1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili ya waliofariki katika mkanyagano Moshi yaangwa

Admin.WagnerD3 Februari 2020

Rais wa Tanzania ataka mapungufu ya utayarishaji wa mikutano ya umma yashughulikiwe, katika taarifa yake ya kuagwa kwa miili 20 ya watu waliofariki dunia katika mkusanyiko wa kidini mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

https://p.dw.com/p/3XDK2
Tansania Moshi Beerdigung
Picha: DW/V. Natalis

Mkusanyiko mkubwa wa watu umeshuhudiwa katika viwanja vya jamhuri vilivyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuaga miili hiyo. Wananchi, viongozi wa dini, serikali na vyama vya siasa kutoka mikoa mitatu ya kanda ya kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro na Manyara wamefika kutoa heshima zao za mwisho. Katika ibada hiyo mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amesema kuwa Rais wa Tanzania John Magufuli hawezi kuzuia mikutano ya dini.

Mghwira amewataka watu wote kuabudu kwa uhuru kulingana na imani zao, lakini amewasisitiza watu kutafuta maarifa katika maandiko matakatifu wanayoyaamini na kuancha kukimbilia miujiza pekee.

Tansania Moshi Beerdigung
Watu waliohudhuria ibada ya kuiaga miili ya watu 20 waliofariki katika mkanyagano uliotokea katika mkusanyiko la kidini Moshi, Tanzania.Picha: DW/V. Natalis

Wengi waliokwenda katika ibada hiyo ya kukanyaga mafuta walitarajia kupata uponyaji kutokana na matatizo mbali mbali yanayowakabili ikiwepo magonjwa, migogoro ya kifamilia na masuala ya kiuchumi. Baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria katika ibada hiyo ya kuaga miili wamesema tukio hilo kamwe haliwezi kuzima imani ya kweli ya Kikristo. Dr. Askofu Dr. Stanley Hotay ni mwakilishi wa umoja wa makanisa Tanzania CCT.

Watu hao walifariki dunia siku ya Jumamosi katika viwanja vya majengo vilivyopo mijini Moshi mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania, baada ya kukanyagana wakati wakigombea mafuta yanayoelezwa kuwa ni ya upako katika mkutano wa injili ulioongozwa na mchungaji Boniphace Mwamposa. Tayari jeshi la polisi linamshikilia mtumishi huyo.