1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa UN akutana na Bin Salman kuijadili Yemen

Angela Mdungu
16 Julai 2019

Mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa Martin Griffiths, amekutana na naibu waziri wa Ulinzi wa Saudia Khaled bin Salman katika mazungumzo aliyosema kuwa yamelenga kuimarisha makubaliano na Yemen ya kuweka silaha chini

https://p.dw.com/p/3M8TA
Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Katika mkutano wake wa leo na naibu waziri wa ulinzi wa saudia, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema wamejadili  juu ya namna ya kuiepusha Yemen na migogoro ya kieneo na namna ya kupiga hatua katika utekelezaji wa makubaliano ya Stockolm pamoja na hatua ya Saudi Arabiakuunga mkono kurejeshwa kwa amani.

Griffiths hapo awali alizisisitiza pande zinazohasimiana kuzingatia utekelezaji wa makubaliano ya Stockolm  akisema kuwa hatua ya kuondoa vikosi katika eneo la bandari ya Hodeida ni lazima ifuatwe na pande zote ili kutimiza makubaliano yaliyofikiwa Stocholm.

Wawakilishi wa pande hasimu nao wakutana

Mkutano wa Bin Salman na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, umefanyika baada ya wawakilishi wa serikali ya Yemen inayosaidiwa na Saudi Arabia na upande wa waasi wa kihouthi kufanya mazungumzo katika meli ya Umoja wa mataifa nje kidogo ya pwani ya Yemen kwa madhumuni ya kupunguza mvutano.

Makubaliano ya kusimamisha vita yalifanyika mwaka uliopita nchini Sweden yakitoa wito kwa waasi wa houthi na serikali ya Yemen kuondoa vikosi nje ya bandari muhimu ya Hodeida na maeneo mengine ya mji. Hatua ya kuondoa vikosi ilitakiwa kufanyika wiki mbili baada ya kutekelezwa kwa tangazo la kuweka silaha chini mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita  lakini lengo halikufikiwa baada ya serikali kuwatuhumu waasi kutoondoa vikosi.

Humanitäre Krise im Jemen | Hafen Hodeida
Sehemu ya bandari ya HodeidaPicha: picture-alliance/dpa/H. Al-Ansi

Mbali na mkutano wa leo, Griffith alikutana na Rais wa Yemen Abderabo Mansour Hadi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Hadi alipomtuhumu kuwapendelea waasi wa houthi. Kufuatia mkutano huo na Rais Hadi, mjumbe huyo wa Mataifa alisema kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa anafurahishwa na nia ya serikali ya Yamen ya kuzingatia makubaliano ya Stockolm.

Wakati haya yakiarifiwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu lilirefusha muda wa tume ya umoja huo inayosimamia usitishwaji mapigano huko Hodeida kwa miezi sita, hadi Januari 15 mwakani. Baraza hilo pia limemtaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress, kupeleka waangalizi katika tume hiyo, ambayo inatakiwa kuwa na wafanyakazi 75, lakini kwa sasa ina wafanyakazi 20 tu huko Hodeida.

Umoja wa Mataifa una matumaini usitishwaji mapigano Hodeida utaruhusu chakula kinachohitajika sana pamoja na misaada ya dawa kuwafikia mamilioni ya watu nchini Yemen.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, mgogoro wa muda mrefu wa Yemen, umeua  maelfu ya watu na kusababisha watu milioni 24 ambao ni mbili ya tatu ya idadi ya watu nchini humo wakihitaji msaada, tangu jeshi la Saudia lilipoingilia nchi hiyo baada ya waasi wa kihouthi kuutwaa mji mkuu, Sanaa mnamo mwaka 2015.

Mandishi: Angela Mdungu/afp/reuters

Mhariri: Josephat Charo