Misri yawahukumu waandishi miaka 7 jela | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Misri yawahukumu waandishi miaka 7 jela

Hatua ya mahakama ya Misri kuwakuta na hatia waandishi wa habari wa shirika la Al-Jazeera umelaaniwa na pande mbali mbali dunia, na nchi kadhaa zimewaita mabalozi wa Misri kulalamikia uamuzi huo wa mahakama.

Waandishi wa habari wa Al Jazeera wakisomewa hukumu mahakamani

Waandishi wa habari wa Al Jazeera wakisomewa hukumu mahakamani

Ni sauti ya jaji wa mahakama mjini Cairo, akitangaza hukumu dhidi ya a hao wa al-Jazeera,ambao ni pamoja na Peter Greste ambaye ni raia wa Australia, Mohamed Fahmy raia wa Canada mwenye asili ya Misri, na Baher Mohammed ambaye ni raia wa Misri. Mahakama hiyo imesema waandishi hao wamekutwa na hatia katika mashitaka yenye uhusiano na ugaidi. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya waandishi wa habari ambao hawakuwepo mahakamani, wamehukumiwa miaka 10 jela kila mmoja.

Uamuzi huo ambao umepitishwa asubuhi ya leo umezusha laana kutoka pande mbali mbali, na hofu kuhusu hatima ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Misri. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Australia Julie Bishop amesema uamuzi huo umeishitua serikali ya nchi yake.

Mwandishi Peter Greste raia wa Australia aliyepewa kifungo cha miaka 7 jela

Mwandishi Peter Greste raia wa Australia aliyepewa kifungo cha miaka 7 jela

''Hukumu kama hii, haiendani na madai ya Misri kwamba iko katika kipindi cha mpito kuelekea demokrasia. Serikali ya Australia inaitaka serikali mpya ya Misri, kutafakari ujumbe ambao dunia inaupata juu ya hali ya mambo nchini humo, kupitia hukumu hii.'' Amesema bi Bishop.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Australia amesema serikali yake inashindwa kuelewa kama kweli uamuzi huo umefikiwa kutokana na ushahidi ulioonyeshwa mahakamani.

Hukumu ya kuchukiza

Sio Australia pekee iliyokasirishwa na uamuzi huo wa mahakama ya Misri. Uingereza imesema imemuita balozi wa Misri nchini humo kulalamikia uamuzi huo ambao imeuita wa kuchukiza.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague, amesema amechukizwa kwa namna ya pekee na hitilafu zilizojitokeza wakati wa uendeshaji wa kesi dhidi ya waandishi hao, hususan upande wa mwendeshamashitaka kukataa kuonyesha ushahidi muhimu kwa upande wa utetezi.

Uholanzi ambayo mmoja wa waandishi waliohukumiwa bila kuwepo mahakamani ni raia wake, imemwita pia balozi wa Misri nchini humo, na waziri wa mambo ya nchi za nje Frans Timmermans amesema atalijadili suala hilo na mawaziri wenzake wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya katika mkutano unaofanyika Luxembourg.

Mchezo wa kuigiza mahakamani

Shirika la Amnesty International limesema hukumu dhidi ya waandishi hao ni kiza kwa uhuru wa kujieleza nchini Misri

Shirika la Amnesty International limesema hukumu dhidi ya waandishi hao ni kiza kwa uhuru wa kujieleza nchini Misri

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeilinganisha hukumu hiyo dhidi ya waandishi wa habari wa al-Jazeera na mchezo wa kuigiza, na kuongeza kuwa leo ni siku ya kiza kwa uhuru wa kujieleza nchini Misri.

Waandishi wote wanaohusika katika kesi hiyo walituhumiwa kulisaidia kundi la Udugu wa Kiislamu lililopigwa marufuku, na kuichafua sura ya Misri baada kuondolewa madarakani rais kutoka kundi hilo, Mohammed Mursi.

Hukumu hiyo imetolewa siku moja baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry,ambaye akiwa mjini Cairo jana aliitolea wito Misri kuheshimu uhuru wa watu kutoa mawazo yao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com