1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milio ya risasi na makombora yamelipuka Mogadishu

19 Februari 2021

Milio ya risasi na makombora yamelipuka katikati mwa mji wa Mogadishu wakati majeshi ya serikali ya Somalia yalipofunga barabara za mitaani kuwazuia waandamanaji waliokasirishwa na hatua ya kuchelewesha uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3paY4
Somalia Mogadischu | gepanzerter Mannschaftstransporter auf Straße
Picha: Feisal Omar/REUTERS

Makabiliano hayo yameibuka saa chache kabla ya kuanza kwa maandamano yaliyopangwa na upinzani. Inaarifiwa kuwa takriban watu wawili wameuwawa na wengine wamejeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya jeshi na wapiganaji.

Video iliyotumwa kwa shirika la habari la Reuters wakati wa maandamano ya kupinga serikali iliwaonyesha raia waliovalia barakoa wakipeperusha bendera ya Somalia wakitawanyika kutokana na milio ya risasi.

Magari ya kivita yaliizunguka ikulu ya rais baada ya mapigano, huku vikundi vya upinzani na wakuu wa koo wakiunga mkono maandamano dhidi ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo.

Kenia Nairobi | Präsident Somalia | Mohamed Abdullahi Mohamed
Rais Mohamed Abdullahi MohamedPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Awali mpinzani maarufu Abdirahman Abdishakur Warsame Wadajir alituma video inayoonyesha akiongoza umati mdogo wa waandamanaji barabarani, licha ya serikali kupiga marufuku maandamano.

Saa kadhaa kabla ya hapo, rais wa zamani wa Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, aliwashutumu wanajeshi wa serikali kwa kuishambulia hoteli ambayo alikuwepo pamoja na rais mwingine wa zamani kabla maandamano ya Ijumaa.

Haikufahamika ni nani aliyefyatua risasi kwanza, lakini Yusuf Mohamed mmoja ya walioshuhudia tukio hilo ameripoti makabiliano makali ya kurushiana risasi kati ya vikosi vya usalama na walinzi wenye silaha wanaowalinda wafuasi wa upinzani ambao walianza maandamano yao kando ya barabara kuu ya uwanja wa ndege.

Waziri wa Usalama wa Somalia, Hassan Hundubey Jimale amedai kuwa upinzani ndio ulianzisha mapigano hayo.

Somalia Tabda|  Kenianische Soldaten | Militäroffensive
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Somalia imekuwa ikigubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu 1991 huku serikali na upinzani wakitumia wafuasi wenye silaha kukabiliana.

Muda wa rais Farmajo ulimalizika mwanzoni mwa mwezi Februari, lakini atasalia madarakani hadi tarehe mpya ya uchaguzi itakapokubaliwa hii ni baada ya mazungumzo ya kisiasa kushindwa kufikia muafaka wa tarehe ya uchaguzi mpya.

Mazungumzo hayo, yaliyojumuisha wawakilishi wa koo mbalimbali za Somalia, yalilenga kuweka taratibu za urais pamoja na kukubaliana juu ya wanachama wa tume ya uchaguzi.

Kucheleweshwa kwa uchaguzi sio sababu pekee ya kuongezeka kwa mvutano Somalia wanapozozania udhibiti wa nchi bali pia wanamgambo wa al-Shabaab wamekuwa wakifanya mashambulizi mara kwa mara.

Vikosi kutoka Umoja wa Afrika na Marekani vinaiunga mkono Serikali ya Somalia katika mapambano dhidi ya al-Shabaab.

 

Vyanzo/ dpa/ Reuters