1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milliband aongoza baada ya mdahalo

17 Aprili 2015

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour nchini Uingereza Ed Milliband ameshinda mdahalo wa mwisho wa televisheni kuhusu uchaguzi mkuu uliokwepwa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

https://p.dw.com/p/1F9yK
Ed Miliband kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour nchini Uingereza katika mdahalo wa uchaguzi.(16.04.2015)
Ed Miliband kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour nchini Uingereza katika mdahalo wa uchaguzi.(16.04.2015)Picha: Reuters

Chama cha Conservative cha Waziri Mkuu David Cameron na mpinzani wake mkuu chama cha Labour cha Ed Milliband viko sambamba katika mchuano huo na vyote viwili yumkini ikabidi vitegemee kushirikiana na vyama vidogo vya kisiasa kuweza kuunda serikali ya mseto.

Waziri Mkuu Cameron ameshutumiwa kwa kutohudhuria mdahalo huo na mpinzani wake mkuu Ed Milliband amempa changamoto moja kwa moja mbele ya kamera kumtaka ajadili naye ana kwa ana masuala ya kuongoza nchi hiyo.

Miliiband amesema " David,iwapo unafikiri uchaguzi huu ni kuhusu uongozi,jadili na mimi ana kwa ana.Jadiliana na mimi na uwache wananchi waamuwe."

Cameron haukuupa umuhimu mdahalo huo na amekataa kushiriki ili kuepuka hatari ya kuharibu kuungwa kwake mkono ambako kiwango chake kilikuwa cha juu kuliko Miliband.

Cameron asakamwa

Washiriki wa mdahalo huo waliuliza masuala kuhusu makaazi,ulinzi,matumizi ya shughuli za serikali kwa umma na uhamiaji.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.Picha: Reuters/T. Melville

Kiongozi wa chama cha Kizalendo cha Scotland SNP Nicola Sturgeon ambacho kinaweza kuwa na usemi wa kuunda serikali ya mseto baada ya uchaguzi huo wa Mei saba pia amemshutumu Cameron kwa kuukwepa mdahalo huo na kurudia tena pendekezo la kushirikina na chama cha Labour kumn'gowa Cameron madarakani.

Sturgeon amesema "Nafikiri ni fedheha kwa David Cameron kutokuwepo hapa usiku huu kutetea rekodi yake.Tuna fursa ya kumn'gowa David Cameron kutoka makao makuu ya serikali ya Downing Street.Usilipe mgongo suala hili wananchi katu hawatokusamehe."

Lakini Milliband amelikataa wazo hilo la kushirikiana na chama ambacho kinapigania uhuru wa Scotland na kutaka kuvunjwa kwa Umoja wa Uingereza na kusisitiza kwamba anakusudia kupata ushindi wa viti vingi kuweza kuunda serikali moja kwa moja.

Milliband aongoza

Uchunguzi wa maoni uliochapishwa baada ya dakika 90 za mdahalo huo umedokeza kwamba Milliband alishinda kwa kujipatia asilimia 35 akifuatiwa na Nicola Sturgeon aliyepata asilimia 31.

Washiriki wa mdahalo wa televisheni wa uchaguzi mkuu wa Uingereza.(16.04.2015)
Washiriki wa mdahalo wa televisheni wa uchaguzi mkuu wa Uingereza.(16.04.2015)Picha: AFP/Getty Images/S. Rousseau

Baadhi ya wahakiki wanasema uchunguzi huo wa maoni ulikuwa umeegemea upande wa wafuasi wa Labour.

Kwa kutohudhuria mdahalo huo uliovishirikisha vyama vyengine vidogo vya kisiasa Cameron amejianika kwenye nafasi ya uwoga wa kisiasa na mara kwa mara Milliband allitumia fursa hiyo kumtaka wajadiliane ana kwa ana masuala ya kitaifa.

Hapo Aprili 30 wiki moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu wa Uingereza Cameron,Milliband na Nick Clegg wa chama cha Liberal Demokrat mshirika mdogo wa chama cha Conservative cha Cameron katika seikali ya mseto watashiriki katika halfla ya mwisho ya televisheni ambapo watajibu masuali ya wapiga kura bila ya kuwa na mdahalo kati yao.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahmed