1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa TV Uingereza

23 Aprili 2010

Nani alishinda jana: Brown,cameron au Glegg ?

https://p.dw.com/p/N4Ub

Baada ya duru ya pili ya mjadala motomoto wa TV kati ya viongozi wa vyama vikuu vitatu -Labour- kikiongozwa na waziri-mkuu Gordon Brown, chama cha Conservative cha David Cameron, na Liberal Democrat, cha Nick Glegg, matokeo ya uchaguzi wa Uingereza mwezi ujao hapo Mei sita, bado si wazi.

Uchunguzi wa maoni baada ya duru ya jana iliotuwama juu ya siasa za nje, umebaini kuwa waziri mkuu Brown na mpinzani wake mkubwa Cameron walikuwa bora kidogo ukilinganisha na duru iliopita.Kiongozi wa chama Kidogo cha Liberal Democrat, Nick Clegg, aliehujumiwa sana na wapinzani wake hao 2 na mwishoe, maoni yasema hakuna mshindi wazi.

Ni chama gani kitaibuka mshindi katika uchaguzi wa mwezi ujao nchini Uingereza, ni vigumu kuagua kutokana na duru ya jana ya majadiliano ya Televisheni .Kiongozi alieusoni kabisa kwa muujibu wa uchunguzi wa maoni tangu miaka 2 iliopita, David Cameron wa chama cha Conservative na mpinzani wake mkuu anaetaka kumtimua madarakani, waziri mkuu wa chama cha Labour, Gordon Brown, walijikuta wakichagizwa kumpiga kumbo kwa hoja zao kiongozi wa chama Kidogo cha Liberal Democrat, Nick Klegg, alietamba duru ya kwanza kwa mujibu wa maoni.

Uchunguzi uliofanywa ghafula baada ya mjadala wa jana uliotuwama juu ya siasa za nje kumalizkka, ulitatanisha -wengine wakisema huyu ameshinda na wengine yule. Vituo viwili vimedai kuwa, Kiongozi wa chama cha Conservative, David Cameron, ndie mshindi wakati vituo vikidai Nick Klegg, ametia tena fora mbele yao wote.

"Nadhani matokeo yalikuwa sare"- alisema Justin Fisher, profesa wa taaluma ya kisiasa katika Chuo kikuu cha Brunel.

Vituo vingi vilivyokuwa vikimpigia upatu kushinda mnamo miaka 2 iliopita David Cameron wa Conservative, sasa vinaonesha kuwa, hakuna chama kitakachoibuka na ushindi wazi kuweza kuunda serikali bila mwenziwe. Na hii ni hali nadra katika Uchaguzi wa Uingereza ambao kidesturi ,ama mshindi hutoka chama cha Labour au cha Conservative.

Kwa sura inavyoonesha sasa, Bw.Clegg wa Liberal Democratic ndie mwenye ufunguo kuamua nani ataongoza serikali ijayo ya Uingereza baada ya uchaguzi wa Mei sita

Mjadala wa jana ulichambua sera za nje, kama vile Afghanistan,Umoja wa Ulaya, lakini pia haukukwepa sera za ndani, kama uhamiaji na silaha za nyuklia za Uingereza.

Magazeti ya Uingereza nayo yabainika kugawika kwa maoni mengi yakiegemea mafungamano yao na vyama hivyo vya kisiasa. The Sun, gazeti kubwa litokalo kila siku nchini Uingereza na linalokiunga mkono chama cha Conservative, limejitokeza na kichwa cha habari: Mtoto aliejizatiti upya"-yaani David Cameron.

Mpinzani wake, Daily Mirror, linalokipendelea chama cha Labour, linadai Cameron amejikwaa tena katika mjadala wa jana.The Guardian, linaloelemea mrengo wa shoto limeandika kuwa Klegg amezima dharuba za wapinzani wake.

Leo ijumaa, macho yataanza kukodolewa upande wa sera za uchumi baada ya kutolewa makadirio ya kukua kwa uchumi wa Uingereza katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE

Uhariri: Miraji Othman