Miaka mitano ya vita vya Iraq hali bado ni ngumu nchini humo. | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Miaka mitano ya vita vya Iraq hali bado ni ngumu nchini humo.

Mwaka wa sita umeanza tangu kuanzishwa kwa vita vya Iraq na utawala wa rais Goerge Bush wa Marekani na hali nchini humo bado inaendelea kuzorota.

default

Rais Bush atetea uamuzi wake wa kuingia Iraq

Miaka mitano iliyopita wairaqi walikuwa wakitazama picha za kutisha za mji mkuu Baghdad ulivyokuwa ukimiminiwa mabomu kutoka angani na wanajeshi wa Marekani waliokuwa kwenye madege ya kivita.

Katika kipindi hicho rais George W Bush wa Marekani aliwaahidi walimwengu kwamba anasaka njia za kuuondoa utawala wa Dikteta Saddam Hussein ambaye alidaiwa kuwa na silaha za maangamizi makubwa na pia alikuwa na uhusiano na kundi la mtanadao wa kigaidi la Alqaeda.

Si hilo tu rais Bush aliwaahidi wairaq enzi mpya ya amani,maendeleo,uhuru na haki.

Lakini miaka mitano baadae,hakuna silaha za maangamizi zilizopatikana,na madai ya kwamba Saddam alihusiana na Alqaeda hayajathibitishwa huku wairaq wakisubiri kuona hali ya usalama ikirudi nchini mwao.

Rais Jalal Talabani wa Iraq akizungumzia hali ya sasa nchini Iraq aliipongeza hatua ya Marekani ya kuungo'a madarakni utawala wa Saddam Hussein lakini amesema hali hiyo pia imechangia kuleta changamoto kadhaa katika kukabiliana na Ugaidi na ulaji rushwa nchini Iraq.

Talabani amesema njia iliyofunguliwa na Marekani miaka mitano iliyopita baada ya kuangushwa kutoka madarakani Saddam Hussein sasa imegubikwa na ghasia na ugaidi huku rushwa ikibakia kuwa donda ndugu.

Matamshi ya talabani yanaungwa mkono na ulimwengu kwani wanaharakati wanaopinga vita hivyo wamepanga kufanya maandamano katika nchi mbali mbali za dunia.

Urussi imesema uvamizi huo wa Marekani umeligeuza taifa la Iraq kuwa mojawapo ya maeneo hatari kabisa ulimwenguni na kusababisha kuuwawa kwa zaidi ya watu laki tatu.Waziri wa mambo ya nje wa Urussi Mikhail Kamynin amesema matokeo ya vita vilivyoanzishwa na Marekani Iraq ni jambo lililo wazi na kwamba ni opresheni nzito ya kijeshi iliyoanzishwa bila idhini ya Umoja wa mataifa.

Wakati wanasiasa wa chama cha Demokratic nchini Marekani wakizidi kupinga vita hivyo vya Iraq mgombea wa Urais kutoka chama cha Republicana ambaye wengi wanamuona kama mtu atakayeshika nyanyo za Bush,John MacCain anasema wanajeshi wa Marekani wataendelea kubakia Iraq na hatua ya kuwaondoa itatoa nafasi ya ushindi kwa kundi la Alqaeda.

Matamshi yake ni sawa sawa na ya rais Bush ambaye anajitapa kwamba hali ya mambo Iraq sasa ni shwari.Rais alisema.

``Tangu tulipoanza kuongeza wanajeshi kiwango cha ghasia kimepungua mauaji ya raia yameshuka chini mauaji ya kimadhahebu yamepungua na mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Marekani pia yamepungua.''

Kwa upande mwingine mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Iraq Staffan De Mistura amewaonya viongozi wa Iraq kwamba muda unayoyoma wa kumaliza tofauti ambazo zinakwamisha juhudi za kisiasa.Mjumbe huyo amesema Umoja wa mataifa unalenga kuchukua jukumu la kujenga hatma ya Iraq baada ya kupata matatizo kwa miaka hiyo mitano.Pamoja na yote lakini cha msingi kinachotambuliwa na ulimwengu mzima ni kwamba mamilioni ya wairaqi bado wanateseka na wengi sasa wamekuwa omba omba wa ajira katika nchi za magharibi na za kiarabu.

 • Tarehe 20.03.2008
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DRyV
 • Tarehe 20.03.2008
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DRyV
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com