1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 70 ya siku ya "D-Day"

6 Juni 2014

Viongozi wa dunia wamekutana kwa kumbukumbu ya miaka 70 tokea uvamizi wa kihistoria wa Ufaransa wa siku inayojulikana kama "D-Day", ambayo iliharakisha kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

https://p.dw.com/p/1CDgb
Viongozi wa Dunia walioshiriki kumbukumbu ya miaka 70 ya "D-Day" huko Normandy Ufaransa. (06.06.2014)
Viongozi wa Dunia walioshiriki kumbukumbu ya miaka 70 ya "D-Day" huko Normandy Ufaransa. (06.06.2014)Picha: picture-alliance/AP Photo

Katika hafla inayofanyika kwenye fukwe za kaskazini mwa Ufaransa ambapo shambulio kubwa kabisa la majini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa katika historia lilianzishwa hapo mwaka 1944,wakuu wa nchi,wafalme na mawaziri wakuu wamekusanyika bega kwa bega na maveterani ambao hivi sasa wako wenye umri wa miaka ya tisini waliojitolea maisha yao kuikomboa Ulaya kutoka himaya ya Manazi wa Ujerumani.

Katika hotuba ya ufunguzi wa hafla ya sherehe hizo Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema tarehe sita mwezi wa Juni kwenye fukwe za Normandy hakuna mtu aliejuwa kwamba siku hiyo itakuwa siku ya kwanza ya mapambano makali ya vita vya kuikomboa Ufaransa kwamba zaidi ya wanajeshi 120,00 waliuwawa wakiwemo raia 20,000.

Wageni wa heshima akiwemo Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza ambaye akiwa na umri wa miaka 88 amefanya ziara hiyo ya kigeni ya nadra na viongozi wengine wa dunia Rais Barack Obama wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi watakula kwa pamoja chakula cha mchana kabla ya kuelekea kwenye fukwe hizo kwa ajili ya hafla hiyo ya taadhima ya kimataifa inayoandamana na ibada.

Ushiriki wa mwisho kwa maveterani

Maveterani 1,800 wa kutoka Uingereza,Marekani,Ufaransa, Canada na hata Urusi na Poland wanatowa heshima zao kwa maelfu ya wapiganaji wenzao waliouwawa katika siku hiyo ya D-Day wengi wao watakuwa wanashiriki katika kumbukumbuku hiyo kwa mara ya mwisho kwa kuzingatia umri wao ambao ni mkubwa.

Maveterani walioshiriki mapambano ya "D-Day" wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya vita hivyo huko Normandy Ufaransa.(06.06.2014)
Maveterani walioshiriki mapambano ya "D-Day" wakati wa kumbukumbu ya miaka 70 ya vita hivyo huko Normandy Ufaransa.(06.06.2014)Picha: Damien Meyer/AFP/Getty Images

Wengi wa maveterani hao wamevalia sare zao za kijeshi zenye kuonyesha medali katika kumbukumbu hiyo.

Hafla za sherehe na kumbukumbu hiyo zitawapa viongozi wa dunia walioko kwenye mfarakano dhamira ya pamoja ya aina yake lakini mzozo wa kidiplomasia wa malumbano mabaya kabisa baina ya mataifa ya magharibi na mashariki kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulizidi kupamaba moto hapo hapo jana na unategemewa kuendelea wakati wote wa hafla hizi.

Kiwingu cha mzozo wa Ukraine

Putin amekuwa kwenye mkwamo mzito wa kidiplomasia tokea Urusi ilipoinyakuwa Crimea hapo mwezi wa Machi na kuwa na mkutano wake wa kwanza na viongozi wa mataifa ya magharibi tokea wakati huo kwa kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi huko Deauville kaskazini mwa Ufaransa. (06.06.2014)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi huko Deauville kaskazini mwa Ufaransa. (06.06.2014)Picha: Reuters

Hollande aliharakisha chakula chake cha jioni na Obama hapo jana kabla ya kukutana na Putin wakati wa chakula chengine cha usiku katika Kasri la Elysee.

Cameron amesema amemfahamisha Putin juu ya madai ya mataifa ya magharibi kuhusiana na suala la Ukraine kwa kile alichokielezea kuwa ulikuwa ni mkutano uliokuwa wazi wenye ujumbe thabiti.

Cameron amesema Urusi inatakiwa itambuwe fika ujumbe huo na kushikiana na rais mpya wa Ukraine ambapo kunahitajika kupunguza hali ya mvutano na kuzuwiya kupeleka silaha na watu nchini Ukraine.Amesema hali iliopo hivi sasa inabidi ibadilike.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani tayari amekutana na Putin leo hii lakini Rais Barack Obama wa Marekani hatarajiwi kuwa na mkutanio rasmi na Putin.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman