1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko miwili ya bomu yauwa watu 27 Libya

Amina Mjahid
24 Januari 2018

Watu 27 wameuawa na wengine wamejeruhiwa vibaya baada ya mashambulizi mawili ya mabomu kutokea Mjini Benghazi Mashariki mwa Libya katika shambulizi hilo lililotokea jana usiku na ambalo lililengwa kuwadhuru watu wengi.

https://p.dw.com/p/2rPsx
Lybien Anschlag in Bengasi
Picha: Reuters

Kulingana na msemaji wa jeshi kapteni Tarek Alkharraz, pamoja na maafisa wa polisi mjini Benghazi, Mripuko wa kwanza ulitokea katika eneo la Salmani mwendo wa saa mbili na dakika ishirini usiku hapo jana , huku bomu la pili likiripuka nusu saa baadaye wakati wakaazi na wahudumu wa afya walipokusanyika kuwaokoa waliyojeruhiwa katika mkasa huo. Afisa mmoja wa afya Hani Belras Ali amesema watu 27 wameuwawa  huku wengine 32 wakijeruhiwa vibaya.

Hadi sasa hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na mashambulizi hayo, lakini Umoja wa Mataifa umelaani tukio hilo kupitia mtandao wake wa kijamii, ukisema kwamba mashambulizi ya moja kwa moja au yale ya kiholela dhidi ya raia hayakubaliki chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu na kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita.

Libya ilitumbukia katika machafuko tangu kuuwawa kiongozi wake Moammar Gadhafi

Libyen Bengasi Libyan National Army LNA Soldaten
Picha: Getty Images/AFP/A. Doma

Libya ilitumbukia katika machafuko kufuatia kuondolewa na kuuwawa kiongozi wake wa muda mrefu Moammar Gadhafi mwaka 2011 na kuanzia mwaka 2014 nchi hiyo, iligawika katika makundi mawili kati ya serikali mbili zinazohasimiana na mabunge mawili moja eneo la Magharibi na jengine eneo la Mashariki yote yakiungwa mkono na makabila na makundi tofauti ya waasi.

Kutokana na hilo wapiganaji wa kundi la dola la kiislamu walichukua mwanya huo kujaribu kujiimarisha nchini Libya lakini walifurushwa na kuondolewa katika miji muhimu nchini humo.

Hata hivyo kwa sasa mji wa Benghazi unabakia kuwa eneo linalokumbwa na machafuko ya mara kwa mara ambako mabomu na mashambulizi tofauti bado hutokea. Mji huo hivi karibuni umekumbwa na mapigano kati ya makundi yaliyomatiifu kwa Khalifa Hifter, anayeliongoza jeshi la kitaifa la Libya katika eneo la Mashariki.

Mwezi Julai mwaka jana Hiftar alitangaza ukombozi kamili wa mji wa Benghazi miaka mitatu baada ya jeshi lake kuanzisha operesheni za kijeshi za kuuokoa mji huo kutoka kwa wapiganaji wa jihadi waliyoufanya mji huo ngome yao kufuatia mapinduzi yaliyofanyika.

Hiftar anaunga mkono bunge lililoko Mashariki mwa Libya huku Umoja wa Mataifa ukiunga mkono serikali ya pamoja iliyoko mjini Tripoli inayojitahidi kutambulika kitaifa.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman