1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Aleppo bado washambuliwa

Sekione Kitojo22 Septemba 2016

Moto mkubwa ulizuka mjini Aleppo Syria wakati mji huo ulipotikiswa na mapigano na mashambulizi ya anga, kabla ya juhudi za mwisho zinazofanywa na mataifa makubwa kuyaokoa makubaliano yaliyoshindwa ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/1K6mY
Syrien Angriff auf Hilfskonvoi
Shambulio dhidi ya msafara wa malori ya misaada mjini AleppoPicha: picture alliance/newscom/O. H. Kadour

Naibu mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Ramzy Ezzeidin Ramzzy amesema ana matumaini mazungumzo ya amani huenda yakaanza tena katika wiki chache zijazo.

Wanadiplomasia wa ngazi za juu wa Marekani na Urusi wanatarajiwa kukutana na wadau wakuu mjini New York baadaye leo, baada ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kusema hatua za amani nchini Syria zinakabiliwa na hali ya kufa na kupona.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Urusi na Marekani yalivunjika mapema wiki hii, na kuruhusu ongezeko la mapigano katika kila eneo la mapigano katika vita vya miaka mitano vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Mapigano makali

Mapigano makali yalilikumba eneo la viunga vya mji wa Aleppo leo, baada ya mashambuilizi ya anga kuzusha moto mkubwa katika eneo la wilaya iliyoharibiwa inayodhibitiwa na waasi.

Wazima moto wa kujitolea walipambana usiku kucha kuuzima moto , ambao wanaharakati katika kituo cha habari cha mjini Aleppo waliposema ulisababishwa na mabomu ya gesi ya phosphorous.

Mabaki ya malori ya misaada ya Umoja wa Mataifa nchini Syria
Mabaki ya malori ya misaada ya Umoja wa Mataifa nchini SyriaPicha: Reuters/A. Abdullah

Shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria limesema mashambulio 14 dhidi ya kitongoji kinachodhibitiwa na waasi cha Bustan al-Qasr na Al-Kalasseh , yamesababisha moto mkubwa usiku kucha.

Mashambulizi mapya ya anga pia yalifanyika katika kitongoji cha Sukkari , limesema shirika hilo, na mapigano makali yamelikumba eneo la wilaya ya kusini magharibi ya Ramussa, ambako makundi ya waasi yanapambana kuzuwia mashambulizi ya majeshi ya serikali.

Shambulio la Jumatatu dhidi ya msafara wa malori ya misaada yalishutumiwa vikali na mashirika ya kutoa misaada na kusababisha Umoja wa mataifa kusitisha kwa muda operesheni zake nchini Syria.

Lakini katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press , rais bashar al-Assad alisema mashambulizi ya anga yaliyosababisha vifo vya wanajeshi wa jeshi la serikali wiki iliyopita yalikuwa ya makusudi, akipuuzia taarifa za maafisa wa Marekani kwamba yalifanyika kwa bahati mbaya.

Assad alisema Marekani inakosa nia ya kujiunga na Urusi katika mapambano dhidi ya waasi. Hata hivyo amesema serikali yake iko tayari kuzungumza.

"Tunatangaza kwamba tuko tayari kutekeleza operesheni yoyote ya kusitisha mapigano, ama iwapo mnataka kuiita , usitishaji mapigano, lakini sio kuhusu Syria ama Urusi , ni kuhusu Marekani na makundi ya magaidi ambao wana mafungamano na Dola la Kiislamu , IS na al-Nusra na al-Qaeda, na kwa Marekani na Uturuki na Saudi Arabia. Wametangaza wazi kwamba hawana nia, na hili sio jaribio la kwanza kusitisha mapigano nchini Syria."

Juhudi za kidiplomasia

Juhudi za kidiplomasia kumaliza vita vya Syria zinatarajiwa kuendelea mjini New York ambapo mkutano mpya wa kundi linalounga mkono Syria ISSG unatarajiwa kufanyika leo Alhamis.

Makamu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel akizungumza na rais Putin wa Urusi
Makamu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel akizungumza na rais Putin wa UrusiPicha: picture-alliance/Russian Presidential Press and Information Office/TASS/M. Klimentyev

Ujerumani inaamini kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba jeshi la syria linahusika katika shambulio la hivi karibuni dhidi ya msafara wa kupeleka misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa, makamu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema leo mjini Moscow.

Gabriel amewataka maafisa wa Urusi kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo, ambalo limewauwa raia 20 karibu na mji ulioharibiwa kwa vita wa Aleppo mapema wiki hii.

Wakati huo huo naibu mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria Ramzy Ezzeldin Ramzy amesema kwamba ana matumaini mazungumzo ya amani ya Syria yataanza tena katika wiki zijazo, licha ya matukio mabaya yaliyojitokeza.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga