Mkakati wa Marekani mashariki ya kati unahofiwa usije ukawageukia | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkakati wa Marekani mashariki ya kati unahofiwa usije ukawageukia

Marekani yawapatia silaha makundi fulani ya wasunni mashariki ya kati

default

Watu walitambua kwamba rais Geoge W. Bush hasikilizi shauri la mtu,tangu ripoti ya kamisheni ya Baker ilipotangazwa na kupendekeza mkondo mpya katika siasa ya Marekani kuelekea Irak.

Badala ya kuwarejesha nyumbani wanajeshi walioko Irak,ametuma wengine nchini humo.Lakini mkakati mpya wa usalama uliolengwa kurejesha amani mjini Baghdad,haujaleta tija.Zaidi ya hayo rais George W. Bush anatumia mbinu ambazo ziliwahi kutumiwa na serikali za zamani za Marekani katika nchi nyenginezo na kushindwa kuleta tija.Marekani inawapatia silaha hivi sasa miongoni mwa wengineo wasunni nchini Irak ili kuwatimua wafuasi wa Al Qaida.Kwa mujibu wa serikali,Al Qaida wanabeba jukumu la mashambulio ya hivi karibuni dhidi ya msikiti mkuu wa wa shiya huko Samara.

Mapigano kati ya Fatah na Hamas katika ukanda wa Gaza,mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa kiislamu nchini Libnan na mapigano kati ya waumini wa madhehebu ya Shiya na Sunni nchini Irak-mapigano hayo hayahusiani sana,isipokua panapohusika na ule ukweli kwamba Marekani na washirika wake wanaingilia kati kwa kuwapatia silaha,fedha na kuwaunga mkono kwa namna ambayo mambo yanazidi kuharibika.

Katika maeneo ya utawala wa ndani wa Palastina,Fatah hawajawahi kukubali kwamba wameshindwa katika uchaguzi wa bunge ulioitishwa mapema mwaka jana.Wamarekani,wa-Jordan na wamisri wanawapa kichwa wafuasi wa fatah katika msimamo wao huo na kuwapatia silaha huku wakiwasusia wafuasi wa Hamas.

Kwa kufanya hivyo walitaka kuwatia kishindo wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kislam wasionje matunda ya ushindi wao.Si hasha kwa hivyo kuona kinyang’anyiro cha kuania madaraka kinachukua sura ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hivi sasa.

Nchini Libnan jeshi la serikali linawazingira wanamgambo mia kadhaa wa kiislam waliojificha kwa takriban wiki nne sasa katika kambi za wakimbizi.Kundi la Fatah al Islam,linasemekana lilikua hadi hivi karibuni likipokea misaada ya fedha kutoka Saud Arabia, eti kuambatana na sera mpya zinazofuatwa na Marekani na washirika wake wa nchi za Ghuba katika kuwaunga mkono wanamgambo wa Libnan.

Ni wanamgambo wa kisunni wanaotumiwa kuleta wezani sawa dhidi ya wanamgambo wa kishiya-Hisbollah.Badala yake wanatakiwa wawe watiifu kwa familia ya Hariri.Alikua muanishi habari wa kimarekani Seymour Harsch aliyefichua mkondo huo mpya wa siasa ya marekani mwezi March uliopita.

Nchini Irak Marekani inayapatia silaha makundi ya wasunni,kwa matumaini kwamba watawaandama wapiganaji wa Al Qaida.Wanaosaidiwa ni familia kubwa kubwa katika mkoa wa Anbar ambao wameshadhihirisha mafanikio katika mapambano dhidi ya Al Qaida.Lakini makundi mengine pia ya wasunni yanayowaandamana waasi katika mikoa mengine pia.Maafisa wa kimarekani katika maeneo hayo ndio wanaotakiwa waamue nani wapatiwe silaha na vipuri baada ya kuahidi watapigana upande wa Marekani.

Mkakati huu mpya hauna maana yoyote.Kwamba silaha zinazotawanywa hivi sasa,itafika siku zitaangukia mikononi mwa watu ambao sio waliokusudiwa, na kulengwa dhidi ya wanajeshi wa kimarekani au washiya,ni suala la wakati tuu.

Gaza wanasaidiwa wapotovu wala mali ya umma waliotimuliwa madarakani kupitia uchaguzi wa kidemokrasi.Nchini Libnan, serikali isiyokua na uhalalifu wowote baada ya kupoteza imani ya wananchi walio wengi ndiyo inayoungwa mkono.Na nchini Irak silaha zinatolewa kwa matumaini eti zitasaidia kuleta amani.Itake isitake,kwa kufanya hivyo Marekani inazidi kupalilia majanga katika eneo hilo.

 • Tarehe 14.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHCf
 • Tarehe 14.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHCf

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com