakati mpya wa Rais Barack Obama kupeleka wanajeshi 30,000 ziada nchini Afghanistan na kuvirejesha nyumbani vikosi hivyo kuanzia kati kati ya mwaka 2011, unaungwa mkono pia na washirika wa Marekani. Lakini hadi hivi sasa ni wachache waliojitolea kupeleka wanajeshi ziada kupambana na Wataliban katika vita vinavyoingia katika mwaka wake wa tisa.

Ujerumani na Ufaransa zimeashiria kuwa hazitoamua vyo vyote vile kabla ya kufanyika mkutano maalum wa Afghanistan mjini London Januari ijayo. Kwa upande mwingine, Uingereza ambayo tayari ina zaidi ya wanajeshi 9,000 huko Afghanistan, imethibitisha kuwa itapeleka wanajeshi 500 wa ziada. Italia nayo hii leo imeitikia wito wa Rais Obama kwa kutangaza kuwa mwakani itapeleka Afghanistan wanajeshi wengine wapatao 500 hadi 1,500.

Wakati huo huo, Ujerumani ambayo baada ya Marekani na Uingereza imechangia wanajeshi wengi zaidi nchini Afghanistan, leo inajadili suala la kurefusha muda wa kuvibakisha vikosi vyake nchini humo.Kwa upande mwingine Kanada na Uholanzi zimeshatangaza kuwa kati yao zinatazamia kuwarejesha nyumbani kama wanajeshi 5,000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Kwa kweli,mkakati mpya wa Rais Obama,umezusha wasiwasi nchini Marekani na Afghanistan hasa miongoni mwa wale wanaopinga kupeleka wanajeshi zaidi na wale wanaopinga kupanga tarehe ya kuanza kuvirejesha nyumbani vikosi hivyo. Kwa hivyo, mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, Jenerali Stanley McChrystal hii leo amewahakikishia maafisa waandamizi mjini Kabul kuwa Washington wala haipangi kuondoka mapema. Lengo la mkakati huo mpya amesema ni kuwapa Waafghanistan nafasi ya kujiandaa vya kutosha ili baadae waweze kujilinda wenyewe. McChrystal anaamini kuwa baada ya mwaka mmoja na nusu baadhi ya wanajeshi wa kigeni hawatohitajiwa tena nchini Afghanistan.

Kwa upande mwingine, Pakistan ina wasiwasi kuwa mkakati mpya wa Obama hautoisadia nchi hiyo inayopakana na Afghanistan. Hofu yake ni kuwa kupelekwa kwa wanajeshi wa ziada nchini Afghanistan huenda kukasababisha wanamgambo kuvuka mpaka na kukimbilia upya Pakistan na hivyo kuhatarisha zaidi eneo hilo lililokumbwa na machafuko.

Jenerali McChrystal na balozi wa Marekani Karl Eikenberry wanatazamiwa kwenda Brussels ambako mawaziri wa mambo ya nje wa NATO wamekusanyika kwa mkutano wa siku mbili. Afghanistan ni mada itakayokuwa juu kabisa katika ajenda yao hiyo kesho baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton kuwasili mjini Brussels.

Mwandishi :P.Martin/RTRE/AFPE

Mhariri: Hamidou,Oumilkher