1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Michezo ya Olimpiki msimu wa baradi yaanza rasmi Beijing

Bakari Ubena4 Februari 2022

China inazindua michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi kwa kujigamba na kuonyesha uwezo wake kimataifa licha ya baadhi ya serikali za Magharibi kususia kidiplomasia.

https://p.dw.com/p/46XeL
Eröffnungsfeier | Olympische Winterspiele 2022 | Peking, China
Picha: ANNEGRET HILSE/REUTERS

Sherehe za uzinduzi zilianza mara tu baada ya kuwasili kwa Rais wa China Xi Jinping na Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Thomas Bach, kwenye Uwanja wa Taifa uliokuwa mwenyeji tukio la uzinduzi wa Olimpiki la mwaka 2008.

China limekuwa taifa la kwanza kwa kuwa mwenyeji wa michezo ya msimu wa baridi na ile ya majira ya joto. Viongozi kadhaa wa kimataifa wamepanga kuhudhuria sherehe hizo za ufunguzi. Waliyo maarufu zaidi ni pamoja na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye kabla ya hapo, alizungumza na Rais Xi faraghani wakati kukiwa na mzozo hatari kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine.

Soma pia : Rais Vladmir Putin amewasili mjini Beijing.

Utendaji wa China

Michezo ya Olimpiki na sherehe ya ufunguzi huwa daima ni mtihani mkubwa wa utendaji kwa taifa mwenyeji wa michezo hiyo, lakini pia nafasi ya kuonyesha utamaduni wa nchi husika na kudhihirisha nafasi yake ulimwenguni, haswa kwa kuonyesha mambo yaliyo bora, jambo ambalo China imekuwa ikilitenda kwa miongo kadhaa.

Lakini katika Michezo ya Beijing ya mwaka huu, tofauti kati ya utendaji na ukweli ni wa kushangaza. Miaka kumi na minne iliyopita, sherehe za ufunguzi wa Beijing ambazo ziligubikwa na maonyesho makubwa, ziliweka kiwango kipya na cha juu katika michezo ya Olimpiki na tangu wakati huo hakuna nchi yeyote iliyofikia kiwango hicho.

Baadhi wasusia hafla ya uzinduzi

Eröffnungsfeier | Olympische Winterspiele 2022 | Peking, China
Picha: EVGENIA NOVOZHENINA/REUTERS

Kwa Beijing, michezo hii ya Olimpiki ni uthibitisho wa nguvu na hadhi yake duniani. Lakini kwa wengi waliopo nje ya China, haswa katika nchi za Magharibi, wamekua wakithibitisha kuwa nchi hiyo imezidi kuwa ya kimabavu zaidi.

Mamlaka za China zinakandamiza harakati za kuunga mkono demokrasia, zimeimarisha udhibiti wao kwa Hong Kong, zimeendeleza mzozo na Taiwan lakini zaidi wamekuwa wakiwatesa Waislamu wa Uyghur, ukandamizaji ambao serikali ya Marekani na wengine wameuita mauaji ya kimbari.

Virusi vya corona pia ni tishio kubwa kwenye Michezo ya mwaka huu, kama ilivyokuwa katika michezo ya majira ya joto huko Tokyo. Zaidi ya miaka miwili tangu maambukizi ya kwanza ya COVID-19 yaripotiwe katika mkoa wa Hubei huko China, takriban watu milioni 6 wamekufa na mamilioni ya wengine kuambukiwa duniani kote.

Soma pia: Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi yaandamwa na rekodi ya haki za binadamu ya China

Hatma ya Peng Shuai

Katika kuelekea michezo hii ya Olimpiki, China inajaribu pia kuuficha utata unaomhusu mchezaji nyota wa tenisi wa nchi hiyo Peng Shuai, aliyetoweka hadharani mwaka jana baada ya kumshutumu afisa wa zamani wa Chama cha Kikomunisti kwa unyanyasaji wa kijinsia. Tuhuma zake zilifutwa haraka mtandaoni, na mjadala juu ya tukio hilo umedhibitiwa mno.