1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri na Uturuki kufanya mazungumzo leo

Angela Mdungu
5 Mei 2021

Misri na Uturuki zinaanza leo mazungumzo ya siku mbili yanayolenga kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo hasimu mjini Cairo

https://p.dw.com/p/3sz7E
Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan
Picha: Aytac Unal/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Misri, mazungumzo hayo, yataongozwa na manaibu wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi hizo.

Wizara ya mambo ya nje ya Misri imesema majadiliano kati ya nchi yake na Uturuki yatajikita katika hatua muhimu zinazoweza kusaidia kurejesha mahusiano ya mataifa hayo kwenye hali nzuri katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Mazungumzo hayo yanafanyika ikiwa ni takribani miezi miwili tangu Uturuki ilipoanzisha mawasiliano ya kidiplomasia na Misri tangu mwaka 2013. Mahusiano ya nchi hizo, yalizorota katikati ya mwaka 2013 baada ya Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi, kuipindua serikali ya Mohammed Morsi aliyekuwa ameteuliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alikuwa akimuunga mkono Morsi, afisa wa juu wa chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho kwa sasa kimepigwa marufuku Misri.

Mnamo mwaka 2011, baada ya machafuko katika mataifa ya Mashariki ya Kati, Uturuki iligeuka kuwa kimbilio kwa wanaharakati wa kiislamu hasa kutoka Misri waliohusishwa na chama cha Udugu wa Kiislamu cha Morsi. Mwezi Machi, washauri wa Rais Erdogan waliwataka baadhi ya watangazaji wenye vipindi maarufu wanaoishi uhamishoni nchini mwake kama vile Moataz Matar na Mohamed Nasser, wapunguze ukosoaji kwa Rais wa Misri.

Ägypten Mohammed Mursi
Mohammed MorsiPicha: picture-alliance/epa/K. Elfiqi

Watangazaji hao machachari ambao walihukumiwa miaka 10 kila mmoja bila kuwepo mahakamani na kuwekwa  wenye orodha ya Misri ya magaidi  "kwa kujaribu kuipindua serikali'', walilazimika kufunga vipindi vyao.

Kutokuaminiana huenda kukaathiri juhudi za kidiplomasia

Mataifa hayo mawili yameanza juhudi za kuweka sawa mahusiano yao, lakini wachambuzi wanasema  kutokuaminiana kwa muda mrefu kutasababisha kutengamaa kwa mahusiano hayo kuchukue muda mrefu. Kwa pamoja nchi hizo zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo zaidi kutoka Marekani tangu alipoondoka madarakani Rais Donald Trump. Uturuki na Misri, kwa pamoja zimekuwa zikiiunga mkono Libya iliyoathiriwa vibaya na machafuko.

Kurejea kwa mahusiano mazuri kati ya Misri na Qatar mnamo mwezi Januari mwaka huu baada ya miaka minne ya mgogoro wa kwenye eneo la Ghuba na Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Bahrain, kunatajwa pia kama kichocheo cha kuendeleza juhudi za kukuza diplomasia katika ukanda huo. Akizungumzia juhudi hizo za kurejesha diplomasia Profesa wa sayansi wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdul Khaleq Abdallah amesema kukutana kwa mazungumzo kwa sasa kunatosha lakini hali ni tete na huenda mambo yakaharibika tena.