Michezo Mwishoni mwa Juma | Michezo | DW | 23.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michezo Mwishoni mwa Juma

Bayer Leverkusen yachukua uongozi wa Bundesliga

Ligi kuu ya Ujerumani:

Kilichotawala zaidi mwishoni mwa juma ni michuano na taarifa za kandanda.Katika ligi kuu ya kandanda hapa Ujerumani Bundesliga, ambapo Bayern Munich bado ina kibarua kigumu baada ya kushindwa tena kuondoka na ushindi ilipolazimishwa sare ya bao moa kwa moja na Bayer Leverkusen kwao mini Munich na Leverkusen kusogea hadi kileleni.

Bundesliga Bayer Leverkusen gg FC Bayern

Stefan Kiessling wa Bayer Leverkusen ( kushoto)akisherehekea ya kuuona wavu wa Bayern Munich.

Matokeo hayo yanaendelea kumkatisha tamaa wa Bayern Munich Mholanzi Louis van Gaal. Van Gaal alisema baada ya mchezo huo na alisema " Hatukucheza vizuri kipindi cha kwanza, tuliona Bayern lishindwa kuonana vizuri,lakini kipindi cha pili tuliwapa shinikizo wapinzani wetu na hata kufunga bao. Hali hii nimekua nikiizungumzia kila mara tangu wiki kadhaa sasa."

Bayern Munich sasa iko nafasi ya 7 ikiwa na pointi 21 wakati Leverkusen imechukua tena uongozi ikiwa na pointi 27, poini moja kuliko Werder Bremen iliyoimwagia Freiburg mvua ya magoli sita kwa bila. Nafasi ya tatu ni Schalke ikifuatiwa na Hoffenheim ambayo iliifunza dimba FC Cologne na kuiaga nyumbani kwao na mabao 4-0.

Kama kweli mcheza kwao hutunzwa ,basi pia haikua hivyo kwa Hamburg iloteremka nafasi moja nyuma ya Hoffenheim ikiwa sasa nafasi ya sita.Hamburg ilitandikwa na Bochum 1-0 .Bochum ,Stuttgart na Hertha Berlin ndizo zinazoninginia katika hatari ya kushuka daraja, huku Hertha iliotoka sare na Stuttgart bao moja kwa moja Jumamosi ikiwa ndiyo yenye kukamata mkia.

Ligi za England na Uhispania:

Katika ligi nyengine za Ulaya , Chelsea imejiimariha zaii katika uongoi wa ligi kuu a England Primier League kwa kuibwaga Wolveshampton mabao 4-0 na sasa ina pointi 33. Manchester United ikiwa nyuma ya Chelsea kwa tafauti ya pointi 5 nayo iliilaza Everton mabao 3-0 wakati nafasi ya tatu ni Arsenal ya mjni London.Hata hivyo Arsenal ilishindwa kufua dafu iliporudi nyumbani kutoka Sunderland ikiwa imetandikwa bao moja kwa bila.

Real Madrid imechukua uongozi wa ligi kuu ya Uhispania "La Liga," ilipofanikiwa kuitandika Santander bao 1-0, wakati Barcelona ililazimishwa sare ya goli 1-1 na Athletico Bilbao .
Real na Barca zinatafautiana kwa pointi moja na mchuano wa kusisimua kati ya miamba hiyo miwili unasubiriwa jumamosi ambapo watakutana kwa mara ya kwanza kaika mchuano wa ligi msimu huu.

Fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka ujao:
Barani Afrika ratiba ya michuano ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika ,mashindano yatakayofanyika nchini Angola kuanzia Januari 10 hadi 31 mwaka ujao sasa imeshafahamika. Ghana na Ivory coast zilizofanikiwa kucheza fainali za kombe la dunia nchini Afrika kusini mwaka uajo zizatoana jasho katika duru ya kwanza ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika. Mabingwa watetezi Misri wakiwa na kiu cha kulinyakua taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo wako kundi la tatu -kundi C pamoja na Nigeria,Msumbiji na Benin. Mchuano wa Ghana na Ivory Coast utawakutanisha wachezaji wawili nyota wa timu ya ligi kuu ya Uingereza Chelsea, Mshambuliaji Didier Drogba wa Ivoy Coast na mchezaji wa kiungo mwenye kutumainiwa Michael Essien wa Ghana.Mchezaji mwengine wa ligi kuu ya Uingereza katika kundi hilo linaloitwa la kifo ni Emmanuel Adebayor kutoka manchester City ambaye atakua na timu ya taifa ya Togo .Nyengine katika kundi hilo ni Burkina Faso.Itakumbukwa mshambuliaji wa Burkina faso moumouni Dagano anayecheza soka la kulipwa huko Qatar alikua mfungaji bora wakati wa michuano ya kutafuta tiketi ya fainali za kombe la dunia na la mataifa ya Afrika 2010 akiwa ameuona wavu mara 12.Dagano alifunga mabao matatu wakati wa mchuano na Seychelles.

Angola mwenyeji wa mashindano hayo ya 52 ya kombe la mataifa ya Afrika iko kundi la kwanza pamoja na Mali,Malawi na Algeria na ina matumaini ya kumaliza nafasi mbili za kwanza katika kundi hili kuweza kucheza robo fainali.Kocha wa Angola Manuel jose ana matumaini kupangwa na Algeria ilioibwaga Misri wiki iliopita kunyakua tiketi ya fainali za kombe la dunia huenda ndiyo itakayoipa kazi ngumu timu yake. Mpinzani mwengine Mali huenda pia ikawa si timu ya mteremko. Wachezaji wake Frederick Kanoute ,Mahamdou Diarra a Seydou Keita ni wakutumainiwa katika ligi kuu ya Uhispania,La Liga ambapo Malawi chini ya Kocha Mnigeria Stephen Keshi wanazingatiwa kuwa wasindikizaji.

Cameroun mabingwa wa mara nne wa mashindano hayo ya shirikisho la soka barani Afrika,itakua timu ngumu kukabiliana nayo katika kundi la tatu-kundi C, ambamo pia zimo Tunisia, Gabon na Zambia.Lakini wachambuzi wa soka wanasema katika mpira mambo huweza kugeuka.

Mashindano hayo ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika zinatarajiwa kuwa kivutio cha kimataifa kwani zitafanyika miezi mitano kabla ya kombe la dunia nchini Afrika kusini,la kwanza kuchezwa barani Afrika.


Shirikisho la vyama vya soka barani ulaya UEFA limesema litataka itolewe adhabu kali kwa wachezaji au kilabu zilizohusika katika kashfa kubwa kabisa iliogunduliwa hivi karibuni ya upangaj wa matokeo ya michezo kadhaa ya kandanda. UEFA imesema inashirikiana na polisi ya Ujerumani na waendesha mashitaka anaoshughulikia uchunguzi kuhusiana na mechi 200 katika ligi tisa za Ulaya.

Kashfa ya upangaji matokeo:
Shirikisho hilo la vyama vya kandanda barani Ulaya limesema ligi tatu za vilabu bingwa na michuano ya ligi 12 za Ulaya inayochunguzwa-yote ilikua michezo za duru za awali.
Michuano hiyo ni sehemu ya mechi 40 ambazo zimetajwa awali kuwa zimo kwenye orodha ya kuchunguzwa. Taarifa kuhusia na michuano kadhaa zimekabidhiwa maafisa wa Ujerumani kutokana na ombi lao. taarifa ya UEFA,Shirikisho la vyama vya soka barani ulaya imesema litaendelea kupambana na kila aina ya rushwa katika soka la Ulaya bila ya kumvumilia yeyote. Taarifa hiyo ikapendekeza adhabu kali za mahakama kwa mtu yeyote, kilabu au afisa atakayehusishwa na vitendo vya udanganyifu na upangaji wa matokeo ya michezo iwe katika misingi ya sheria za serikali au za vyombo vya michezo.

Kisa cha mfaransa Henry :

Wito wa chama cha soka na maafisa wa serikali katika Jamhuri ya Ireland kutaka mpambano kati ya Ufaransa na Ireland kuwania nafasi ya kucheza afainali za kombe la dunia mwaka ujao nchini Afrika kusini, urudiwe unaendelea licha ya kugonga mwamba mbele ya maafisa wa soka wa Ufaransa na Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA.

Vyombo hivyo viwili vimekataa kurudiwa kwa mchezo huo. Chama cha soka nchini Ufaransa na FIFA zimelipinga takwa hilo huku FIFA ikisema taratibu za shirikisho hilo ni kuwa uamuzi wa muamuzi uwanjani ndiyo wa mwisho. Katika mchuano huo Jumatano iliopita, Ufaransa ilisawazisha bao kuyageuza matokeo kuwa bao moja kwa moja na kuinyima Ireland nafasi ya kwenda Afrika kusini kutokana na ushindi wa Ufaransa wa bao 1-0 katika mchuano wa durui ya kwanza. Hata hivyo kabla ya bao hilo, mshambuliaji wa Ufaransa Thierry Henry aliunawa mpira .

Henry binafsi amekiri kufanya hivyo na kusema uamuzi muwafaka na heshima ungekuwa mechi hiyo kurudiwa tena. Tukio hilo limeigawa jamii ya Ufaransa kuanzia wanasiasa hadi raia. baadhi ya magazeti pia yameuita ushindi huo kuwa wa aibu na mfano mbaya kwa kizazi kijacho.

Wakati huo huo akizungumza na gazeti la Le Parisien mlini wa zamani wa timu ya taifa ya Ufarnsa ililinyakua kombe la dunia 1998 Bixente Lizarazu aliuita ushindi wa Ufaransa dhidi ya Ireland kuwa " Uusiostahiki na wa udanganyifu." Akiongeza kwamba Ufaransa ilizidiwa mno na Ireland kwa mbinu na ufundi katika mchuano huo.
Pamoja na hay nahodha wa timu ya Ireland ameyaeleza matamshi ya Thierry Henry kukiri kwamba aliunawa wazi mpir na kuwa mechi hiyo ingerudiwa, kuwa ni ya heshima na ujasiri mubwa." na kumpongeza mchezaji huo. pia mashabiki kadhaa wa soka nchini Ufaransa wamejiorodhesha kwenye mtandao wa serikali kuelezea kutofurahishwa kwao na kilichotokea.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman /afp,rtr

Mhariri:Aboubakary Liongo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com