Miaka 65 baada ya maangamizi ya wayahudi - HOLOCAUST | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.01.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Miaka 65 baada ya maangamizi ya wayahudi - HOLOCAUST

Maadhimisho ya ukombozi wa kambi ya AUSCHWITZ ambapo mafashisi waliwaangamiza wayahudi-HOLOCAUST, miaka 65 iliyopita.

Rais wa Israel Shimon Peres akihutubia bunge la Ujerumanii.

Rais wa Israel Shimon Peres akihutubia bunge la Ujerumanii.

Rais Shimon Peres wa Israel leo amesema kwamba wote waliotenda uhalifu wa kifashisti lazima waadhibiwe.

Rais Peres amesema hayo katika hotuba aliyoitoa kwenye bunge la Ujerumani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kukumbuka kukombolewa kwa kambi Auschwitz ambapo mafashisti walitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu miaka 65 iliyopita.

Katika hotuba yake, rais Peres amesema wote waliotenda uhalifu wakati wa utawala wa mafashisti lazima wafikishwe mbele ya sheria.

Bwana Peres aliwaambia wabunge wa Ujerumani kwamba maangamizi ya wayahudi-Holocaust - ni onyo la daima na wakati huo huo yanawapa binadamu wajibu wa kuutukuza uhai.

Rais Peres amesema watu walioshiriki katika kutenda uhalifu huo mkubwa-Holocaust- bado wanaishi Ujerumani, katika nchi nyingine za Ulaya na katika sehemu zingine za dunia.

Amewataka wabunge wa Ujerumani wafanye kila wanaloweza ili wahalifu hao wafikishwe mbele ya sheria.

Ameeleza kwamba mwito wake siyo kitendo cha kulipiza kisasi, bali ni funzo.

Siku kama ya leo, miaka 65 iliyopita, muda mfupi kabla ya kumalizika vita kuu vya pili, askari wa kisoviet -Urusi ya zamani , walifika kwenye kambi ya Auschwitz ambapo wahalifu wa kifashisti walifanya maangamizi. Askari hao walifika kwenye kambi hiyo nchini Poland baada ya watu zaidi ya milioni moja kuangamizwa.

Naye akizungumza katika kuadhimisha mwaka wa 65 tokea kukombolewa kwa watu waliokuwamo katika kambi ya Auschwitz, Spika wa bunge la Ujerumani, Nobert Lammert, aliirudia tena ahadi ya Wajerumani, juu ya kutosahau yaliyotokea.

Amesema wajerumani wataendelea kutekeleza wajibu wa kupambana kwa uthabiti wote,na aina zote za chuki, ubaguzi, na chuki dhidi ya Wayahudi.

Bwana Lammert, amesema kwa Ujerumani, kuendelea kuwapo kwa Israel, siyo suala la majadiliano. Amesisitiza kwamba Ujerumani ina wajibu kwa Israel.

27.01.2010 dw-tv journal tt ausschwitz Schimon Peres Horst Koehler 1

Marais Shimon Peres wa Israel na mwenyeji wake Horst Köhler.

Katika maadhimisho yaliyofanyika bungeni kuwakumbuka wahanga wa uhalifu wa mafashisti, pia walishiriki Kansela Angela Merkel na rais wa Ujerumani, Horst Köhler.

Siku ya leo ya kukumbuka kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz inaadhimishwa pia kwenye kambi hiyo ya zamani nchini Poland ambapo watu zaidi ya milioni moja , na hasa wayahudi waliangamizwa na mafashisti wakati wa vita kuu vya pili.

Mwandishi/Mtullya Abdu/DPAEIEPD/LPD/ZA.

Mhariri: Miraji Othman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com