1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yapanga kulipiza kisasi dhidi ya Senegal

Bruce Amani
28 Machi 2022

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Misri Carlos Queiroz amesema timu hiyo itajilinda zaidi kwa "kucheza na wachezaji 16 nyuma" ili kutetea ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Senegal watakapokutana Jumanne

https://p.dw.com/p/498d3
WM Qualifikation Ägypten Senegal
Picha: Ahmed Gomaa/Xinhua News Agency/picture alliance

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Misri Carlos Queiroz amesema timu hiyo itajilinda zaidi kwa "kucheza na wachezaji 16 nyuma" ili kutetea ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Senegal watakapokutana kesho Jumanne katika mechi ya mchujo wa raundi ya pili ya kuwania kuingia kwenye michuano ya Kombe la Dunia.

Kocha huyo mzaliwa wa Msumbiji na aliyewahi pia kuwa meneja wa klabu ya Real Madrid na meneja msaidizi wa Machester United, amesema timu yake inastahili kushinda mchuano huo dhidi ya Senegal na kwa hivyo kila mchezaji anapaswa kuongeza juhudi mara mbili.

Michuano ya kesho Jumanne itaamua timu tano za Afrika zitakazofuzu kwenye michuano ya kombe la dunia la mwaka 2022 nchini Qatar. Kwa upande mwingine kocha mpya wa Ghana Otto Addo ana matumaini kwamba timu yake hiyo Black Stars inaweza kufuzu kuingia michuano ya kombe la dunia licha ya kutoka sare ya 0-0 na Nigeria katika mchuano wa kwanza.

Cameroon chini ya kocha Rigobert Song itakabana koo na Algeria ikiwa nyuma bao moja kwa sifuri kutokana na mechi ya kwanza.

Morocco itaialika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi ambayo kocha wa Morocco Vahid Halilhodzic  alikiri kuwa ilikuwa ngumu mno

"Tulicheza dhidi ya timu nzuri sana ya Congo. ndani ya uwanja uliona mpira unapaa angani. Lazima tujitume sawasawa mjini Casablanca, tucheze vizuri zaidi ya tulivyofanya huko Congo. Kulikuweko na matukio ya udanganyifu pia kwa hiyo bado tuna furahia matokeo tuliyoyapata. Hata kama inaumiza kwa kupoteza penalti ”

Mali watakuwa ugenini dhidi ya Tunisia wakiwa nyuma kwa bao moja kwa sifuri.

afp, dpa, ap, reuters