Michafuko ya Wa-Uigur katika Mkoa wa Xinjiang, China | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Michafuko ya Wa-Uigur katika Mkoa wa Xinjiang, China

Wa-Uigur wa China wanataka haki zao

Rais Hu Jintao wa China

Rais Hu Jintao wa China

Mkutano wa kilele wa nchi nane zenye utajiri mkubwa hapa duniani unfanyika bila ya kuweko mkuu wa nchi na wa chama kutoka China, Hu Jintao. Kutokana na michafuko na ghasia zilizotokea katika mkoa wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa Uchina, Bwana Hu Jintao amerejea mapema nyumbani, Peking. Huu ni uamuzi uliozusha mshangao, kwa mujibu wa maoni ya Matthias von Heine wa hapa Deutsche Welle.


Bila ya shaka, mambo ni magumu huko Xinjiang. Zaidi ya watu 150 wamekufa kutokana na vitendo vya utumiaji nguvu na vya kulipizana visasi baina ya Wa-Uigur na Wachina wa kabila la Han. Tena kuna huu mshangao wa Rais Hu Jintao kuondoka kutoka Italy, licha ya kwamba waziri mkuu wake, Wen Jiabao, yuko mjini Peking, na licha pia ya kwamba majeshi ya usalama yanaonekana yameidhibiti hali ya mambo. Kwa nini basi Hu Jintao amemwacha mwanachama wa baraza la dola, Dai Bingguo, aiwakilishe China katika mkutano wa madola makuu ya dunia? Kuna sababu mbili ambazo hazipingani.


Kwanza: Hu Jintao alitazamia kwamba nchi yake itasifiwa katika mkutano wa L'Aquila, Italy, wa nchi nane zinazoongoza kiuchumi duniani, kwa vile China imekuwa ni kama kisiwa cha utulivu katika mzozo wa sasa wa uchumi duniani. Na pia kwa vile China na India zimetoa ishara za kuregeza kamba katika masuala ya kulinda usafi wa hali ya hewa duniani. Michafuko iliotokea huko Urumqi, mji mkuu wa mkoa wa Xinjiang, yamelirejesha suala la watu wa makabila ya walio wachache katika ajenda ya siasa huko Uchina. Na Hu Jintao hapendi kulizungumzia suala hilo.


Katika mazungumzo yake huko Roma mnamo siku za karibuni, Hu Jintao hajalitaja suala la Xinjiang; lakini suala hilo, bila ya shaka, lingegusiwa huko L'Aquila. Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel, alishatangaza kwamba angefanya hivyo. Huenda Hu Jintao alitaka kujiepusha na hali hiyo isiokuwa nzuri.


Sababu ya pili ni kwamba wakuu wa China wanaitathmini hali ilivyo huko Xinjiang kuwa ni ya hatari; kwamba kwa sasa mtu mwenye nguvu kabisa katika siasa inabidi aweko nchini. Kwa vyovyote vile, michafuko hiyo ya huko Urumqi ni ya umwagaji mkubwa kabisa wa damu kwa watu wa makabila ya wachache huko China tangu kupita miaka sasa. Na mkasa huo umetokea muda mfupi kabla ya kuadhimishwa mwaka wa 60 tangu kuasisiwa Jamhuri ya Umma wa Uchina hapo Oktoba Mosi. Katika hadithi za kubuni zenye kutiwa sura ya propaganda huko China, kunatajwa kuishi pamoja kwa utulivu na kwa amani familia ya watu wa makabila makubwa mbali mbali huko China. Kwa ujumla kuna makabila makubwa 56. Na ndio maana hivi sasa michafuko hiyo inadaiwa kwamba inachochewa na kuongozwa kutoka nje ya China. Madai hayo hayalingani na hali halisi, ukiwaona Wachina wa kabila la Han na Wa-Uigur wakikabiliana, kila upande umejizatiti kwa kubeba marungu na nondo. Ni Hu Jintao aliyekuja na msamiati wa jamii yenye kuwafikiana na kuelewana. Na kwa msamaiti huo alitaka yeye aingie katika vitabu vya historia kama mhunzi wa jamii kama hiyo. Lakini katika mabarabara ya Urumqi, msamiati huo umepoteza uaminifu wowote uliokuwa nao.


Itasisimua kuangalia vipi viongozi wa China watajikwamua katika hali hii ngumu. Kwamba Wachina wa kabila la Han wanatajwa katika vyombo vya habari vya serekali kuwa ndio walioonewa, ni jambo ambalo halitasaidia kujenga uelewano baina ya makabila makubwa ya Uchina. Amani na maelewano baina ya makabila itakuja tu ikiwa China itaachana na uwongo uli kuweko maisha, na kwamba Wa-Uigur na watu wa makabila mengine ya wachache, kama vile Watibeti, waonekane wana sababu ya haki wanapolalamika. Ile haki yao ya kuwa na utawala wa ndani iko karatasini tu. Ukweli ni kwamba Wa-Uigur ni watu walio wachache wanaowekwa pembezoni mwa jamii, tena ndani ya ardhi yao. Katika eneo hilo lugha inayotawala ni Kichina. Katika sekta muhimu za uchumi, kama vile katika taasisi za fedha, mawasiliano, viwanda vya mafuta na gesi ya ardhini, huwakuti Wa-Uigur. Mkuu wa chama mwenye nguvu katika mkoa huo ni Mchina, kama vile mkuu wa polisi. Kwa hivyo, Wa-Uigur hawahitaji mtu kutoka nje awachochee. Kwa vyovyote, mbinyo waliowekewa ndani nchini ni mkubwa; wanahitaji haki ya kulalamika.


Mwandishi: von Hein, Matthias/Othman Miraji

Mhariri: Josephat Charo


 • Tarehe 08.07.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ijr8
 • Tarehe 08.07.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ijr8
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com