1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hiroshima mji wa amani

6 Agosti 2015

Walimwengu wameikumbuka miaka 70 tangu bomu la kwanza la kinyuklia kudondoshwa Hiroshima, kisa kilichoilazimisha Japan kusalim amri na kumalizika vita vikuu vya pili vya Dunia.

https://p.dw.com/p/1GB0H
Familia za wahanga wanaweka mashada ya mauwa mbele ya bustani ya kumbukumbu za amaniPicha: Getty Images/AFP/Jiji Press

Maelfu wamekusanyika katika bustani ya kumbukumbu za amani katika mji huo wa Hiroshima wenye wakaazi milioni moja na laki mbili, magharibi mwa Japan-mji unaoangaliwa kama kitambulisho cha wapenda amani.

Watoto,wazee walionusurika na wajumbe kutoka mataifa 100, akiwemo balozi wa Marekani nchini Japan Caroline Kennedy na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya kudhibitiwa silaha, Rose Gottemoeller ni miongoni mwa umati wa watu waliohudhuria kumbukumbu hizo.

Mashada ya mauwa yamewekwa mbele ya bustani ya amani huku njiwa wakipeperushwa hewani.

Kengele zilihanikiza dakika ile ile ndege ya kivita ya Marekani chapa B-29 iliyopewa jina Enola Gay, ilipodondosha bomu la urani na kuripuka janga la moto na mauti katika mji huo.

"Tukiwa nchi pekee iliyowahi kushambuliwa kwa bomu la nuklea,waajibu wetu ni kubuni ulimwengu bila ya silaha za nuklea"-amesema waziri mkuu wa Japan Shin zo Abe mbele ya umati wa watu katika kumbu kumbu hizo.

Nae meya wa Hiroshima Kazumi Matsui akashadidia kwa kusema:"Ili tuweze kuishi pamoja tunabidi kukomesha matumizi ya silaha zote za nuklea-chanzo cha maovu ambayo si ya kibinaadam.Na wakati wa kulifikia lengo hilo ni huu."

Mswaada wa azimio dhidi ya silaha za nuklea kufikishwa katika Umoja wa Mataifa

Japan inapanga kuwasilisha mswaada wa azimio mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa mataifa, baadae mwaka huu kutaka silaha za nuklea zipigwe marufuku.

Japan Hiroschima Abwurf Atombombe 1945
Bomu la nuklea lililoporomoshwa Agosti 6 mwaka 1945 HiroshimaPicha: U.S. Army/Hiroshima Peace Memorial Museum via Reuters

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anaehudhuria mkutano wa kikanda katika nchi jirani ya Malaysia amelitaja shambulio la kinuklea dhidi ya hiroshima kuwa "kumbusho kubwa la madhara ya kudumu ya vita kwa binaadam na kwa nchi pia."

Watu laki moja na 40 elfu wanasemekana waliuwawa katika shambulio hilo la bomu mjini Hiroshima, wakiwemo wale walionusurika kwanza na kufariki dunia siku, wiki au miezi michache baadae kutokana na mionzi ya nuklea.

Madhara ya nuklea mpaka leo yanakutikana Hiroshima

Shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu limesema hii leo hospitali bado mpaka leo hii zinawatibu maelfu ya wahanga walionusurika na shambulio la bomu hilo la nuklea.

Japan Hiroschima Zeremonie Gedenkfeierlichkeiten 70 Jahre Abwurf Atombombe
Bustani ya kumbu kumbu za amani ambako walimwengu waliikumbuka miaka 70 tangu Marekani ilipodondosha bomu la nuklea huko Hiroshima nchini JapanPicha: Getty Images/C. McGrath

Agosti tisa bomu jengine la nuklea la Marekani lilipodondoshwa karibu na mji wa bandari wa Nagasaki,watu 70 elfu waliuliwa.

Mashambulio hayo mawili ya mabomu ya nuklea ndio chanzo cha kusalim amri Japan Agosti 15 mwaka 1945 na kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga