1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Mjue Kinjekitile Ngwale

Yusra Buwayhid
25 Julai 2018

Kinjekitile Ngwale ni jina tata katika historia ya Tanzania. Mwanzoni mwa karne ya 20 aliwashawishi watu katika nchi inayojulikana sasa kama Tanzania kusiamama na kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala nchi hiyo wakati wa ukoloni, akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza.

https://p.dw.com/p/2rWNU

Kinjeketile Ngwale anachukuliwa kama ishara ya upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani huko Tanganyika ambayo kwa sasa ni Tanzania. Mwanzoni mwa karne ya 20, alidai kwamba yeye ni roho na kwa sababu hiyo akawataka watu wa Tanganyika kuwapinga Wakoloni ambapo aliwapa maji aliyodai kuwa na dawa ambayo yangewafanya wasiweze kudhurika.

Aliishi: Ngarambe, Matumbi huko Tanganyika ambayo kwa sasa ndiyo Tanzania. Alinyongwa mwezi Agosti mwaka 1905 na maafisa wa Ujerumani kwa kosa la uchochezi.

Illustrationen - African Roots
Picha: Comic Republic

Anafahamika sana kwa: kupagawa na Hongo ambaye ni roho. Kulingana na mkongwe huyo, roho huyo alijitokeza kama nyoka, akamburuza Kinjeketile chini ya maji na alipoibuka baada ya saa ishirini na nne, alikuwa amekauka na akaanza kufanya utabiri.

Anafahamika pia kwa kuyaunganisha makabila ya eneo hilo na kadri ujumbe wake ulivyozidi kusambaa, akachangia kuwa tu wa kwanza kuleta utaifa Tanganyika.

Anajulikana pia kwa kuwaambia wafuasi wake kwamba iwapo watatumia maji yake yaliyo na dawa, risasi za Wajerumani hazingewaingia.

Anafahamika kwa kuwa mwanzilishi wa vita vya Maji Maji, ingawa yeye mwenyewe alikufa muda mfupi baada ya vuguvugu hilo kuanza. Vita vya Maji Maji vilianza mwaka 1905 na kuisha 1907 na vilikuwa mojawapo ya vita vikuu dhidi ya ukoloni barani Afrika.

Asili ya Afrika: Kinjeketile Ngwale

Alikashifiwa kwa: kuchangia kwa vifo vya watu wengi baada ya kuwadanganya kwamba maji yangewakinga dhidi ya risasi. Inakadiriwa kwamba kati ya watu 180,000 na 300,000 walifariki dunia wakati wa vita vya Maji Maji kutokana na mapigano na njaa, jambo lililopunguza idadi ya watu kwa thuluthi moja. Mwaka wa 1969 mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Tanzania Ebrahim Hussein alichapisha mchezo wake "Kinjeketile" kuhusu maisha ya mwasisi huyo na vita vya Maji Maji.

Mwandishi: Jacob Safari

Mhariri: Gakuba Daniel  

James Muhando, Hawa Bihoga na Philipp Sandner wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.