1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri: Kura ya maoni kumruhusu el Sissi kutawala hadi 2030

Oumilkheir Hamidou
20 Aprili 2019

Wamisri wanayapigia kura mabadiliko ya katiba yatakayomruhusu rais Abdel-Fatah el-Sissi abakie madarakani hadi mwaka 2030, yatakayolizidishia nguvu jeshi na kupiga hatua ziada kuelekea utawala wa kiimla.

https://p.dw.com/p/3H8HG
Ägypten Präsident Abdel Fattah al Sisi
Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/V. Belousov

Kura hiyo ya maoni inaitishwa huku wakosoaji wakiandamwa kwa nguvu kupita kiasi. Serikali ya el-Sissi imewakamata maelfu ya watu, wengi wao ni wafuasi wa itikadi kali ingawa kuna wanaharakati wa kawaida pia na kwa namna hiyo kurejesha nyuma uhuru uliopatikana kutokana na vuguvugu la mwaka 2011 la kudai demokrasia.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa tangu saa tatu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki. Zoezi la kupiga kura litaendelea kwa muda wa siku tatu ili kuwawezesha wapiga kura kutoa sauti zao.

Nje ya kituo cha kupiga kura, karibu na piramidi za Giza, dazeni mbili ya watu, wengi wao  mabibi wazee, wamepanga foleni wakisubiri zamu yao huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi na vikosi vya usalama.

Haja Khadija, bibi wa miaka 63, anasema amekuja kupiga kura kwasababu ya "usalama na utulivu" wa nchi. "Tunampenda el-Sissi. Amefanya mengi. Ametuongezea malipo ya uzeeni," anasema.

Kituo cha televisheni ya taifa kinasema el-Sissi amepiga kura katika mkoa wa Heliopolis, karibu na kasri la rais mjini Cairo.

Sauti za upande wa upinzani zimenyamazishwa kutokana na jinsi kura hiyo ya maoni ilivyoitishwa kwa pupa. Vyombo vya habari vinavyoelemea upande wa serikali vimekuwa vikifanya kampeni zao tangu wiki kadhaa na kuitaja "kura ya ndio kuwa ni wajibu wa kitaifa."

Bibi huyo anatoka kupiga kura
Bibi huyo anatoka kupiga kuraPicha: Reuters/A. Abdallah Dalsh

Upande waa upinzani haukuruhusiwa kuendesha kampeni

Kuanzia mapema mwezi huu wa April, mji mkuu wa Misri umejaa mabango na maandishi yanayowahimiza wapiga kura waunge mkono mageuzi. Mabango mengi yanasemekana yamegharamiwa na vyama vinavyoiunga mkono serikali, wafanyabiashara na wabunge.

Bunge linalodhibitiwa na wafuasi wa el-Sissi limeunga mkono kwa wingi mageuzi hayo Jumanne iliyopita. Sauti 22 tu ndizo zilizopinga na moja kutoelemea upande wowote kutoka jumla ya wabunge 554 waliohudhuria kikao hicho. Siku ya pili yake tume ya uchaguzi ikatangaza zoezi la kupiga kura litaanza Jumamosi,

Mageuzi yanayotarajiwa yanatajwa na wakosoaji kuwa hatua ziada kuelekea utawala wa kimabavu.

Kura ya maoni inafanyika miaka minane baada ya vuguvugu la kudai demokrasia kumaliza utawala wa miongo mitatu wa Hosni Mubarak na miaka karibu sita baada ya el-Sissi kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'owa madarakani rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia huru, mfuasi wa itikadi kali Mohammed Mursi.

Makundi mawili ya kimataifa, Human Rights Watch na halmashauri ya kimataifa ya wanasheria yameihimiza serikali ya Misri ibatilisha mageuzi hayo.

Kongamano la vyama vya kiliberali vinavyoelemea mrengo wa kushoto limewahimiza Wamisri wateremke kwa wingi vituoni ili kupiga kura ya "la" dhidi ya mageuzi hayo. Kongamano hilo linasema linatumia mtandao wa kijamii kueneza wito huo kwasababu limekatazwa kutundika mabango majiani .

Mageuzi hayo yanarefusha muhula wa rais kutoka miaka minne hadi sita na kumruhusu atawale kwa mihula isiyopindukia miwili.