Michezo katika Juma | Michezo | DW | 13.08.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo katika Juma

Wiki hii kilichotawala ni kandanda .

Harakati za usajili miongoni mwa vilabu kadhaa vya ligi kuu za ulaya zinaendelea kwa msimu huu mpya. Wakati ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga ikifungua dimba wiki ijayo, mabingwa wa zamani Wolfsburg wanakaribia kukamilisha usajili wa mchezaji kutoka Brazil Diego kutoka kilabu ya Italia ya Juventus. Gazeti la Bild liliripoti kwamba Wolfsburg mabingwa wa 2009, imekubali kumsajili Diego kwa ya euro milioni 17, ikiwa ni kasoro ya milioni moja kuliko kitita ambacho Juventus ikidai.

Bundesliaga si ligi ngeni kwa Diego ambaye msimu wa 2006 hadi 2009 aliicheza Werder Bremen. Kabla ya kuhamia Juventus.Lakini Mbrazil huyo alishindwa kun´gara katika msimu wake wa kwanza na Juventus.Wolfsburg iliomaliza nafasi ya nane msimu uliopita wa Bundesliga inajaribu kujiimarisha kwa msimu mpya chini ya Kocha mpya Muingereza Steve McClaren, ambaye amefanikiwa kumbakisha mshambuliaji kutoka Bosnia Edin Dzeko, ambaye akiandamwa na vilabu kadhaa vya Ulaya, baada ya kumaliza ligi msimu uliopita akiwa mfungaji bora.

Wakati mashabiki wa soka hapa nchini wakisubiri kwa hamu kuanza Bundesliga tarehe 20 mwezi hu wa Agsosti, tayari makocha kadhaa wameungama kuwa Bayern Munich watautwaa tena ubingwa wanaoushikilia. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la habari la Ujerumani DPA, makocha 15 kati ya wapinzani 17 wa Bayern katika ligi hiyo kuu wameagulia kuwa ubingwa tena utakua wa kilabu hiyo ya kusini mwa Ujerumani.

Deutschland Fußball Supercup Bayern Schalke

Kikosi cha Bayern Munich.

Ni Kocha Thomas Schaarf wa Werder Bremen na Marco Kurz wa kilabu iliopanda daraja msimu huu Kaiserslautern ambao hawatarajii matokeo kuwa hivyo. Schaaf hakuitaja timu nyengine wakati Kurz amesema taji la ubingwa litanyakuliwa ama na Bremen au Schalke 04. Kocha wa Bayern Munich Louis van gaal pamoja na kupigiwa debe kuwa atautwaa tena ubingwa, binafsi hakuitaja timu yoyote. Hata hivyo alisema anaamini timu yake iatapiga hatua zaidi mbele baada ya msimu uliopita kuutwaa ubingwa wa ligi kuu, na kombe la Shirikisho la kandanda la Ujerumani pamoja na kufika fainali ya ubingwa wa ulaya Champions league. Kocha wa zamani wa Bayern ambaye sasa yuko na kilabu ya Schalke Felix Magath amebashiri kuwa bayern itautwaa tena ubingwa kwa sababu inakikosi bora zaidi cha wachezaji.

Kocha mwengine wa zamani wa Bayern Munich Jupp Heynckes anayeifunza Bayer Leverkusen amesema pamoja na kwamba Bayern siku zote wanapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa ubingwa, lakini msimu huu Schalke ina usajili bora zaidi.

Nje ya Ujerumani,mchezaji wa kiungo wa timu ya taifa ya Denmark Christian Poulsen amejiunga na kocha wake wa zamani Roy Hodgson wiki hii,baada ya kukubali kusajili na kilabu ya Uingereza ya Liverpool kwa mkataba wa miaka mitatu. Mtandao wa miamba hiyo ya Primier League , ligi kuu ya England, uliripoti kwamba Poulsen mwenye umri wa miaka 30 amejiunga na Liverpool kutoka Juventus ya Italia ambako alicheza misimu miwili isiyo ya mafanikio kwake,baada ya kujiunga na kilabu hiyo ya mjini Turin kutoka Sevilla ya Uhispania.

Umesema Liverpool ilikubali kuwa ada ya euro milioni 5 na laki nne inaweza kulipwa, ikitegemea uchezaji wake. Poulsen ambaye ameichezea timu ya taifa ya Denmark mara 77 anauchezaji unaofanana na ule wa Mu-argentina Javier Marscherano na hivyo uwezekano wa Marcherano kuiihama kilabu hiyo sasa kuwa mkubwa zaidi.Mchezaji huyo ameungama ana nia ya kuhamia kilabu nyengine na sio kwamba anadukuduku na Liverpool bali anataka kupata uzoefu mpya mahala kwengine. Tayari inasemekana kilabu ya Barcelona ya Uhispania ina muwinda.

Fußball Manchester United Sir Alex Ferguson

Kocha wa Manchester United Alex Ferguson

Kwa upande wa kocha Hodgson, ambaye pia amemsajili mchezaji wa kuiungo Joe Cole kutoka Chelsea na Milano Jovanovic kutoka Standard de Liege ya Ubeligiji anayecheza kona ya kulia tangu alipochukua mamlaka ya kuifunza Liverpool, aliwahi kuwa na Poulsen wakati Hodgson alipokuwa mwalimu wa FC Copenahagen ya Denmark.

Kwa upande mwengine wakati usajili miongoni mwa timu za Ulaya ukiendelea tayari kwa msimu mpya wa ligi, kilabu nyengine ya England Manchester United,Ilikamilisha wiki hii taratibu za kumsajili mshambuliaji Bebe kutoka kilabu ya Guimaraes ya Ureno. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alitazamiwa kukamilisha taratibu za ukaguzi wa afya tayari kujiunga na MANU ambayo imekamilisha usajili wake wa tatu kwa msimu huu. Kocha Alex Ferguson amekua akiwania kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, na hivyo Bebe atajiunga na Mmexico Javier Hernandez aliyefunga bao la kufuta machozi pale United ilipolazwa mabao 3-1 na Chelsea katika pambano la kuwania ngao ya jamii kwenye uwanja wa Wembley Jumapili iliopita.

Nchini Ufaransa ulizuka mvutano hapo jana kati ya mabingwa wa soko nchibni humo kilabu ya Olympique Marseilles na mchezaji wake wa kiungo Hatem Ben Arfa. Ben Arfa anataka kuihama kilabu hiyo, lakini Marseilles inashikilia kwamba anabakia. Mchezaji huyio anataka kuhamia New castle ya Uingereza, huku akiwaambia maafisa wa Marseilles kuwa alifikia uamuzi huo kabla ya kutoka mazoezini Alhamisi.

Mwenyekiti wa Marseilles Jean Claude Dassier alitoa taarifa fupi hata hivyo akisena Ben Arfa hendi kokote. Kocha Didier Deschamps ambaye kwa upande mwengine ameonyesha kuchukizwa kwake na takwa la mchezaji mwengine mshambuliaji Mamadou Niang kutoka Senegal, kuhamia kilabu nyengine, alikata kutamka lolote.

Marseilles alianza kampeni ya kuutetea ubingwa wake, kwa mshtuko baada ya kufungwa na Caen mwishoni mwa Juma lililopita mabao 2-1 .

Tukibakia na kandanda, Italia imeelezea kuridhishwa kwake baada ya mazungumzo na ujumbe wa Shirikisho la vyama vya kandanda barani ulaya UEFA, juu ya ombi la nchi hiyo kugombea mashindano ya kandanda ya kombe la Ulaya 2016. Gianni Letta Katibu mkuu wa ofisi ya Waziri mkuu Silvio Berlusconi alilipongeza taifa hilo kwa kuungana, akiongeza amaamini ukarimu,historia yake ya kuhifadhi mambo ya kale, mandhari ya nchi hiyo na hali ya hewa ni miongoni mwa sifa zitakazoweza kuipa nafasi Italia kuandaa mashindano hayo. Italia ilikua mwenyeji wa mashindano makubwa ya kandanda 1990, ilipoandaa kombe la dunia.

Na sasa barani Afrika, ambako kwanza huko Tanzania pambano la kukata na shoka lilikuwa likisubiriwa leo baina ya kilabu mbili maarufu nchini humo Young Africans - Yanga au vijana wa Jangwani na Simba vijana wa Msimbazi zote za Dar es salaam, umeahirishwa . Kwa mujibu wa afisa wa habari wa Shirikisho la Kandanda Tanzani Florian Kaijage, pambano hilo sasa litachezwa Jumatano ,Agosti 18.

Huko Ghana, kocha Mserbia Milovan Rajevac anatarajiwa kurefusha mkataba wake na timu ya taifa ya nchi hiyo.Rajevac mwenye umri wa miaka 56 aliwaambia waandishi habari Alhamisi mjini Johannesburg baada ya Ghana kufungwa na Afrika kusini bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki. Mkataba wake wa awali wa miaka miwili utamalizika mwezi ujao na sasa anasema ameshajadiliana na chama cha kandanda cha Ghana iliomaliza kombe la dunia katika robo fainali, kuendelea kuwa kocha wa Black Stars.

Tunisia imerejesha tena matumaini kuelekea fainali zijazo za kombe la mataifa ya Afrika 2012. Katika mechi ya kutafuta nafasi ya kushiriki katika fainali, iliochezwa mjini Tunis Jumatano, Tunisia iliibwaga Chad 3-1.

Katika mechi ya kwanza Tunisia ilipata pigo ilipofungwa, tena katika uwanja wa nyumbani na Botswana. Fainali zinazo za kombe la mataiafa ya Afrika 2012 zitaandaliwa kwa ubia - Guinea ya Ikweta ikishirikiana na Gabon.

Na ikijitayarisha kwa michezo ya kuania kufuzu kwa fainali hizo za kombe la mataifa ya Afrika timu ya taifa ya Tanzania ,Taifa Stars iliumana na timu ya taifa ya Kenya Harambe Stars katikati ya Juma hili mchezo uliomalizika sare ya bao moja kwa moja. Pambano hilo lilifanyika mjini Dar-es-Salaam. 

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/afp,rtr

Mpitiaji:Josephat Charo