1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka sita katika gereza la Guantanamo Bay.

Mwakideu, Alex2 Mei 2008

Sami al Haji anafurahia kuwa huru lakini anasema anasikitikia wenzake aliowaacha katika gereza la Guatanamo Bay

https://p.dw.com/p/DsP5
ua unaozungtuka gereza la Guantanamo BayPicha: AP

Mpiga picha wa Aljazeera aliekuwa ameshikiliwa katika gereza la Marekani la Guantanamo Bay kwa miaka sita ameachiliwa.


Sami Al-Haji mzaliwa wa Sudan ambaye anakabiliwa na matatizo ya kiafya baada ya kugomea chakula kwa mda mrefu amewasili katika mji mkuu wa Sudan-Khartoum kwa usafiri wa ndege ya kijeshi ya Marekani.


Marekani haijaongea lolote kuhusu kuachiliwa huru kwa mpiga picha huyo lakini afisa mmoja mkuu katika wizara ya usalama mjini Washington ambaye hakutaka kutajwa amesema al-Haj hakuachiliwa huru ila amekabidhiwa serikali ya Sudan.


Shirika la habari la Al Jazeera limesema mpiga picha huyo alikamatwa na majasusi wa Pakistan alipokuwa anasafiri karibu na mpaka wa Afghanistan disemba mwaka wa 2001. Juhudi zake za kujitambulisha kwa kutumia kibali rasmi cha kufanya kazi na shirika hilo la habari katika maeneo ya Afghanistan hazikumsaidia.


Shirika hilo limeendelea kusema kwamba mfanyikazi wake Haj aliekuwa anatuhumiwa kwa kutengeza video za Osama Bin Laden alikabidhiwa serikali ya Marekani mnamo januari 2002 lakini hakushtakiwa wala kupelekwa mahakamani.


Mkurugenzi mkuu wa Kamati ya maswala ya wanahabari yenye makao yake New York Joel Simon anasema hatua hiyo ya kumkamata mwanahabari na kumweka nguvuni kwa miaka sita bila kutekeleza sheria kikamilifu ni kama kuizika haki na ni tisho kubwa kwa wanahabari wote wanaofanya kazi katika maeneo ya vita.


Al Jazeera inasema Haj alikuwa amegomea chakula tangu mwaka wa 2007 na amekuwa akilishwa kwa lazima kwa kutumia pua zake mara mbili kwa siku huku akiwa amefungwa.


Waziri wa haki nchini Sudan Abdel Basit anasema Marekani imepata wakati wa kutosha wa kutafuta ushahidi dhidi ya mpiga picha huyo kwahivyo Sudan haina budi kumwachilia huru.


Al Jazeera imeonyesha video ya Haj akibebwa na kupekwa siptali na ikaripoti kuachiliwa kwa raia wengine wawili wa Sudan kutoka gereza la Guantanamo.


Alipohojiwa na shirika hilo la habari Haj amesema anafurahia uhuru wake lakini pia anawasikitikia wenzake ambao bado wanashikiliwa katika gereza hilo la kimataifa na akawashutumu wakuu wa gereza hilo kwa kukiuka haki za wafungwa.


Wakili wa Haj Zachary Katznelson anasema hawaamini kama kuna sababu yoyote inayoweza kupelekea kufungwa kwa mpiga picha huyo hata kwa siku moja nchini Sudan.


Mkurugenzi wa shirika la habari la Al Jazeera Wadah Khanfar ambaye alikwenda mjini Khartoum kumpokea mfanyikazi wake Haj ameshutumu jeshi la Marekani kwa kile alichodai ni kumlazimisha mpiga mwanahabari huyo achunguze shughuli za shirika hilo. Amesema Haj ataendelea kufanya kazi na shirika la Al Jazeera.


Mwanahabari wa shirika la BBC Alan Johnson ambaye alitekwa nyara na kushikiliwa kwa miezi kadhaa katika ukanda wa Gaza alimuandikia barua Haj mwaka jana na kumuonyesha jinsi anavyounga mkono kuachiliwa kwake na pia akamshukuru kwa wito aliotoa uliochangia kuachiliwa kwake kutoka sehemu za mafichoni huko Gaza.  


Katika wito wake aliotoa mnamo machi mwaka uliopita Haj alisema licha ya Marekani kumteka nyara na kumshikilia kwa miaka mingi, hiyo haimaanishi kwamba waislamu wanapaswa kuiga hayo.


Kuna mamia ya wafungwa katika gereza la Guantanamo. Wakwanza kuwasili katika gereza hilo walifungwa takriban miaka sita iliyopita baada ya Marekani kuanzisha kile ambacho Rais George W Bush anakiita vita dhidi ya ugaidi kilichofuatia mashambulizi ya September 11 yaliyotekelezwa na mtandao wa Al Qaeda unaoongozwa na Osama Bin Laden.