1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan itolewe katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi

10 Septemba 2019

Misri imetoa wito wa kuungwa mkono serikali mpya ya kiraia ya nchini Sudan. Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry pia ameitaka Marekani iiondoe Sudan kutoka kwenye orodha ya nchi zinazodhamini ugaidi.

https://p.dw.com/p/3PL27
Ägypten Außenminister Sameh Shoukry
Picha: Getty Images/AFP/A. Schmidt

Marekani iliiorodhesha Sudan kama mojawapo ya mataifa yanayodhamini ugaidi mnamo 1993. Kabla ya kumaliza muda wake madarakani utawala wa Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama ulianza mchakato rasmi wa kuiondoa Sudan kwenye orodha hiyo lakini, taratibu zikasimamishwa mara baada ya kuanza maandamano ya kupinga utawala wa Rais wa zamani Omar al-Bashir.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri amesema Sudan sasa ni nchi mpya yenye serikali chini ya makubaliano ya kugawana madaraka kati ya wanaharakati wa demokrasia na wanajeshi. Awali wengi walihofia kwamba majenerali wa jeshi wangeendelea kubakia madarakani kwa nguvu.

Huku hayo yakiariofiwa hivi karibuni Umoja wa Afrika uliirejeshea Sudan uanachama wake, baada ya kusimamishwa kwa miezi mitatu ikisubiriwa kuunda serikali ya kiraia kufuatia kuondolewa madarakani kwa rais wa muda mrefu Omar al Bashir. Sudan ilisimamishwa uanachama wake katika Umoja wa Afrika mwezi Juni kufuatia vurugu za maandamano ambapo madaktari wa upande wa upinzani walisema watu kadhaa waliuwawa katika vurugu hizo kati ya jeshi na upinzani.

Lakini baada ya jeshi na vyama vya kiraia pamoja na viongozi wa maandamano kutia saini mkataba wa miaka mitatu, wa kugawana madaraka mwezi Agosti, Sudan ilimteua Abdalla Hamdok kuwa Waziri Mkuu.

Wiki iliyopita Hamdok aliunda baraza la kwanza la mawaziri nchini humo tangu mwezi Aprili wakati Omar al Bashir alipoondolewa madarakani.