Michezo: Champions League. | Michezo | DW | 23.11.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michezo: Champions League.

Werder Bremen yaweka matumaini ya kusonga mbele.

Thomas Frings wa Werder Bremen akiunganisha mpira wa kichwa katika pambano na Chelsea, Bremen ilishinda bao 1-0.

Thomas Frings wa Werder Bremen akiunganisha mpira wa kichwa katika pambano na Chelsea, Bremen ilishinda bao 1-0.

Na hatimae Michezo.Baada ya michuano ya kusisimua jana usiku ya kombe la ligi ya vilabu bingwa vya Ulaya-Champions League- leo ni zamu ya ile ya kombe la Shirikisho la vyama vya kandanda barani Ulaya-UEFA.

Tukianza kwa mukhtasari na mtazamo wa michuano ya jana Werder Bremen ya Ujerumani ilidhihirisha ule usemi wa “Mcheza kwao hutunzwa”, ilipowaangusha wenyeji wao na miamba ya soka ya Uingereza Chelsea katika pambano la ligi ya vilabu bingwa vya ulaya-Champions League hapo jana 1-0 mjini Bremen. Hata hivyo pamoja na kipigo hicho Charles inasonga mbele.

Kutokana na matokeo hayo, sasa matokeo ya sare tu katika mchezo wake ujao Desemba 5 dhidi ya Barcelona ya Uhispania yatatosha kuipa nafasi Bremen ya kuingia katika duru ya timu 16 za mwisho na itakua ni kwa msimu wa tatu mfululizo.

Kocha wa Bremen Thomas Schaaf alisema anafahamu fika kwamba watahitaji kujiapatia pointi katika pambano lake lijalo na mabingwa hao wa Uhispania. Ama kwa upande wake Frank Raykaard, kocha wa Barcelona- amejigamba kwamba wataiangusha Bremen mchezo ujao na kusonga mbele.

Lakini usemi wa mcheza kwao hutunzwa haukufanya kazi kwa Levski Sofia ya Bulgaria ilipojikuta ikiaibika nyumbani mjini Sofia mbele ya mabingwa wa Uhispania Barcelona mabao 2-0 , lakini itakua na kibarua kigumu katika pambano lake lijalo dhidi ya Bremen , ikihitaji ushindi wa lazima kuweza kusonga mbele.

Chelsea na Bremen zina pointi sawa katika kundi hilo-10 kila moja , huku mabingwa hao wa Uingereza wakiwa na magoli zaidi ya kufunga ,wakati Barcelona ina pointi 8 katika nafasi ya tatu.

Wakati huo huo mashindano ya kombe la Shirikisho la vyama vya kandanda ulaya -UEFA yanatimua vumbi jioni hii ambapo timu zitakazofanikiwa zitaingia katika hatua ya mtoano. Bayer Leverkusen ya Ujerumani inamenyana na Tottenham Hotspur ya Uingereza tayari jana polisi walilazimika kuzuwia fujo za wahuni wa soka zilizozuka mjini Cologne, pale mashabiki wa kandanda wa Kiingereza wapatao 80 walipoanza kuvunja kilichokuwemo katika mkahawa mmoja na kusababisha hasara ya euro 5,000. Kwa kawaida mashabiki wa soka huzunguka kwenye mikahawa ya eneo la mji wa kale wa Cologne kabla ya kuelekea Leverkusen kwa mpambano huo baadae jioni hii.

Timu nyengine katika kundi hilo ni Dinamo Bucharest ya Rumania na Bruges ya Ubeligiji. Tottenham ndiyo inayoongoza kwa pointi 6 ikifuatiwa na Bucharest yenye pointi 3 wakati Leverkusen ikiwa nafasi ya tatu na pointi moja tu na Bruges haina pointi. Timu nyengine ya Ujerumani ilioko katika mashindano hayo ni Eintracht Frankfurt katika kundi linalozijumuisha New castle United ya Uingereza.Palermo ya Italia na Celta Vigo ya Uhispania.

Uingereza ina jumla ya timu nne, na mbali ya Tottenham na New castle itakayochuana na Celta Vigo, nyengine ni Blackburn Rovers ambayo itakua ikitoana jasho na Feyenoord ya Uholanzi huku Rangers ya Scotland ikicheza na Auxerre ya Ufaransa. Mechi nyengine ni Fernabahce ya Uturuki dhidi ya Palermo ya Italia, Sevilla ya Uhispania inamenyana na Baraga ya Ureno na Sparta Prague ya Jamhuri ya Cheki inaikaribisha Ajax Amsterdam ya Uholanzi.

 • Tarehe 23.11.2006
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHcu
 • Tarehe 23.11.2006
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHcu
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com