Michezo mwishoni mwa wiki | Michezo | DW | 25.04.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo mwishoni mwa wiki

Kombe la klabu bingwa barani Afrika uwanjani na Bundesliga yazikutanisha mabingwa Stuttgart na viongozi wa Ligi B.Munich.

B.Munich ilipocheza na St.Petersburg

B.Munich ilipocheza na St.Petersburg

Duru nyengine ya kombe la klabu bingwa barani Afrika na kombe la shirikisho-CAF inarudi viwanjani mwishoni mwa wiki hii huku macho yakikodolewa mpambano kati ya mabingwa Al Ahly ya Misri na chipukizi Platinum stars ya Afrika kusini mjini Johannesberg.

Bundesliga pia inarudi uwanjani kwa mpambano wa kukata na shoka kesho jumapili kati ya mabingwa Stuttgart na viongozi wa Ligi-Bayern Munich.

Wanariadha wa Afrika lakini wanajiwinda kuwasili Addis Ababa wiki hii ijayo kujinoa kwa michezo ijayo ya Olimpik mjini Beijing:

►◄

Tukianza na kombe la klabu bingwa ,mabingwa wa Afrika Al Ahly ya Misri -klabu ilioasisiwa zaidi ya miaka 100 iliopita ina miadi na Platinum stars-timu iliopanda daraja ya kwanza ya ligi ya afrika kusini miaka 5 tu iliopita.

Kocha wa Platinum stars-muargentina Miguel Gamondi amejitapa hatahivyo, kwamba Al Ahly ndio timu ya mwisho kati ya zote 16 waliotamani kukutana nayo. Ajali kwahivyo imeshawaangukia na wanasubiri hatima yao.

Klabu nyengine ya Misri-Zamalek na mabingwa wa Afrika mara 5 inakumbana na timu ya polisi ya Angola-Inter club mjini Cairo.Na pia huo hautakua mteremko kwa waangola.

Mabingwa watetezi wa kombe hili la klabu bingwa Etoile du Sahel ya Tunisia, wanawatembelea Dynamo ya Zimbabwe katika changamoto nyengine ya kaskazini na kusini mwa Afrika.Kuna mabingwa wengine 5 wa kombe hili uwanjani wanaoania zawadi ya kitita cha dala milioni 1 kwa mshindi:

Mabingwa 2 wanakutana-Enyimba ya nigeria ina miadi na Club Africain ya tunisia huko Aba, mashariki mwa Nigeria.

TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,timu ya kwanza kabisa kuvaa taji mara mbili mfululizo wanakutana na Al-Ittihad ya Libya mjini Tripoli.

Al Hilal ya Sudan wanawakaribisha mamelodi Sundowns kutoka Afrika kusini.

Ama upande wa kombe la Shirikisho-CAF- Ajax Cape Town ya afrika kusini inapambana nyumbani na Mount Cameroon wakati Dolphin ya Nigeria inaumana na Asante kotoko ya ghana.Mjini Bulawayo,Zimbabwe -Highlanders wanachuana na Al Merreikh ya Sudan.

Katika changamoto za Ligi za ulaya mwishoni mwa wiki hii,macho ya mashabiki wa ujerumani yatakodolewa kesho mpambano wa kukata na shoka baina ya mabingwa Stuttgart na viongozi wa Bundesliga-Bayern Munich.Munich imefungua mwanya wa hadi pointi 10 kutoka Schalke na ingawa ilishimndwa juzi kutamba katika nusu-finali ya kombe la ulaya la UEFA huko Petersburg,Russia, inahitaji pointi zote 3 kesho kumaliza udhia na kutia mfukoni kombe lake la pili msimu huu.Wiki iliopita, Munich ilitoa B.Dortmund kwa mabao 2:1 na kutawazwa mabingwa wa kombe la shirikisho la kabumbu la Ujerumani DFB.Munich imepania kutwaa vikombe 3 msimu huu.

Schalke ionaitembelea Hamburg leo wakati Brem,en iko nyumbani mwa Karlsruhe.Hannover inaahidi kutamba nyumbani inapocheza na Hertha Berlin huku Nuremberg ilioanza kufufuka upya inaikaribisha Armenia Bielefeld.Energie Cottbus pia iko nyumbani na mahasimu wao leo ni Hansa Rostock.Bochum inakamilisha kalenda ya leo ya Bundesliga kwa changamoto na Duisburg,inayoonesha itarudi daraja ya pili msimu ujao.

Ama katika zahama za Premier League,leo asie na mwana aeke jiwe na asie na mguu atie gongo-Manchester united iliomudu sare tu ya 0:0 na Barcelona juzi katika champions League inaonana na Chelsea iliotoka pia suluhu na Liverpool ya bao 1:1 katika kombe hilo.Huu huenda ukawa finali ya kwanza ya kombe la klabu bingwa mwezi ujao mjini Moscow.

Liverpool inaitembelea Birmingham city huku Manchester City wakijinoa kwa mkutano wao na Fulham.Wigan athletic wanacheza na Reading wakati sunderland wana miadi na Middlesbrough.Changamoto za leo za premier league zinakamilishwa kwa changamoto kati ya Tottenham Hotspur na Bolton wanderes.

RIADHA:

Zaidi ya wanariadha 2,000 kutoka nchi 43 za afrika watashindana mjini Addis Ababa,Ethiopia kuanzia April 30 hadi Mei 4 kujinoa kwa michezo ya olimpik ya beijing hapo August.

Wenyeji Ethiopia hawakukawia kuwapelekea mahasimu wao salamu kwamba,jogoo la mjini limekusudia kuwika.

salamu hizo pengine ni kwa wakenya,lakini pia kwa waafrika ya kaskazini-Morocco na Algeria.

Bingwa wa mabingwa Kenenisa bekele atatamba katika mita 10.000 wakati Tariku Bekele ataongoza mbio za mita 5,000 upande wa wanaume.

Katika safu ya wanawake: Bingwa wa dunia Turnish Dibaba ataongoza mkuki wa Etghiopia katika mita 10.000 huku mita 5000,atazamiwa kutamba bingwa mwengine Meseret Defar.

Mashindano ya riadha ya ubingwa wa afrika huandaliwa kila baada ya miaka 2.