Michuano ya AFCON yafungua pazia nchini Misri | Matukio ya Afrika | DW | 22.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Michuano ya AFCON yafungua pazia nchini Misri

Michuano ya 32 ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika imefungua pazia lake nchini Misri jana Ijumaa kwa mchezo kati ya wenyeji Mafarao wa Misri  dhidi ya timu ya taifa ya Zimbabwe.

Katika mchezo huo wa kundi A wenyeji Misri wameichapa Zimbabwe bao moja kwa bila mbele ya zaidi ya mashabiki 70,000 waliofurika katika uwanja wa kimataifa wa michezo mjini Cairo.

Kiungo wa timu ya taifa ya Misri, Mahmoud Trezeguet ndiye aliyewatoa kimasomaso wenyeji hao wa michuano ya 32 ya kombe la mataifa ya Africa wakati wa mechi hiyo ya ufunguzi iliyokuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wa kandanda nchini Misri.

Bao lake la mnamo dakika ya 41 lilisadifu kuwa muhimu kuiwezesha timu yake kijinyakulia alama tatu za mapema katika fainali hizo zitakazoendelea karibu mwezi mzima.

Bao la Trezeguet liliibua shangwe na kuizima kwa muda nyota ya mshambuliaji mashuhuri anayeichezea ligi ya Premier Mohamed Salah ambaye alishangiliwa kwa nguvu mara zote alipougusa mpira.

Salah alipata nafasi mbili muhimu katika dakika za awali za mchezo na baadaye wakati wa kipindi cha pili lakini hakufanikiwa kutikisa nyavu za wazimbabwe.

Timu ya taifa ya Misri ambayo ni kigogo katika  historia ya michuano ya AFCON inasaka kuchukua ubingwa kwa mara ya nane baada ya kushinda mara ya saba mwaka 2010.

Zimbabwe walidorora?

Kwa upande wao wachezaji wa timu ya taifa ya  Zimbambwe walionekana kutokuwa na ari ya mchezo ikizingatiwa waliingia uwanjani siku moja ya kutishia kususia fainali hizo kwa sababu ya kutolipwa madai yao.

Kitisho cha mgomo wa wachezaji wa Zimbabwe kilizua wasiwasi wa kutokea aibu kubwa kwa mpira wa miguu barani Africa ambao tayari unakabiliwa na changamoto chungu nzima.

Wachezaji wa Zimbabwe walikataa kufanya mazoezi siku ya Alhamisi wakishinikiza kulipwa marupupurupu ya kushiriki michuano hiyo pamoja na deni jingine la kushiriki michuano ya kikanda iliyofanyika mwezi uliopita.

Mgomo wao ulimalizwa baada ya kukutana na maafisa wa CAF kwa mazungumzo.

Ulinzi waimarishwa nchini Misri

Michuano ya AFCON ya mwaka huu 2019 imeongezea idadi ya timu zinazoshiriki kufikia 24 badala ya 16 na inafanyika wakati wa majira ya joto yanayofahamika kwa joto kali.

Mtangane wa kufungua pazia, ulitanguliwa na sherehe za ufunguzi zilizojumuisha onesho kabambe la sanaa na muziki wa kiafrika.

Rais wa Misri Abdelfattah al-Sisi, rais wa Shirikisho la  Kandanda Ulimwenguni, FIFA  Gianni Infantino pamoja na rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika, CAF, Ahmad Ahmad walihudhuria sherehe za ufunguzi.

Mapema kabla ya kuanza kwa mechi hiyo makumi kwa maelfu ya mashabiki walijipanga kwa zaidi ya saa 12 kuweza kuingia uwanjani kushuhudia sherehe za ufunguzi na mchezo wa kwanza.

Ulinzi umeimarishwa kote nchi Misri kukabiliana na wasiwasi wa mashambulizi ya kigaidi na michuano hiyo inafanyika siku chache baada ya kifo cha rais wa zamani wa taifa hilo Mohamed Morsi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo kiasi askari 15,000 watahusika na ulinzi wakati wa fainali hizo zinazochezwa kwenye viwanja sita vilivyo kwenye miji minne ya Cairo Alexandria, Suez  na Ismailia.

 

DW inapendekeza