Miripuko yaitikisa Afghanistan wakati mahasimu wakijiapisha | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Miripuko yaitikisa Afghanistan wakati mahasimu wakijiapisha

Afghanistan imetumbukia zaidi katika mzozo wa kisiasa Jumatatu baada ya viongozi wawili hasimu - Rais Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah kujipaisha kuwa marais katika hafla mbili sawia zilizovurugwa na miripuko ya mabomu.

Mzozo mbaya kati ya rais Ashraf Ghani na mtendaji wake mkuu wa zamani Abdullah Abdullah umezusha hofu juu ya demokrasia tete ya Afghanistan, mnamo wakati Marekani inajiandaa kuondoka nchini humo kufuatia makubaliano ya mwezi Februari na kundi lenye nguvu na lililoungana na Taliban.

Uchaguzi ulifanyika mwezi Septemba, lakini ucheleweshaji wa mara kwa mara wa matokeo na tuhuma za udanganyifu vilimaanisha kwamba Ghani, rais wa sasa, alitangazwa tu kama mshindi mnamo mwezi Februari -- na kusababisha majibu ya hasira kutoka Abdullah, alieapa kuunda serikali yake sambamba.

Siku ya Jumatatu, Ghani, akivalia vazi la kitaifa la Afghanistan na kofia nyeupe, aliwasili kwenye kasri la rais ili kuapishwa, akizungukwa na wafuasi wake, wanasiasa waandamizi, wanadiplomasia na wageni kutoka mataifa ya nje, akiwemo mjumbe maalumu wa Marekani Zalmay Khalilzad.

Dakika kadhaa baadae, katika kona nyingine ya eneo la kasri la rais, Abdullah alievalia suti alijitawaza mwenyewe kuwa rais, akiahidi "kulinda uhuru, mamlaka ya taifa, na mipaka" ya Afghanistan.

Afghanistan Kandidaten Kabul Wahl

Hafla ya kuapishwa kwa rais Ashraf Ghani kwenye kasri la rais mjini Kabul.

Miripuko yatawnya wageni

Wakati mamia ya watu wakifuatilia hafla ya Ghani, miripuko miwili mikubwa ilisikika, na kusababisha baadhi ya watu kukimbia. Hakukua na ripoti zozote za maafa kutoka na miripuko hiyo, iliyoakisi tukio la Agosti 2018, wakati wapiganaji walipofyatua mizinga kadhaa wakati Ghani akitoa hotuba kwenye kasri hilo na kusababisha raia sita kujeruhiwa.

"Sijavaa vesti ya kuzuwia risasi, nina shati langu tu," Ghani alisema akiwaambia wale waliobakia nyuma huku vin'gora vikilia. "Nitabaki hata kama inamaanisha kutoa kafara kichwa changu."

Mwandishi wa shirika la habari la AFP aliwaona wengi waliokimbia wakirejea kwenye viti vyao baada ya hatua ya Ghani kukataa kuondoka kwenye jukwaa kusababisha vigelegele na makofi.

Malumbano yahatarisha makubaliano ya amani

Mapambano hayo ya kuwania madaraka yameutia majaribuni uvumilivu wa jumuiya ya kimataifa na raia wa Afghanistan pia, huku Marekani ikionya mapema kwamba mzozo huo unayaweka hatarini makubaliano ya kuondoka kwa wanajeshi wake, ambayo yanalitaka kundi la Taliban kufanya mazungumzo na serikali ya Kabul.

Migawiko inayozidi miongoni mwa wanasiasa wa Afghanistan inaweza kuwaacha waasi wa Taliban wakiwa na nafasi ya juu katika mazungumzo hayo. Lakini pia mzozo huo umewaacha raia wengi wakiwa wamekataa tamaa kuhusu mustakabali wa taifa lao.

"Haiwezekani kuwa na marais wawili katika taifa moja," alisema Ahmad Jawed, 22, aliewasihi viongozi hao "kuweka kando maslahi yao binafsi na kufikiria tu juu ya taifa lao badala ya kupigania madaraka."

Afghanistan Kabul Vereidigung Präsident Ashraf Ghani

Rais Ashraf Ghani akihutubia baada ya maroketi kadhaa kufyatuliwa wakati wa hotuba yake, Machi 9, 2020.

"Badala ya kuendesha hafla za kujiapishwa wanapaswa kuzungumza na kutafuta suluhu," aliliambia shirika la habari la AFP.

Ghani atoa mkono wa maridhiano kwa mahasimu wake

Wakati wa hotuba ya Jumatatu, Ghani alionekana kusogeza mkono wa maridhiano kwa wapinzani wake: "Leo ndiyo siku ya umoja tunapaswa kufikiria kuhusu mustakabali."

"Natoa wito kwa ----mahasimu (wa zamani) wa kisiasa kuungana nami ili tuhudumie taifa hili. Lengo letu ni amani na kukomesha miaka 40 ya vita, aliongeza.

Wafghanistan wameonyesha shauku ndogo sana kwa Abdullah, Ghani na mchakato wa uchaguzi kwa ujumla. Wengi wao hawakushiriki uchaguzi wa mwaka jana ambao ulishuhudia wagombea wakiwasilisha mawazo kidogo sana au sera.

Ukosefu wa ajira uko katika kiwango cha juu, na hata wahitimu wa vyuo vikuu kama Jawed wanapambana kutafuta ajira, huku vurugu zikiendelea bila kusita isipokuwa tu wakati wa wiki moja ya mapatano kuelekea makubaliano kati ya Marekani na Taliban.

Katika shambulio baya zaidi kuikumba Afghanistan katika muda wa wiki kadhaa, wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu waliwapiga risasi na kuwauwa watu 32 na kuwajeruhi wengine kadhaa kwenye mkutano wa kisiasa mjini Kabul siku ya Ijumaa.

Afghanistan Kandidaten Kabul Wahl

Abdullah Abdullah naye akiendesha hafla yake ya kuapishwa kama rais wa Afghanistan kwenye kona nyingine ya kasri la rais, Machi 9, 2020.

Taliban, ambalo limeukosoa mchakato wa uchaguzi kuwa "suala la uzushi linaloendeshwa na mataifa ya kigeni", limeongeza pia mashambulizi dhidi ya vikosi vya Afghanistan na raia. Msemaji wa waasi hao Zabihullah Mujahid aliliambia shirika la AFP kwamba hafla kinzani zinaonesha kwamba "hakuna kilichomuhimu zaidi kwa watumwa kuliko maslahi yao binafsi."

Usalama ulionekana kuimarishwa kwa ajili ya hafla hizo, ambapo barabara zilifungwa na vituo kadhaa vya ukaguzi kuundwa mjini Kabul saa kadhaa kabla ya wanaume hao wawili kuapishwa.

Malumbano kuigharimu serikali

Watalaamu wanasema malumbano ya ndani yanaweza kuigharimu serikali, ambayo tayari inakabiliwa na shinikizo baada ya kuachwa nje ya majadiliano ya Doha kwa ajili ya makubaliano ya Marekani na Taliban.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliosaniwa nchini Qatar, wanajeshi wa kigeni wataondoka kutoka Afghanistan katika muda wa miezi 14, kwa ahadi kadhaa za kiusalama kutoka kwa Taliban pamoja na kushiriki mazungumzo na serikali ya Kabul.

Mchambuzi wa kisiasa Atta Noori alisema malumbano kati ya Ghani na Abdullah yanaweza kuathiri vibaya msimamo wa serikali katika mazungumzo yajayo ya wa Afganistan." "Umoja ndiyo nija pekee ya kusonga mbele ikiwa wanataka kushindwa kwenye meza ya mazunguzo," alisema.

chanzo: afpe