Michuano ya kufuzu katika dimba la CHAN yaanza | Michezo | DW | 22.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michuano ya kufuzu katika dimba la CHAN yaanza

Michuano ya kufuzu ya dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani - CHAN iimeanza na baadhi ya matokeo ya michuano hiyo yamesababisha makocha kupigwa kalamu.

Tanzania imemtimua kocha Mholanzi Mart Nooij, Malawi ikampiga teke Young Chimodzi, nayo Msumbiji ikamwambia kwaheri Joao Chisano.

Hii ni baada ya timu hizo zote zilipoteza mechi zao kza mwishoni mwa wiki. Chimodzi alipoteza kazi baada ya Malawi kushindwa mbili moja nyumbani dhidi ya Zimbabwe, wakati Chisano akifungasha virago baada ya Msumbiji kurambishwa moja bila na Rwanda.

Malawi na Msumbiji kisha zikachukua uamuzi wa haraka kuwapa majukumu ya uongozi wa muda wachezaji wa zamani wa timu za taifa Ernest Mtawali na Helder ‚ Mano Mano‘ Muianga.

Shirikisho la kandanda la Tanzania TFF limesema mrithi wa Nooij mwenye umri wa miaka 61, atatangazwa karibuni. Katika matokeo mengine Ethiopia iliishinda Kenya mbili bila wakati Zimbabwe ikipata matokeo sawa na hayo dhidi ya Visiwa vya Comoro.

Djibouti ilitoka sare ya goli moja kwa moja na wageni Burundi wakati Lesotho na Botswana zikitoka sare tasa katika mchuano mwingine. Mechi za marudiano zitachezwa wikendi ijayo huku nyingine zikichezwa wikendi ya kwanza ya mwezi wa Julai.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman