1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Obama aenda Darfur.

Abdu Said Mtullya1 Aprili 2009

Mjumbe wa Marekani Scott Gration amesema lazima misaada ipelekwe tena katika jimbo la Darfur.

https://p.dw.com/p/HOAJ
Rais Omar al Bashir wa Sudan alieyafukuza mashirika ya misaada katika jimbo la Darfur .Picha: AP

Mjumbe wa Marekani Scott Gration anatarajiwa kuwasili nchini Sudan ikiwa ni sehemu ya juhudi za rais Obama katika kuishinikiza serikali ya Sudan ili iruhusu kurejea kwa mashirika ya misaada katika jimbo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.

Mjumbe huyo anaenda Sudan wakati ambapo hali katika jimbo hilo imezidi kuwa mbaya, baada ya serikali ya Sudan kuyatimua mashirika ya misaada .

Kuanzia mwezi ujao huenda watu milioni moja wa jimbo hilo wakakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Ziara ya mjumbe wa Marekani Scott Gration imeongeza matumaini juu ya kuzijumuisha nchi kadhaa za Afrika na za kiarabu katika juhudi za kumshinikiza rais wa Sudan Omar al Bashiri akubali kuyaruhusu mashirika ya misaada ya kimataifa yarejee tena katika jimbo la Darfur.Pana wasiwasi kwenye Umoja wa Mataifa juu ya hali ya Darfur kutokana na kufukuzwa kwa mashirika hayo.

Mjumbe wa Marekani bwana Scott Gration anaetarajiwa kuwasili nchini Sudan atatembelea majimbo ya Darfur, Juba na mji wa mafuta wa Abyei kabla ya kurejea katika mji mkuu, Khartoum ambapo bwana Gration atakutana na mafisa wa serikali ya Sudan.

Mbali na kuwa na wasiwasi juu ya kutokea maafa mengine makubwa katika jimbo la Darfur, utawala wa Marekani pia una wasiwasi juu ya kuvunjika kwa mkataba wa amani baina ya Sudan ya kaskazini na ya kusini uliofikiwa mnamo mwaka 2005.

Mjumbe wa Marekani atakutana na maafisa wanaopitisha sera za nchi.Bwana Gration amesema pana haja ya kuweka utaratibu utakaowezesha kurejea nchini Sudan kwa mashirika ya misaada na asasi nyingine zisizo za serikali .Mjumbe huyo amewaambia wandishi habari kwamba lazima ipatikane njia ya kuendelea kutoa misaada katika jimbo la Darfur.

Mwandishi Mtullya Abdu.

/AFPE/EAA