Miaka minne tangu kupinduliwa Saadam Hussein kutoka madarakni nchini Iraq. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Miaka minne tangu kupinduliwa Saadam Hussein kutoka madarakni nchini Iraq.

Leo unatimia mwaka wa nne tangu kupinduliwa kutoka madarakani rais wa zamani wa Iraq, Saadam Hussein. Alinyongwa Disemab 30, mwaka jana kutokana na hatia aliyopatikana ya kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu. Jana serekali ya Iraq ilisema April Tisa kutoka sasa itakuwa ni siku ya kawaida ya kazi, na haitakuwa tena sikukuu. Jee hii ina maana kumalizika utawala wa Saadam Hussein sio sababu kwa Wa-Iraqi kusheherekea?

Saadam Hussein baada ya kukamatwa karibu na mji wa Tikrit alikozaliwa, nchini Iraq.

Saadam Hussein baada ya kukamatwa karibu na mji wa Tikrit alikozaliwa, nchini Iraq.

Japokuwa aliyekuwa waziri wa habari wa Iraq, chini ya Saadam Hussein, alikuwa hataki kukiri kuporomoka utawala huo, lakini vifaru vya jeshi la Wamarekani vilikuwa tayri vimeshaingia ndani ya mji wa Baghdad hapo April 9, mwaka 2003. Wa-Iraqi na Walimwengu walioneshwa mbele ya macho yao kwamba enzi mpya imechipuka, au angalau, kwa uchache, enzi ya Saadam Hussein imemalizika. Pamoja na kikundi kidogo cha waandamanaji wa Ki-Iraqi, jeshi la Kimarekani likitumika karandinga, lililin’goa sanamu kubwa la Saadam Hussein lililokuweko katikati ya mji- kitendo kilichooneshwa moja kwa moja na televisheni duniani kote.

Kama ilivotarajiwa, kilikuwa kibarua kikubwa kulin’goa sanamu hilo. Polepole na kwa kutumia nguvu nyingi ndipo lilipoanguka chini kabisa. Lakini hamna mtu aliyejuwa vipi kitendo hicho kitakavokuwa mfano kwa hali ya baadae ya Iraq. Na zaidi, jaribio la wanajeshi wa Kimarekani kukifunika kichwa cha sanamu hilo na bendera ya Kimarekani ilikuwa ni ishara isiotarajiwa ya nini ambacho kitakuja baadae.

Miaka minne tangu kuangushwa mdikteta huyo wa Iraq, nchi hiyo ilio na mito miwili ya Euphrates na Tigris, iko mbali zaidi kupata ufumbuzi wa matatizo yake kuliko wakati wowote mwengine. Saadam Hussein hayuko tena. Baada ya kutafutwa kwa miezi aligunduliwa mwishoni mwa mwaka 2003, akawasilishwa mahakamani na kunyongwa mwisho wa mwaka 2006. Lakini utulivu na amani havijarejea Iraq. Nchi hiyo inajikuta katika hali ilio karibu sawa na vita vya kienyeji ambapo jamii mbali mbali za kikabila na kidini zinapigana, kwa sehemu zinasaidiwa na magaidi na dola za kutoka kutoka nje. Hatari kwamba Iraq itasambaratika kutokana na uhasama huo uliokuweko ni jinamizi lililitandani vichwani mwa watu, licha ya majaribio yote yaliofanywa kuifanya nchi hiyo iwe mfano wa dimokrasia katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kulikuweko na uchaguzi huru katika Iarq, katiba ikakubaliwa, na kwa hivyo moja wapo ya mashartio ya nchi hiyo kuendelea kwa amani ilitimizwa. Lakini chaguzi na katiba sio kila kitu. Kuna pia ile hali ya kwamba nchi hiyo bado inakaliwa na majeshi ya Kimarekani, licha ya juhudi zote, na hata za wabunge wa chama cha Democratic huko Marekani kupinga jambo hilo. Mwisho wa nchi hiyo kukaliwa na majeshi ya Marekani hakuonekani. Na makisio ya mwishoni yanaonesha kwamba pia hata mrithi wa Rais Bush, inaweza akawa wa kutoka Chama cha Democratic, huenda asiweze kuyaondosha majeshi hayo.

Suali ni kama rais huyo ataweza au atataka? Ikiwa majeshi yataondoshwa bila ya kwanza kuweko utulivu huko Iraq, basi hapo huenda likaripuka janga la kweli. Na pindi majeshi hayo ya Kimarekani yatabakia nchini humo, basi kila wakati kutakuweko sababu ya kuweko michafuko na kukosekana usalama. Kwa wiki kadhaa sasa Marekani imekuwa ikijaribu kuendesha kampeni ya kuleta usalama, hata kuzidisha majeshi yake, ili kuituliza hali ya mambo katika Baghdad. Badala yake idadi ya Wamarekani wanaouliwa inaongezeka, na pia idadi ya mashambulio na kutekwa watu nyara. Jeshi la watu walio tayari kujitolea mhanga yaonesha halizuiliki, kila siku kunatokea mashambulio, kila wiki, kila mwezi.

Wao ndio walio wengi kabisa kati ya wale wanaoathirika kutokana na mapambano haya ya utumiaji nguvu. Yule anayeweza kukimbilia ngambo, hujaribu kujificha kokote pale. Lakini hakuna usalama. Ugaidi na matumizi ya nguvu hayajuwi kanuni zozote. Miaka minne baada ya kupinduliwa Saadam Hussein yaonesha jambo moja ndio la uhakika. Kupinduliwa kwa mdikteta huyo hakujaleta suluhisho, ulikuwa tu ni mwanzo wa kipindi cha kutisha katika historia ya Iraq.

Miraji Othman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com