Miaka 75 ya Umoja wa Mataifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

UN inajivunia nini miaka 75 tangu iasisiwe?

Miaka 75 ya Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa watimiza miaka 75 wakati ukiwepo ukosefu wa wazi wa mshikamano miongoni mwa nchi zenye nguvu duniani

Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu tarehe 21.09.2020 inaadhimisha miaka 75 ya kuasisiwa kwake wakati dunia ikiwa katika janga kubwa la kiafya la virusi vya Corona ambalo limeionesha wazi hali tete iliyopo ya ushirikiano wa kimataifa.

Kumbukumbu hiyo itafungua rasmi mwanzo wa vikao vya kila mwaka vya baraza kuu ya Umoja wa Mataifa ambapo kawaida viongozi na wajumbe kutoka takriban nchi 200 wanakutana pamoja kujadili kuhusu matatizo ya dunia na kutoa mapendekezo ya ufumbuzi.

Hata hivyo mwaka huu hali itakuwa tofauti eneo la Manhattan halitoshuhudia hekaheka ya misafara isiyokuwa na mwisho ya magari ya kifakhari ya washiriki wa mkutano huo mkuu,wala waandishi habari na wakalimani kwenye kumbi za Umoja wa Mataifa.

Badala yake kutokana na Covid-19 bado kuzuia duniani kote shughuli za watu kusafiri, kila nchi kati ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa 193 itaruhusiwa kutuma muwakilishi mmoja na ambaye tu tayari yuko Marekani. Wengine wote wanahitajika kushiriki mkutano huo kupitia njia ya vidio ikiwemo kiasi ya viongozi 160 hadi 170 wa nchi na serikali wanaopanga kuhutubia mkutano huo.

Viongozi wa nchi watakaohutubia

Rais wa Urusi Vladmir Putin anajiandaa kuhutubia mkutano huo kwa njia ya vidio siku ya Jumanne na rais wa China Xi Jinping ambaye  katika kipindi  cha nyuma wamekuwa wakiwaacha wanadiplomasia wao wa ngazi za kuu kuzungumza kwenye mkutano huo kwa niaba yao pamoja na rais Donald Trump.

Na siku ya Jumatano utakuwa uwanja wa rais wa Venezuela Nicolas Maduri ambaye sehemu kubwa ya dunia inamuoana kama kiongozi asiyekuwa halali. Lakini kwa upande mwingine viongozi ambao hawana mpango wa kuzungumza mbele ya hadhara kuu hiyo ya Umoja wa Mataifa ni pamoja na rais wa Syria Bashar al Assad na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumzia juu ya hilo amesema kwamba suala la diplomasia kufanya kazi linahitaji yawepo mawasiliano na ni masikitiko kwamba wameshindwa kupata fursa ya kuwaleta pamoja viongozi wa mataifa yote.

Kadhalika kiongozi huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amebaini kwamba itakuwepo mikutano mingi kwa njia ya mtandao ya pembeni mwa mkutano huo wa baraza kuu ambayo itajadili masuala kadhaa ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi,migogoro ya Libya na Lebanon miongoni mwa mwasuala mengine.

Azimio la maadhimisho

Maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa inasherehekewa kwa kutolewa pia azimio la pamoja lililotawaliwa na nia njema pamoja na mwito wa kupambana na ubinafsi.

Hata hivyo sura hiyo inatofautiana na ukweli wa mambo ulioshuhudiwa tangu uripuke ugonjwa wa Covid-19 mwanzoni mwa mwaka huu ambako imeshuhudiwa mipaka ikifungwa,ushirikiano ukipungua na nchi zikilazimika kila mmoja kuwa na msimamo wake. Bertrand Badie profesa kutoka taasisi ya mafunzo ya siasa ya Paris anasema nchi zenye nguvu zilipoteza fursa ya janga la virusi vya Corona kuimarisha ushirikiano wa kidunia.

Na badala yake ushirikiano ulivunjika vipande vipande kutokana na madai kwamba China na shirika la afya duniani WHO zilichukua hatua za mwendo wa kobe kushughulikia mripuko huo. Na Marekani nayo ikatangaza itasimama kivyake na kujiondowa katika shirika hilo la WHO.

Badie anasema matukio hayo yameonesha ni kwa jinsi gani nchi zenye nguvu zimesababisha kushindwa hata kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kimsinghi liliundwa kuongoza pale inapotokea changamoto kubwa kama hii ya kuitetemesha dunia.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri; Sudi Mnette

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com