1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo Wiki hii

12 Machi 2010

Drogba achaguliwa tena "mwanasoka wa mwaka wa Afrika".

https://p.dw.com/p/MRYT
Didier Drogba -mchezaji wa mwaka wa Afrika.Picha: picture-alliance/dpa

Kombe lijalo la dunia likinyemelea hapo Juni, mwaka huu nchini Afrika Kusini, kocha wa wenyeji Bafana Bafana,mbarzuil Carlos Alberto Parreira,anatumai timu yake hiyo itajifunza kucheza staili ya Brazil katika Kombe hilo la dunia.Vipi Afrika Kusini inavyotembeza utalii wake kupitia Kombe la dunia ? Thelma Mwazaya atatuarifu kutoka maonesho ya utalii Berlin ?

Tunawajulisha nani Didier Drogba ,nahodha wa Tembo wa Ivory Coast,aliechaguliwa wiki hii "Mchezaji bora wa dimba wa mwaka wa Afrika".Na kinyan'ganyiro cha Bundesliga kimegeuka sasa cha timu 3:Bayern Munich,Bayer Leverkusen na Schalke 04. Na Je, Manchester United, itauachia tena usukani wa premier League,kurudi kwa Chelsea ikiwa na miadi kesho (Jumapili) na Fulham ?

Katika Bundesliga, Bayern Munich, leo (Jumamosi) inacheza na Freiburg wakati mahasimu wao Schalke, jana (ijumaa) walikuwa na miadi na Stuttgart.Leverkusen kesho, ina kibarua kigumu ikicheza na Hamburg.

Katika Premier League, Manchester United, inacheza na Fulhalm kesho wakati wenzao wa mtaani,Manchester City, wameitembelea Sunderland.Chelsea iko nyumbani mwenyeji wa West Ham united.Hull City, inaikaribisha leo Arsenal.

Afrika Kusini,ndie mwenyeji wa Kombe lijalo la dunia ,la kwanza barani Afrika Juni, mwaka huu.Isitoshe, ni moja kati ya timu 6 zitakazo pepea bendera ya Afrika baina ya juni 11 pale Bafana Bafana, itakapofungua dimba na Mexico, hadi finali Julai 11.Afrika kusini,lakini, inaugua na Bafana bafana ,haikuwakilishwa hata katika Kombe lililopita la Afrika,jirani nchini Angola.

Baada ya kumtimua kocha wake wa zamani mbrazil, Santana, ilimrudisha mbrazil mwengine,alieiongoza katika Kombe la Afrika la mataifa 2008 nchini Ghana: Carlos Alberto Parreira, alieiongoza pia Brazil,kutwaa taji la dunia, 1994 nchini Marekani.

Parreira, amesema wiki hii kwamba, anatumai Bafana Bafana itajifunza kucheza dimba kwa staili ya Brazil kufuatia mazowezi ya mwezi mzima. Parreira anaongoza kikosi cha wachezaji 29 wa Bafana Bafana katika kambi ya mazowezi ya timu ya Teresopolis huko Brazil.Ameahidi , Afrika kusini itacheza mechi kadhaa za kirafiki ili kujiandaa kwa Kombe la dunia.

Bafana bafana, ikijinoa kucheza staili ya Brazil chini ya kocha wa ki-brazil isisahau tu kwamba, Brazil, hasa itakuwa uwanjani-Brazil ya akina kaka,Grafeti na Robinho.

Mbali na maandalio ya dimba, Afrika Kusini , imejitembeza wiki hii huko Berlin katika maonesho ya utalii ya ITB vivutio vyake mfano wa Mbuga Taifa ya Kruger Park,mahoteli yake katika bahari ya hindi na kadhalika. Bw.Sithole mjumbe wa Afrika kusini katika ITB Berlin, alimwambia mwandishi wetu Thelma Mwadzaya:

"Tumefanya maandalio mengi.Kwanza ,Uwanja wetu ambao Ujerumani itacheza mojawapo ya mechi zake, umeshakamilika na unachukua mashabiki 70.000.Pia ,ni kivutio cha utalii. Pili, katika mawasiliano na usafiri, tumetengeza njia na barabara zote zinazoelekea uwanja wa ndege.Kwahivyo, hakutakua na matatizo kwa mashabiki wanaoelekea uwanja wa mpira.

Na tatu, tutakuwa na uwanja mpya wa Ndege wa Kimataifa mjini Durban. utakaofunguliwa rasmi Mei mosi,mwaka huu.Swali jengine, ni mapokezi:Kuna nafasi za kutosha mahotelini kwa mashabiki wataokuja kwa Kombe la dunia."Alisema Bw.Sithole huko Berlin.

Shirikisho la dimba la Afrika (CAF) kati ya wiki hii ,lilimchagua nahodha wa Ivory Coast na stadi wa Chelsea,Didier Drogba "mchezaji wake bora wa dimba wa mwaka barani Afrika:Lakini nani huyu Didier Drogba na alianza vipi maisha yake ya dimba hadi kuwa nahodha wa Corte d'Iviore,kutamba na Olympique Marseille huko Ufaransa kabla kujiunga na Chelsea klabu yake sasa ya Uingereza?

Akiwa amezaliwa Machi 11,1978 mjini Abidjan, jiji kuu la ivory Coast, Didier Drogba, alianza maisha yake ya dimba na klabu ya daraja ya pili ya Ufaransa, Le Mans. Hakukawia kugonga vichwa vya habari katika msimu wa 2002-2003 alipopachika mabao 17 katika mechi 34 akiichezea klabu ya daraja ya kwanza ya Guingmp.Mwaka huo, macho ya klabu maarufu ya ufaransa, Olympique Marseille,klabu ya muafrika mwengine Abedi Pele,yakamkodolea Drogba na akatia mabao 18 alipoisaidia timu hiyo kuingia finali ya kombe la ulaya la UEFA.

Mwaka uliofuatia , 2004 , salamu alizotoa Drogba huko Ufaransa, zikafika Premier League-Ligi ya Uingereza.Chelsea, ikamfungisha mkataba Drogba kwa kitita cha dala milioni 35.Hakukawia pamoja na Chelsea kutwaa ubingwa wa Uingereza Premier League na kombe la League cup tena msimu wake wa kwanza tu huko Uingereza.Ni Drogba alielifumania lango la Liverpool katika finali ya Kombe la Ligi alipotia bao la ushindi baada ya kurefushwa mchezo na Chelsea kutamba kwa mabao 3:2, Drogba alikwsha kuwa maarufu hata Uingereza.

Msimu uliofuata ,Drogba akavaa taji jengine na Chelsea pale klabu hiyo ilipokuwa timu ya pili tu kuvaa taji la premier League kwa mwaka wapili mfululizo.

Kimataifa, Drogba alivaa jazi ya Ivory Coast, kwa mara ya kwanza Septemba 8,2002 pale Tembo walipocheza na Bafana bafana (Afrika Kusini).Drogba alitia bao lake la kwanza kwa timu ya taifa pale Tembo walipo wakanyaga simba wa nyika -Kameroun, hapo Februari 11, mwaka 2003 na kuondoka na ushindi wa mabao 3-0.

Halafu Drogba akapewa unahodha wa kuiongoza Ivory Coast katika Kombe la Afrika la Mataifa hapo 2006,lakini jahazi lake lilienda mrama katika finali na mafiraouni Misri, mjini Cairo.Baada ya kuachana sare 0:0 mikwaju ya penalty ilibidi kuamua hatima ya Kombe la Afrika: nahodha Drogba, akalizamisha jahazi lake pale mkwaju wake wa adhabu ulipokosea shabaha aliolenga.Furaha ilioje kwa mafiraouni na sultani wao wa dimba Hassan Shehata.

Taji alilovishwa Didier Drogba , wiki hii la "mchezaji bora wa dimba wa Afrika" si geni kwa Drogba, kwani, alikwishalivaa 2006,alipompita chupu-chupu tu, stadi mwengine wa Afrika,mkameroun Samuel Eto-o kwa kura 79:74. Ni mwaka ambao, Drogba aliisaidia Ivory Coast,kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza kombe la dunia hapa Ujerumani, ikiangukia kama mwaka huu kundi la kufa-kupona.

Ingawa Ivory Coast, ilitimuliwa nje isicheze robo-finali ya kombe la Afrika la Mataifa, huko Angola, Drogba ataiongoza Juni hii,Ivory Coast ,kutamba tena katika Kombe la dunia.Akiteremka uwanjani, Drogba anajua , anabeba kama nahodha sio tu matumaini ya Ivory Coast -bali ya Afrika nzima. Bila ya shaka , hatujasikia salamu za mwosho za jogoo hili la Chelsea na la Afrika !

Mwandishi: Ramadhan Ali/ DPAE/RTRE

Imepitiwa na Hamidou Oummilkheir