1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 60 ya kutiwa saini makubaliano ya Geneva

Saumu Ramadhani Yusuf28 Julai 2011

Wakimbizi bado wanateseka duniani.Umoja wa Mataifa unasema kuna wakimbizi 43 millioni kote duniani mpaka mwaka 2010

https://p.dw.com/p/125QO
Wakimbizi wa ndani nchini Uganda eneo la KaskaziniPicha: picture-alliance/dpa

Ni miaka 60 leo tangu kutiwa saini makubaliano ya Geneva juu ya kuwalinda wakimbizi duniani.Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi duniani linasema kwamba kuna wakimbizi zaidi ya millioni 43 kote duniani kutokana na hali ya vita,njaa na matatizo mengine ya kibinadamu.Aidha Kamishna mkuu anayehusika na masuala ya wakimbizi katika Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaka jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhisho la kudumu kumaliza tatizo la wakimbizi duniani.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi UNHCR limetangaza kwamba hadi mwaka 2010 idadi ya wakimbizi imefikia watu millioni 43 wengi wakitokea katika nchi za Iraq,Pakistan,Somalia,na maeneo ya Afrika Kaskazini.Tatizo hilo linazidi kuumiza vichwa vya watunga sera katika jumuiya ya Kimataifa hasa ikizingatiwa kwamba wengi wanakimbilia katika nchi za Ulaya na Marekani kuomba hifadhi ya ukimbizi.

Hali ya wakimbizi wakisomali huko nchini Kenya inazidi kutia wasiwasi hasa kutokana na tatizo hilo kupata makali zaidi kufuatia janga la ukame na njaa katika eneo hilo zima la pembe ya Afrika.hivi karibunikamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya kibinadamu Kristalina Geogieva aliilaumu jumuiya ya Kimataifa kwa kutochukua hatua za kutosha katika kujiandaa na majanga ya kiasili kutokana na kinachoshuhudiwa huko Afrika Mashariki.

Aliongeza kusema kwamba janga la njaa na ukame katika pembe ya Afrika ni funzo kwa jumuiya ya Kimataifa kwamba inabidi kuwekeza katika kupambana na majanga aina hiyo.Akitolea mfano alisema ni bora kutoa yuro tano kujiandaa kuzuia baa la njaa kuliko kutoa yuro 200 wakati janga limeshazagaa.Kamishna huyo wa Umoja wa Ulaya pia aliweka wazi kwamba hali ya kisiasa nchini Somalia inabidi kushughulikiwa ili kuepusha matatizo zaidi miongoni mwa jamii.Mtazamo kama huo pia umezungumziwa kwa jumla na Antonio Guterres akisema kwamba ili kulitatua suala la wakimbizi duniani jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushughulikia kwamba migogoro ya kisiasa.

Lybien Choucha Flüchtlinge Flash-Galerie
Kambi ya Choucha nchini Tunisia inayowahifadhi wakimbizi wa LibyaPicha: Gaia Anderson

Katika kuadhimisha miaka 60 tangu kutiwa saini makubaliano ya Geneva juu ya kuwalinda wakimbizi shughuli mbali mbali zimendaliwa kote duniani na mashirika yanayohusika katika kuwalinda wakimbizi duniani ikiwemo UNHCR. Mikutano mbali mbali inafanyika juu ya suala hilo.Mjini Brussels kwa mfano kunafanyika mkutano unajadili kuhusu mfumo wa pamoja wa kushughulikia uombaji wa hifadhi ya ukimbizi barani Ulaya,mfumo unaojulikana kama CEAS. Mkutano zaidi unajikita kuangalia mafanikio na mapungufu yanayotokana na mfumo huo katika kuwalinda wanaoomba hifadhi ya Ukimbizi barani  barani Ulaya.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri AbdulRahman.