1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkakati wa Bush Irak

14 Septemba 2007

Rais George Bush ametangaza kupunguza sehemu ya majeshi ya Marekani nchini Irak.Wapinzani wake hawakuridhika na kuondoa sehemu tu ya majeshi.

https://p.dw.com/p/CH8D

Rais George Bush wa Marekani,alilihutubia jana Taifa na kuchambua mkakati wake juu ya vita nchini Irak.

Mwanzoni mwa wiki,amirijeshi wake mkuu huko Irak,Jamadari David Petraeus,alitoa ripoti yake juu ya hali ilivyo nchini Irak-ripoti ambayo ilikumbwa na ila kali kutoka wajumbe wa chama cha Upinzani cha Democratic party.

Jana usiku Rais Bush akachambua msimamo wake na akatangaza kuondoa Irak sehemu ya wanajeshi wake.

Kama mwanzo,rais George Bush amevinjari kusonga mbele na mkakati wake nchini Irak.Anapitisha wakati na anategemea zaidi majeshi kurekebisha kilichoenda kombo nchini Irak.Na sio bila ya sababu wiki hii alimtanguliza kwanza jukwaani jamadari wake David Petraeus kumfungulia njia na iliofuatia ni kuitikia mapendekezo ya jamadari Petraeus.

Isitoshe, jamadari Petraeus amemfungulia Bush mlango kwa mara ya kwanza kudhukuru kile ambacho hadi sasa hajakisema:kuondoa baadhi ya askari wa Marekani kutoka Irak.

Baadhi ya wanaomkosoa, tena chamani,waweza hapo kutulizwa na uamuzi huo,lakini kwa wanajeshi wa Marekani hauna umuhimu mkubwa.

Hadi majira ya kiangazi mwakani,Bush anapanga kupunguza majeshi na kubakisha idadi sawa na ile iliokuwapo Januari mwaka huu .Hii inatokana na kuwa jamadari Petraeus hapangi kuomba askari zaidi wa kuichukua nafasi ya wale ambao muda wao wa kutumika Irak ulikuwa unamalizika.

Mpango wa kuongeza idadi ya askari tangu hapo ulikuwa wa muda tu.

Madhumuni ya rais Bush ni kuwavunja kasi wapinzani wa vita vyake nchini Irak kwa kuwaambia angalieni :nawarejesha nyumbani wanajeshi kama mnavyodai.

Kwamba wademokrat hawakufumba macho kutonahayo ni barabara.Kabla ya likizo ya majira ya kiangazi,Bunge la Marekani-Congress lilijaribu kushikamanisha kugharimia kwa fedha majeshi ya marekani yaliopo Irak kwa sharti kuwa tarehe inatolewa ya kurudishwa nyumbani.Kutaja tarehe tu hakutoshi.

Kwani katika jambo moja rais Bush hajakosea:kuporomoka kwa Irak katika kipindi kifupi kijacho kungekuwa ni tatizo kubwa kwa Ghuba na kipindi kirefu kwa ulimwengu.Na hali hii ingezuka, endapo majeshi ya Marekani yangehamishwa kwa papara papara.

Suluhisho lenye busara lafaa lipatikane hapo.

Kiroja cha mambo katika mkasa huu wa vita vya Irak,wiki hii si waziri wa ulinzi gates wala waziri wa nje Dr.Condoleeza Rice waliojitokeza hadharani.Na hii yabainisha kuwa Irak ni vita vya George Bush pekee.Urais wake umeandamana na vita vya Irak,kwani yafaa aungame kwamba hakutimiza nchini Irak hata shabaha yake moja.

Amen’gan’gania usukani wake lakini, ameanza kupepesuka:kwa mara ya kwanza ameungama pia kuwapo kwa majeshi ya Marekani nchini Irak,kutadumu zaidi kuliko muda wake yeye madarakani.Ni Matamshi mapyaya Bush,lakini,kamwe si siasa mpya.