Mjadala bila ya mshindi | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mjadala bila ya mshindi

Ngumi kali lakini bila ya kupigwa knock-out – hivyo ndivyo lilivyoandika gazeti moja la hapa nchini baada ya mjadala kati ya wagombea wawili wa kiti cha rais nchini Ufaransa uliotangazwa jana kupitia televisheni. Mwanasiasa wa chama cha kihafidhina Nicolas Sarkozy na mshindani wake wa kisoshialisti, Bi Segolene Royal walibadilishana maneno makali – na zaidi ya Wafaransa Millioni 20 waliwasikiliza.

Mechi ya maneno

Mechi ya maneno

Mita mbili – huu ni umbali kati ya wagombea wawili katika studio ya televisheni ambamo walijadiliana juu ya malengo yao ya kisiasa. Umbali kati ya sera zao lakini ni mkubwa zaidi. Sio msoshialisti Segolene Royal wala mgombea wa kihafidhina Nicolas Sarkozy walishinda katika mjadala huo, walisema wadadisi wa mambo ya kisiasa. Badala yake wote wawili waliwavutia wale wapigaji kura ambao tayari walishafanya chaguo lao. Mamillioni ya Wafaransa lakini hawakuamua bado watamchagua nani.

Ni mara ya kwanza na ya pekee mjadala huo wa hadhara kufanyika kati ya wagombea hawa wawili wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa. Kwa mujibu wa wataalamu wa uchaguzi, Nicolas Sarkozy aliweza kutopoteza utulivu wake – licha ya kuwa Sarkozy anasemekana kuwa ni mchokozi. Wakati huo huo, msoshialisti Bi Royal alionyesha ujuzi katika sekta mbali mbali baada ya kukosolewa hapo kabla kwamba anakosa ustadi.

Masuala yaliyozungumiwa yalihusu kila sehemu ya siasa, ikiwa ni ajira, sera za elimu au usalama wa ndani. Katika suala la kodi, wagombea hawa wawili walikuwa na mawazo tofauti kabisa.

“Katika suala la kodi nitazipa kipaumbele kodi zinazohusiana na mazingira. Nataka kutekeleza mageuzi ya kodi zinazohusu ajira katika sekta ya mazingira.”

Haya aliyasema Bi Segolene Royal. Mshindani wake, Nicolas Sarkozy, alizingatia hasa kuweka masharti ya ujumla ya kodi: “Iwapo nitachaguliwa kuwa rais wa nchi, nataka malipo ya kodi yasizidi nusu ya mishahara.”

Bi Royal alimshutumu Sarkozy kwa kutoweza kutuliza ghasia nchini Ufaransa licha ya sera zake kali dhidi ya wafanya fujo. Sarkozy lakini alijitetea kwa hoja ya vitendo vya uhalifu vimepungua kwa asilimia 10 katika miaka tano iliyopita. Watetezi hao walikubaliana katika suala la kulipa mshahara wa chini, lakini walitofautiana katika maoni juu ya muda wa kazi ambao nchini Ufaransa ni saa 35 kwa wiki. Msoshialisti Royal alisisitiza kuwa muda huu wa kazi ni ushindi wa kijamii; Sarkozy, kwa upande wake lakini alisema kufupisha muda wa kufanya kazi kuliathiri vibaya uchumi.

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi tarehe 22 Aprili, Sarkozy alipata asilimia 31 ya kura, na Segolene Royal alimfuata akipata karibu asilimia 26. Kulingana na kura za maoni, Sarkozy bado anaongoza.

 • Tarehe 03.05.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHEv
 • Tarehe 03.05.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHEv

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com