1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milioni 30 waambukizwa virusi vya corona duniani

Angela Mdungu
22 Septemba 2020

Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona duniani kote imepindukia milioni 30, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, huku Shirika la Afya Duniani likisema kiwango cha maambukizo barani Ulaya kinatia wasiwasi.

https://p.dw.com/p/3iqek
Tschechien Prag | Coronakrise
Picha: David W Cerny/Reuters

Hata hivyo, idadi hii ya watu walioambukizwa zinaakisi sehemu tu ya jumla halisi ya maambukizo ya virusi vya corona duniani, kwani hizi ni taarifa zinazotokana na mamlaka rasmi za mataifa husika pamoja na WHO. Uwezekano ni kwamba wale wanaoambukizwa bila kuripotiwa kwenye mamlaka hiyo ni wengi zaidi.

Hadi sasa, vifo vinavyotokana na virusi hivyo ni takribani laki 943,086 tangu lilipoanza janga hilo nchini China mwaka uliopita.

Marekani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na maambukizo mengi, ikiwa na watu milioni 6 waliaombukizwa na vifo 197,364. India inafuatia ikiwa na zaidi ya watu milioni 5 walioambukizwa na vifo zaidi ya 83,000, huku Brazil ikiwa na takribani na watu milioni nne walioupata ugonjwa huo na vifo vinavyozidi 134,000.

Uingereza kurejesha hatua za tahadhari

Kutokana na ongezeko la maambukizo ya virusi hivyo, mataifa mengine yameanza kufikiria kuchukua tahadhari ili kukabiliana na wimbi la pili la maambukizo.

Großbritannien, London | Boris Johnson im Parlament
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anataka hatua mpya za hadhari dhidi ya virusi vya corona.Picha: PRU/AFP

Kwa upande wake, serikali ya Uingereza inapanga kutangaza hatua mpya za kupambana na corona, baada ya mshauri mkuu wa masuala ya kisayansi nchini humo, Patrick Vallance, kuonya kuwa nchi hiyo inaweza kushuhudia maambukizo mapya 50,000 kila siku ifikapo mwezi ujao iwapo haitachukua hatua madhubuti.

Migahawa na baa kote nchini humo zitapaswa kufungwa kuanzia saa 4:00 usiku kuanzia Alkhamis, wakati wakaazi wa baadhi ya maeneo watapigwa marufuku ya kuwa na muingiliano na watu wengine wa nje ya nyumba zao.

Hatua hizi zilitarajiwa kutangazwa na Waziri Mkuu Boris Johnson Jumanne (Septemba 21) jioni.

Wajerumani wazidi kuandamana kupinga hatua za tahadhari

Hata hivyo, mapambano dhidi ya virusi yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na raia katika baadhi ya mataifa kupinga hatua zinazochukuliwa katika kupambana na janga hilo.

70. Geburstag der Zentralrat der Juden
Serikali ya Ujerumani inasema kuwa hatua zake ya hadhari zimesaidia sana kupunguza kasi ya maambukizo.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Katika jimbo tajiri la Bavaria nchini Ujerumani, kwa mfano, takribani watu 10,000 walikusanyika katika maandamano mjini Munich yaliyolenga kupinga hatua za kupambana na corona, watu hao wakiwa ni mara mbili ya wale waliojiandikisha kuhudhuria mkusanyiko huo.

Mwezi uliopita pia makumi kwa maelfu ya watu walikusanyika katika mji mkuu, Berlin, kupinga hatua za tahadhari zinazochukuliwa kupambana na COVID-19 wakiziita kuwa ni za kidikteta.

Siku ya Jumamosi, Kansela Angela Markel alitetea hatua zinazofuatwa na serikali yake kupambana na maambukizo ya virusi vya corona, lakini alisema kuwa wako "tayari kukosolewa na kujadili maamuzi ya serikali."