Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ahimiza majadiliano na upinzani baada ya kura ya Burundi | Matukio ya Afrika | DW | 25.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ahimiza majadiliano na upinzani baada ya kura ya Burundi

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi amelihimiza taifa hilo kuanzisha tena majadiliano na upinzani unaopinga matokeo ya kura ya maoni ambayo itamruhusu Rais Pierre Nkurunzinza kubaki madarakani hadi 2034.

Mjumbe huyo, Michel Kafando aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana kwamba Burundi itaweza kutatua mgogoro wake wa kisiasa kupitia majadiliano ya pamoja. Ikiwa hilo halitotokea, ameonya, upinzani dhidi ya matokeo ya kura ya maoni utazidi kuongeza kasi ya hali ya mvutano wa kisiasa inaoendelea hivi sasa.

Burundi imegubikwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji mwingine pamoja na kuzorota kwa hali ya kijamii na kiuchumi na hali ya kibinadamu kwa jumla.

Muungano mkuu wa vyama vya upinzani nchini Burundi Alhamisi iliyopita uliitaka mahakama ya kikatiba nchini humo kufuta matokeo ya kura ya maoni ya wiki iliyopita. Tume ya uchaguzi ilisema Jumatatu iliyopita kwamba zaidi ya asilimia 73 ya kura milioni 4.7 zilizopigwa iliunga mkono mabadiliko ya katiba, ikiwa ni pamoja na kumruhusu Rais Pierre Nkurunziza kubaki madarakani kwa miaka mengine 14 baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka 2020.

Warundi walitaka mabadiliko

Mshauri Mkuu wa Rais Pierre Nkurunziza Willy Nyamitwe ameiambia DW kwamba kura ya maoni ilikuwa ni pendekezo la wananchi wa Burundi waliotaka kufanyike mabadiliko nchini humo.

"Warundi walitaka mabadiliko ya kanuni zinazoongoza nchi. Kulifanyika mazungumzo na kupitia hayo mazungumzo Warundi wakaamua kwa kusema kipi kibadilishwe. Na ndio maana serikali ikajiandaa na kutengeneza rasimu ya katiba na hiyo sasa wakaipigia kura, na Warundi kwa wingi wakakubali kwamba mabadiliko hayo yanapaswa kuwa ndani ya katiba", amesema Willy Nyamitwe.

Michel Kafando (UN/Manuel Elias)

Michel Kafando, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi

Lakini kabla ya hata matokeo kutangazwa, muungano unaojulikana kama Amizero y'Abarundi ambao ulikuwa ukiongoza kampeni ya hapana dhidi ya kura hiyo ya maoni uliyakataa matokeo. Muungano huo ulisema kwamba, kura hiyo iliendeshwa kwa udanganyifu pamoja na vitisho.

Waangalizi walitegemea kwa kiasi kikubwa mabadiliko hayo kupitishwa kwa kura za wananchi, kutokana na kwamba Nkurunziza bado ana uungwaji mkono mkubwa katika maeneo ya vijijini, lakini pia ni kutokana na miaka mitatu ya ukandamizaji wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Nkurunziza, mwenye umri wa miaka 54, aliitumbukiza nchi yake katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2015 baada ya kukwepa kikomo cha mihula miwili ya uongozi akidai kwamba muhula wake wa kwanza ulitokana na uchaguzi wa bunge, na sio wa wananchi wa Burundi.

Takriban watu 1,200 wameuawa na 400,000 wamepoteza makaazi yao tangu nchini hiyo ilipoingia katika mgogoro wa kisiasa, kulingana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Nkurunziza ni kiongozi wa karibuni kabisa barani Afrika kufanya mabadiliko ya katiba ili aweze kubaki madarakani, ikiwa ni pamoja na Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Biya wa Cameroon na wengine kadhaa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com