1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasifu wa Anna Mghwira

23 Oktoba 2015

Anna Mghwira ni mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya chama kipya cha upinzani cha ACT - Wazalendo. Ni mwanamke pekee miongoni mwa viongozi wanaogombea urais katika uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 25.

https://p.dw.com/p/1GtB3
Anna Mghirwa, Präsidentschaftskandidatin der ACT in Tansania
Anna Mghwira; mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT-WazalendoPicha: ACT/Wazalendo

Anna Mghwira alizaliwa Januari 23, mwaka 1959 mkoa wa Singida na umri wake ni miaka 56.

Tanzani ni taifa lenye miaka 50 ya mfumo dume wa uwongozi wa wanaume pekee, lakini sasa Watanzania wamepata fursa ya kumpigia kura kiongozi mwanamke kupitia chama cha ACT - Wazalendo. Hata hivyo, katika mahujiaono na DW Mghwira alisema, suala sio kumpa kura mgombea mwanamke bali ni kumchagua kiongozi anayeweza kutimiza majukumu yake kwa taifa analoliongoza.

Udhubuti wa fikra pamoja na uelewa wa sheria za nchi ni mambo ambayo Mghwira anauwezo nayo, kulingana na historia yake ya kielimu pamoja na kitaaluma.

Bibi Mghwira alipata elimu ya Msingi katika shule ya Msingi ya Nyerere Road kati ya mwaka 1968 na 1974.

Aidha, alipata elimu ya sekondari katika shule za sekondari za Ufundi ya Ihanja baina ya mwaka 1975 hadi 1978, na shule ya Seminari ya Lutheran baina ya mwaka 1979 hadi 1981.

Huo ulikuwa ndio mwanzo wa safari yake ndefu ya kutafuta elimu. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Mghwira alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini na kuhitimu na shahada ya Theolojia mnamo mwaka 1986.

Bila ya kupoteza muda mwaka huohuo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na huko alihitimu na Shahada ya Sheria.

Mwaka 1999 Mghwira alijiunga na Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza na mwaka 2000 alipokamilisha masomo yake na alitunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sheria.

Anna Mghirwa, Präsidentschaftskandidatin der ACT in Tansania
Anna Mghwira; mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT-WazalendoPicha: ACT/Wazalendo

Siasa

Mghwira mbali na kuwa msomi wa taaluma ya Sheria na Theolojia, lakini pia sio mgeni wa masuala ya siasa.

Alianza kama mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League).

Ila kilipoundwa chama cha CCM, Mghwira alipunguza kujihusisha na siasa na badala yake kutumia muda wake zaidi katika kujiendeleza kimasomo pamoja na kujenga familia yake.

Mwaka 2009, alirudi tena katika uwanja wa siasa kwa kujiunga na chama cha upinzani cha Chadema.

Akiwa mwanachama wa Chadema, Mghwira alishika nyadhifa mbili muhimu, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake pamoja na Katibu wa Baraza la Wanawake.

Na mwaka 2012, Mghwira alijaribu kujiingiza katika Mchakato wa kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki.

Hata hivyo katika kura ya maoni ya ndani ya Chadema, chama hicho kilimnyima fursa hiyo.

Machi ya mwaka huu, Mghwira aliamua kujiunga na chama kipya cha ACT - Wazalendo. Na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, Mghwira aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ACT.

Urais ACT - Wazalendo

Chama cha ACT kilisema kuwa Mghwira ana sifa zote za kuwa kiongozi bora wa taifa la Tanzania.

Ni mtu mwenye upeo mkubwa wa kufikiri, na ana uwezo wa kuwa mlinzi wa taifa. Ni mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu, pamoja na upeo wa uandishi. Kwa mujibu wa chama hicho Mghwira ni kiongozi anayeandika mwenyewe hotuba zake, kutokana na uzowefu wake wa kuandika makala mbalimbali kama mchango katika jamii.

Kuhusu maisha yake ya kawaida, Mghwira aliolewa mnamo mwaka 1982 na Shedrack Maghwiya - ambaye sasa ni marehemu - na walijaaliwa watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.