Michezo ya Olmypik China yabakisha kumbukumbu ya muda mrefu | Michezo | DW | 25.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michezo ya Olmypik China yabakisha kumbukumbu ya muda mrefu

China yajipongeza kwa kufanikiwa kuandaa Michezo ya Olympik yenye shani kubwa ambayo imeliacha taifa hilo kuwa la kujiamini na la wazi,Kenya nayo yajipongeza kwa mafanikio makubwa iliowahi kupata katika Olympik.

default

Wasanii wakionyesha vitu vyao wakati wa kufungwa kwa Michezo ya Olympik mwaka 2008 mjini Beijing China Jumapili ya tarehe 24 mwezi wa Augusti 2008.

China imemaliza Michezo ya Olympik mwaka 2008 kwa kuwa juu kabisa ya mezani ya medali ambapo ilijinyakulia medali 51 za dhahabu, 21 za fedha na 28 za shaba.

Wakati medali jumla 100 za China zimepitwa na Marekani ilioshika nafasi ya pili ambayo ina medali jumla110 za dhahabu zikiwa 36 taifa hilo mwenyeji wa michezo ya Olympik mwaka huu linaweza kuangalia nyuma kwa fahari kutokana na kukidhi matarajio yake ya kimichezo.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 72 kwamba nchi mbali na Marekani na Urusi imeweza kujisombea medali nyingi za dhahabu katika michezo hiyo ya Olmypik ya majira ya kiangazi na kuashiria mustakbali ambapo China inaonekana kama linakuwa taifa kubwa la michezo duniani.

Kujiimaarisha huko kwa China katika michezo kumekuwa kwa vishindo baada ya kushika nafasi ya pili katika Michezo ya Olympik ya Athens mwaka 2004 ambapo ilijipatia medali 34 za dhahabu ikitanguliwa na Marekani iliokuwa na medali 36 za dhahabu.

China ilijipatia medali yake ya kwanza ya dhahabu katika Michezo ya Olympik ya Los Angeles Marekani hapo mwaka 1984 wakati katika michezo ya Sydney Australia hapo mwaka 2000 ilizowa medali 28 za dhahabu.

Mjini Beijing China ilijipatia medali nyingi za dhahabu kuliko taifa jengine lolote lile katika mchezo wa viungo,kuogelea kwa kupiga mbizi,bedminton, mpira wa mezani,kutunga shabaha na kuinuwa vitu vizito.

Wanamichezo wa China hususan walitamba katika uogeleaji wa kupiga mbizi ambapo walinyakuwa medali saba za dhahabu kati ya nane na katika mpira wa meza walizowa medali zote nne za dhahabu na kujiongezea medali mbili za fedha na mbili za shaba.

Kwa upande wa Afrika Kenya imeinuwa uso wa bara hilo baada ya nchi hiyo kujisombea medali 14 zikiwemo tano za dhahabu.

Ushindi wa hapo jana wa Samuel Wanjiru katika mbio ndefu ambayo ni medali ya kwanza kabisa ya dhahabu katika fani hiyo kwa Kenya umeiweka Kenya katika nafasi ya 15 katika meza ya medali ikiwa mbele kwa nafasi tatu ya mpinzani wake mkubwa wa Afrika Ethiopia.

Kenya hususan imekuwa ikijivunia wanariadha wake wa kike ambapo Pamela Jelimo na Nancy Jebet Langat walipeleka nyumbani medali za kwanza za dhahabu kwa wanawake wa Kenya katika mbio za mita 800 na mita 1,500.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya amesema katika taarifa kwamba ni mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano kwa wanariadha wa kike wa Kenya kujishindia medali mbili za dhahabu. Amesema ushindi wao na wanariadha wenzao wa kiume umeliletea taifa hilo heshima.

Washindi wa medali ya dhahabu wa Kenya watazawadiwa shilingi za Kenya milioni 1.75 sawa na dola 25,000 za Marekani.

Uingerea itakuwa mwenyeji wa michezo ya Olympik mwaka 2012.Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown wakati akiimgwajia sifa China kwa kuandaa vizuri Michezo hiyo ya Olymik iliomalizika jana hakusita kuipigia debe nchi yake.

Lakini muulize mtu yoyote yule nani ni wanamichezo nyota katika michezo hii jibu la haraka yumkini litakuwa ni muogeleaji Michael Phelps wa Marekani aliejishindia medali nane za dhahabu na mwanariadha wa Jamaica Usain Bolt aliyeshinda medali tatu za dhahabu.

Michezo hiyo ya Olympik imemalizika hapo jana kama ilivyoanza kwa mbwembwe kubwa za aina yake ambazo zitaiweka China katika kumbukumbu za ulimwengu kwa kipindi kirefu kijacho.

 • Tarehe 25.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F4Ot
 • Tarehe 25.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F4Ot
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com