1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Inadaiwa kuwa ni mashambulizi ya kujitowa muhanga

10 Oktoba 2015

Takriban watu 86 wameuwawa Jumamosi (10.10.2015) katika mji mkuu wa Uturuki Ankara wakati mabomu mawili yalipowalipukia wanaharakati wa sera za mrengo wa kushoto na wafuasi wa Kikurdi kwenye maandamano ya amani.

https://p.dw.com/p/1GmCE
Hali kufuatia miripuko katika maandamano ya Ankara. (Jumamosi10.10.2015)
Hali kufuatia miripuko katika maandamano ya Ankara. (Jumamosi10.10.2015)Picha: Getty Images/G. Tan

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema kuna dalili nzito kwamba miripuko hiyo imetokana na mashambulizi ya kujitowa muhanga. Waziri Mkuu huyo pia ametangaza maombolezo rasmi ya siku tatu kwa wahanga na manusura wa mashambulizi hayo.

Shambulio hilo karibu na kituo kikuu cha reli mjini Ankara limezidi kupalilia mvutano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Novemba Mosi wakati hali hiyo tayari ikiwa ni mbaya kutokana na mashambulio ya serikali dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi.

Miili ya wanaharakati waliouwawa ilikuwa imetapakaa barabarani kufuatia miripuko hiyo huku mabango waliokuwa wameyabeba kwa ajili ya maandamano hayo ya " Kazi, Amani, Demokrasia." yakiwa pembezoni mwao.

Waziri wa Afya Mehmet Muezzinoglu amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara kwamba watu 62 wamekufa hapo hapo na wengine 24 wamefia hospitalini. Amesema wengine 186 wamejeruhiwa katika shambulio hilo ambapo 28 kati yao hali zao ni mbaya.

Mashambulizi yalenga kuvuruga umoja

Rais Recep Tayep Erdogan wa Uturuki amelaani mashambulizi hayo kuwa ni ya ouvu mkubwa na kwamba "yamelenga umoja wetu na amani ya nchi yetu."Afisa wa serikali ya Uturuki ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali inashuku kwamba mashambulizi hayo yana uhusiano na ugaidi bila ya kutowa ufafanuzi zaidi. Repoti zinasema serikali inachunguza iwapo washambuliaji wa kujitowa muhanga wamehusika katika mashambulizi hayo.

Muda mfupi kabla ya miriouko ya Ankara. (10.10.2015)
Muda mfupi kabla ya miriouko ya Ankara. (10.10.2015)Picha: Reuters/M. Tombalak/dokuz8HABER

Kulikuwa na hali ya vurugu kufuatia miripuko hiyo wakati magari ya wagonjwa yakikimbilia kuwasaidia majeruhi huku polisi ikilifunga eneo hilo lilioko karibu na kituo cha reli.Shuhuda mmoja aliekuwa akilia amekaririwa akisema wailisikia mripuko mkubwa uliofuatia na mwengine mdogo kabla ya taharuki na hofu kutawala mahala hapo amesema "maandamano yaliokuwa yamepangwa kuendeleza amani yamegeuka kuwa mauaji,sifahamu hali hii".

Ukanda wa ridhaa wa kituo cha televisheni cha NTV umeonyesha wanaharakati wenye tabasamu wakishikana mikono na kucheza kabla ya kuanguka chini kufuatia mripuko mkubwa nyuma yao.Repoti zinasema mamia ya watu mjini Ankara wamekimbilia hospitali kutowa mchango wao wa damu kwa wahanga.

Shambulio baya kabisa

Mripuko huo ni mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya sasa ya Jamhuri ya Uturuki kupita miripuko miwili ya mabomu ya mwezi wa Mei mwaka 2013 huko Reyhanli iliyouwa zaidi ya watu 50.

Maandamano ya Ankara. (10.10.2010)
Maandamano ya Ankara. (10.10.2010)Picha: Getty Images/D. Karadeniz

Wakati wasi wasi wa kimataifa wa kukosekana kwa utulivu ukiongezeka kwa nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameihimza Uturuki kuwa kitu kimoja katika kupambana na magaidi.

Serikali ya Uturuki imepiga marufuku urushaji wa habari za mashambulizi hayo zenye kuonyesha taswira ya taharuki baada ya milipuko hiyo na miili ya damu ilioyozagaa barabani. Kufuatia miripuko hiyo watu wengi mjini Ankara hapo Jumamosi wameshindwa kuwa na mawasiliano na mtandao wa Twitter na mitandao mengine ya kijamii.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP/

Mhariri : Grace Kabogo