Mjerumani aliyetekwa nyara Iraq aachiliwa huru | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 11.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Mjerumani aliyetekwa nyara Iraq aachiliwa huru

Mama wa Kijerumani aliyeachiliwa huru jana miezi mitano baada ya kutekwa nyara nchini Iraq, leo amewaomba watekaji nyara wamuachilie huru pia mwanawe ambaye bado yuko mikononi mwao. Wakati huo huo, mauaji na mapigano yanaendelea Iraq na jeshi la Marekani linalitarajia kundi la Al Qaida kulipiza kisasi kwa mashambulizi yaliyofanywa dhidi yao.

Waziri Steinmeier alipoarifu habari hizo

Waziri Steinmeier alipoarifu habari hizo

Habari juu ya kuachiliwa bibi Hannelore Krause zimetolewa leo asubuhi na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akithibitisha kuwa Bi Krause yuko salama salimina katika ubalozi wa Ujerumani mjini Bagdhad. Saa chache tu baada ya hapo, Mama huyu alionekana kwenye televisheni ya Al Arabiya akiwashukuru watekaji nyara wake kwa kumtendea vizuri na kuwaomba wamuachilie pia mwanawe Sinan. Mama Krause ambaye ameolewa na Muiraki alitekwa nyara pamoja na mwanawe miezi mitano iliyopita.

Kijana Sinan mwenye umri wa miaka 20 lakini bado hajaachiliwa. Ndiyo sababu, waziri Steinmeier amewaomba waandishi wa habari wasisambaze tetesi juu ya kisa hicho: “Siwezi kusema chochote kwa wakati huu, na hapa naomba tuelewane, kwani kiasi tunachofurahia juu ya kuachiliwa huru Bibi Krause, bado tumeshikwa na hisia ya hofu ya kutojua juu ya hali ya mwanawe ambaye bado yuko mikononi mwa watekaji nyara.”

Wizara yake itafanya kila iwezalo ili mtekwa nyara wa pili aachiliwa huru pia, waziri Steinmeier aliongeza. Watekaji nyara walitaka wanajeshi wote wa Kijerumani waondoshwe kutoka Afghanistan. Katika risala mbili za video walitishia kuwaua mahabusi wao, lakini serikali ya Ujerumani ilisisitiza haiwezi kushinikizwa. Watekaji nyara wamejitambulisha kuwa wa kundi la “Mishale ya utakatifu”.

Wakati huo huo jeshi la Marekani linaonya dhidi ya mashambulio ya kulipa kisasa ya kundi la Al Kaida kama alivyoarifu msemaji wa jeshi. Katika miezi miwili iliyopita, hatua zetu ziliharibu miundo mbinu ya kundi hilo, msemaji huyu aliongeza. Taarifa zake zinafuata umwangaji mkubwa wa damu mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Iraq ambapo watu wasiopungua 250 waliuawa. Maafisa kadhaa wa jeshi la Marekani walisema wanatarajia mashambulio mabaya katika muda wa miezi miwili ijayo kabla ya ripoti ya jeshi juu ya hali ilivyo Iraq itakapotolewa mbele ya bunge la Marekani. Rais George Bush, ambaye anakabiliwa na upinzani mkali dhidi ya sera zake za Iraq, aliomba bunge na wakosoaji wake kuisubiri ripoti hiyo. Alisema: “Tumeanza tu hivi punde. Wanajeshi wengine walifika tu wiki chache zilizopita na wameanza shughuli zao. Hivi sasa kuna watu huko Washington wanaotaka tuwasimamishe? Nadhani bunge linapaswa kumpa kamanda David Petraeu muda zaidi kutathmini hali ilivyo baadaye mwaka huu kabla ya kuchukua uamuzi.”

Baada ya kutumwa wanajeshi 28.000 zaidi, Marekani sasa ina wanajeshi 157.000 huko Iraq. Bush hasa aliyapuuza madai ya kutoka ndani ya chama chake cha Republicans. Maseneta kadhaa walimtaka Bush arekebishe sera zake za Iraq na kuzipa kipaumbele juhudi za kulipa mafunzo na vyombo jeshi la Iraq. Bush lakini alionya kwamba kuondoka haraka kutalipa nafasi zaidi kundi la Al Qaida na hivyo kuathiri usalama wa kizazi cha watoto wa sasa.

 • Tarehe 11.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB2u
 • Tarehe 11.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB2u
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com