Migomo, maandamano yaitikisa Ugiriki | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Migomo, maandamano yaitikisa Ugiriki

Vyama vya wafanyikazi nchini Ugiriki vimeitisha mgomo wa masaa 24 ili kupinga hatua ya serikali kufunga shirika la utangazaji la serikali la ERT kama hatua ya kupunguza matumizi.

Studio za Televisheni ya taifa ya Ugiriki ERT.

Studio za Televisheni ya taifa ya Ugiriki ERT.

Maandamano hayo ya leo yaliopangwa na vyama viwili vikubwa vya wafanyikazi yalivuruga usafiri wa umma na kusababisha hospitali kuhudumu kwa wafanyikazi wachache, huku usafiri wa ndege ukipaswa kusimamishwa kati ya saa kumi na saa kumi na mbili jioni ya leo.

Waandamanaji wakipeperusha bendera nje ya makao makuu ya Televisheni ya Taifa, ERT wakipinga kufungwa kwa televisheni hiyo.

Waandamanaji wakipeperusha bendera nje ya makao makuu ya Televisheni ya Taifa, ERT wakipinga kufungwa kwa televisheni hiyo.

Waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras bado anasisitiza kuwa shirika hilo la ERT litaendelea kufungwa na wafanyikazi wote 2,600 watakuwa bila kazi hadi pale stesheni mpya ya serikali itakapofunguliwa.

Uchaguzi wa mapema

vyombo vya habari vya Ugiriki vimezungumzia kuhusu matarajio ya uchaguzi wa mapema, wakionya kuwa safari hii Samaras angeweza kusukuma washirika wa muungano mbali sana.

Wasosholisti na chama cha wachache cha mrengo wa kushoto wanaounga mkono serikali hiyo ya Ugiriki tayari wanakumbwa na shinikizo la ndani juu ya hatua kali zisizo maarufu, Ugiriki imekuwa ikitumia kwa kipindi cha miaka minne.

Gazeti la Kathimerini daily la kiliberali la Ugiriki limesema suluhu ipatikane kwa kipindi cha wiki moja au kuwe na uchaguzi huku gazeti la mrengo wa kati likizungumzia kuhusu michezo hatari ya sarakasi.

“Iwapo kutakuwa na hali ya kutoafikiana, mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi wa mapema yatakuwa na nguvu zaidi,” lilisema Kathimerini.

Samaras alionekana kuchukua hatua ya nyuma hapo jana, baada ya wasosholisti na vyama vya wachache vya mrengo wa kushoto vinavyounga mkono muungano wa serikali, kusema hatua hiyo ya kufunga shirika la ERT ni hatua isiyokubalika.

Wafanyakazi wa ERT wameendelea kutangaza habari za moja kwa moja kupitia mtandao wa intaneti asubuhi ya leo.

Wafanyakazi wa ERT wameendelea kutangaza habari za moja kwa moja kupitia mtandao wa intaneti asubuhi ya leo.

Samaras kujadiliana na washirika wake

Duru kutoka serikalini humo zinasema kuwa waziri mkuu huyo ataitisha mkutano na washirika wake kujadiliana kuhusu suala hilo.

Hapo awali Samaras alitetea hatua ya kufunga shirika hilo, akisema wanaondoa matumizi yasio hitajika na kwamba wanalinda maslahi ya umma.

Vituo vya runinga na radio vilizimika ghafla hapo jana, na takriban wafanyikazi 2,700 wa vituo hivyo walifutwa kazi kama hatua ya serikali ya muungano ya Ugiriki kupunguza matumizi.

Polisi wa kutuliza ghasia waliwekwa nje ya ofisi za ERT nchini kote ili kuzuwia uharibifu wowote kufuatia maandamano hayo ya leo.

Mwandishi: Dalila Athman/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com